1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Tripoli wakabiliwa na uhaba mkubwa wa mahitaji muhimu

29 Agosti 2011

Baraza la mpito la waasi wa Libya limesema mji wa Tripoli unakabiliwa na uhaba mkubwa wa mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na chakula, dawa na nishati. Huku waasi wakigundua uovu zaidi wa majeshi ya Gaddafi.

https://p.dw.com/p/12PET
Wakazi wa Tripoli wakiwa wanatafuta za majiPicha: dapd

Msemaji wa Baraza la Mpito la waasi wa Libya ameeleza kuwa watu katika mji Mkuu wa Libya, Tripoli hawana chakula, maji wala mafuta ya petroli. Kutokana na hali hiyo msemaji huyo bwana Ben Ali ametoa mwito kwa madaktari wote wa Libya wanaofanya kazi nchi za nje warejee nyumbani haraka. Ameeleza kuwa hali ni mbaya sana kwenye hospitali.

Wakati huo huo waasi wanazidi kugundua ushahidi wa ukatili uliotendwa na utawala uliopinduliwa wa Kanali Gaddafi.

Bürgerkrieg in Libyen Erfolg der Rebellen
Waandishi wa habari wakiwa TripoliPicha: dapd

Waandishi wa habari wanazungumzia juu ya wafungwa wa kiraia na watu waliouliwa katika siku za mwisho za utawala wa Gaddafi.

Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch likiwakariri watu walioshuhudia limearifu kwamba wafuasi wa Gaddafi wamewauwa raia ambao hawakuwa na njia yoyote ya kujitetea. Raia hao ni pamoja na wafungwa.

Waandishi wa habari wameripoti kwamba, wafuasi wa Gaddafi waliwaua wafungwa hao baada ya kubaini kwamba hawakuwa tena na uwezo wa kupambana na waasi.

Wakati huo huo uhaba wa mahitaji muhimu umezidi kuwa mkubwa katika mji wa Tripoli. Mtu mmoja amesema "Hakuna chakula kabisa na shughuli zote za biashara zimefungwa. Watu wanakimbia hapa"

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon watu milioni tatu nchini Libya wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa mahitaji muhimu. Katika mji wa Tripoli hakuna maji licha ya joto kali linalofikia nyuzi joto 30 hata kivulini.

Huduma ya umeme pia imekatika kwa kiwango kikubwa. Na hata majenereta hayana dizeli.

Lakini Baraza la mpito limeahidi kuirekebisha hali hiyo haraka. Baraza hilo limesema mahitaji ya dizeli, maji na umeme yapo njiani yanapelekwa mjini Tripoli.

Kijana mmoja amewaambia waandishi wa habari kwamba vijana watasimama mstari wa mbele katika kuikabili hali mbaya inayoikabili nchi yao "Vijana wa Libya wataijenga upya nchi yao. Vijana ndiyo mustakabal wa Libya na siyo mtoto wa Gaddafi Seif al Islam."

Wakati akiyasema hayo kijana huyo alikuwa analitumia shati la Gaddafi kuvipangusia viatu vyake.

Msemaji wa Baraza la Mpito amefahamisha kwamba baadhi ya mabomba ya gesi yameanza kufanya kazi na juhudi zinafanyika ili kuirejesha hali ya kawaida katika mji wa Tripoli na nchini Libya kote.

Lakini pamoja na juhudi hizo mapambano yanaendelea. Waasi sasa wanajitayarisha kuingia katika mji wa uzawa wa Kanali Gaddafi wa Sirte uliopo umbali wa kilometa 360 mashariki ya mji mkuu Libya. Waasi wanaosaidiwa na ndege za NATO wamesemaa kuwa sasa wanakaribia kuingia katika mji huo. Hata hivvyo mpaka sasa hakuna habari zozote juu ya mahala ambapo Kanali Gaddafi anajificha.

Mwandishi/Wegerhoff,Cornelia/ARD/ZDF
Tafsiri/Mtullya Abdu
Mhariri/Josephat Charo