1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mizozo mipya yadhoofisha vita vya Bush

Marekani,ikidai kuwa hatimae imeanza kufanikiwa katika vita vyake dhidi ya ugaidi nchini Irak, sasa yajikuta ikikabiliwa na mizozo mipya katika maeneo ya vita hivyo:-kuanzia Pakistan,Uturuki na hadi katika Pembe ya Afrika.

Hali ya hatari iliyotangazwa mwishoni mwa juma lililopita na Rais wa Pakistan Jemadari Pervez Musharraf,kitisho cha Uturuki kuwashambulia Wakurdi kaskazini mwa Irak na uwezekano wa kuzuka vita kati ya Eritrea na Ethiopia inayoungwa mkono na Marekani ni mambo yanayodhihirisha kuwa Washington imekuwa muhanga wa serikali na viongozi wasioeleweka wala kuweza kudhibitiwa.

Ukweli kuwa Waziri wa Nje wa Marekani,Condoleezza Rice hakuwa na uwezo mwingine isipokuwa kuwapigia simu viongozi wa nchi kutekeleza matakwa ya Marekani: yaani Uturuki kutovamia eneo la Wakurdi kaskazini mwa Irak;na Musharraf kutotangaza hali ya hatari umesisitiza kwa umbali gani dola kuu pekee duniani limepoteza nguvu za ushawishi wake.

Lakini miongoni mwa migogoro hiyo mitatu mipya,hali ya mpakani Uturuki na kaskazini mwa Irak inahatarisha zaidi juhudi za Marekani kuleta utulivu nchini Irak.Kwa hivyo maafisa wa Kimarekani wa ngazi za juu wanatumaini kuwa ziara iliyofanywa hivi karibuni na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mjini Washington,itasaidia kuwatuliza makamanda wa kijeshi na viongozi wa upinzani nchini Uturuki,wanoitaka serikali ichukuwe hatua ya kijeshi dhidi ya waasi wa Kikurd kaskazini mwa Irak.Erdogan,wakati wa ziara yake nchini Marekani aliahidiwa na Rais George W.Bush ushirikiano zaidi kupambana na wanamgambo wa Kikurd wa chama cha PKK ambao wana vituo vyao kaskazini mwa Irak.

Hofu ya wachambuzi wa kisiasa ni kwamba Uturuki ikichukua hatua ya kijeshi,wanamgambo wa Kiiraki wenye asili ya Kikurd huenda wakajaribu kuzuia uvamizi huo.Na Washington inawategemea Wairaki hao wa Kikurdi kuhifadhi usalama na utulivu kaskazini mwa Irak na vile vile kulipatia jeshi jipya la Irak wakuruti wanaoaminika.Wakati huo huo,Uturuki ni mshirika wa karibu wa NATO na Marekani inaruhusiwa kutumia anga ya Uturuki kusafirisha zana muhimu kwa majeshi yake nchini Irak.

Hatari nyingine kubwa imezushwa na tangazo la hali ya hatari nchini Pakistan.Nchi hiyo imekuwa kiini cha vita dhidi ya ugaidi tangu wanamgambo wa Al-Qaeda na Wataliban kutimiliwa Afghanistan mwaka 2001 na kukimbilia sehemu za mpakani za nchi jirani.

Kwa upande mwingine mgogoro wa hivi sasa kwenye Pembe ya Afrika haupewi kipaumbele kama mizozo ya Uturuki na Pakistan.Lakini kundi linaloshughulika na mizozo ya kimataifa-ICG limeonya kuwa eneo hilo pia linazidi kukabiliwa na kitisho kikubwa. Ikiwa jumuiya ya kimataifa na hasa Marekani hazitochukua hatua,kuna uwezekano wa kuzuka vita vipya kati ya Ethiopia na Eritrea.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com