1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa UN aelekea Korea Kusini

5 Desemba 2017

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa umeelekea Pyongyang kwa ziara isiyo ya kawaida, kwa lengo la kujaribu kuuzima mvutano kati ya taifa hilo na Marekani kufuatia mpango wa silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini

https://p.dw.com/p/2omLb
Nordkorea Kim Jong Un bei Besuch einer Fabrik für Nuklearwaffen
Picha: Reuters/KCNA

Mvutano mkali unaoendelea kati ya Marekani na Korea kaskazini kutokana na mpango wake wa silaha za nyuklia unaendeleza hali ya wasiwasi katika eneo la Korea na duniani kwa ujumla. Kutokana na hali hiyo, umoja wa mataifa umetuma ujumbe wake kwenda Korea kaskazini kujaribu kutuliza hali.

Jeffrey Feltman - mshauri wa umoja wa mataifa katika maswala ya kisiasa
Jeffrey Feltman - mshauri wa umoja wa mataifa katika maswala ya kisiasaPicha: picture-alliance/Pacific Press/A. Lohr-Jones

Ziara ya Jeffrey Feltman – mshauri wa umoja wa mataifa anayehusika na masuala ya kisiasa, ni ya kwanza kufanywa na mwanadiplomasia wa cheo cha juu wa umoja huo tangu mwaka 2010. Haya yanajiri siku chache baada ya Korea Kaskazini kusema imefanikiwa katika jaribio la kombora jipya linaloweza kufikia Marekani.

Ziara hii pia inakuja siku moja baada ya Marekani na Korea kusini kuanza mazoezi ya pamoja na  kijeshi, kuonyesha utayarifu wa kukabiliana na kitisho cha Korea kaskazini.

Mnamo siku ya Jumatatu, Feltman, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kisiasa, aliwasili nchini China ambako alikutana na makamu waziri wa maswala ya kigeni wa China mjini Beijing.

China, ambayo ni mshirika wa pekee wa kidiplomasia na kijeshi wa Korea Kaskazini, imetoa wito kwa Marekani kusitisha mazoezi hayo kijeshi,na kuitaka pia Korea ya Kaskazini isitishe majaribio ya makombora ili kutuliza hali  hiyo tete.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric alisema, akiwa Korea Kaskazini Feltman  atajadili juu ya  "maswala ya maslahi ya pamoja na yenye umuhimu zaidi" na viongozi wa taifa hilo la kikomunisti pamoja na kukutana na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jung-Un.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeliwekea taifa hilo lililotengwa la Korea kaskazini, vikwazo zaidi  kufuatia kuendeleza majaribio yake ya makombora na silaha za nyuklia ambayo yameitia wasiwasi Marekani na washirika wake Korea Kusini na Japan.

Nordkorea Raketentest
Kombora lililofyetuliwa na Korea KaskaziniPicha: picture-alliance/AP Photo/KCNA

Korea kaskazini ilisababisha wasiwasi mkubwa zaidi kwenye eneo la Korea siku tano zilizopita wakati ilipotangaza ufanisi wa jaribio la kombora jipya, ambalo inasema linaweza kuipiga Marekani.

Katika miaka ya hivi karibuni, Korea Kaskazini imeongeza juhudi zake na kuwekeza katika teknolojia ya nyuklia na makombora, huku Marekani ilishutumu taifa hilo kwa uadui.  Vita vya maneno makali vimekuwa zikiendelea baina ya Rais Donald Trump wa Marekani na Kiongozi wa Korea Kasakazini Kim Jong Un.

Katika uhariri mpya Jumanne, vyombo vya habari vya Korea kaskazini viliishtumu muungano wa pamoja wa Marekani na Korea Kusini wa utayarifu wa kukabiliana na kitisho cha taifa hilo na kuutaja kujiingiza katika moto utakaowaunguza.

Mwishoni mwa juma lililopita, mshauri wa usalama wa Taifa wa Trump HR McMaster aliliambia kongamano la usalama kuwa uwezekano wa vita na Korea Kaskazini "unakuwa kila siku."

Lakini washauri wengine wa Trump wanasema chaguo la hatua ya kijeshi ya Marekani ni dogo wakati Korea kaskazini  inaweza kuushambulia  mji mkuu wa Korea Kusini – ulio ukaribu ,kilomita 50 kutoka mpaka uliozingirwa vilivyo kwa nguvu za kijeshi na eneo la makaazi kwa  watu milioni 10.

Bunge la  Japan jumatatu liliutaja mpango wa silaha za nyuklia wa Korea kaskazini kama tishio la karibu. Kombora lililofyatuliwa wiki iliopita liliingia katika sehemu ya bahari ya Japan.

Wizara ya mambo aya  nchi za kigeni ya China ilionya kwamba hali hiyo inabakia kuwa swala nyeti na kuzitaka pande zote kufanya kila ziwezalo kupunguza mvutano na kujiepusaha na  uchochezi.

Mwandishi: Fathiya Omar/AFPE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman