1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yavunja serikali za mitaa

Mohamed Abdulrahman28 Juni 2011

Mahakama Kuu ya Utawala nchini Misri imeamuru kuvunjwa kwa mabaraza ya serikali za mitaa, ambayo wawakilishi wake walichaguliwa chini ya utawala wa rais aliyeondolewa madarakani Hosni Mubarak.

https://p.dw.com/p/11kll
Waandamanaji kwenye uwanja wa Tahriri baada ya mapinduzi ya umma
Waandamanaji kwenye uwanja wa Tahriri baada ya mapinduzi ya ummaPicha: picture alliance / dpa

Hayo yamethibitishwa na afisa mmoja wa mahakama hiyo, amesema kuwa amri hiyo inafuatia pingamizi kadhaa za kisheria zinazoshutumu madiwani kutoka chama cha Mubarak cha National Democratic (NDP), ambacho hivi sasa kimevunjwa.

Wanaharakati wanaopigania demokrasia zaidi, ambao walianzisha vuguvugu lililoleta mapinduzi yaliyomaliza utawala wa miaka 30 wa Mubarak, wamekuwa wakishinikiza kuvunjwa kwa mabaraza hayo ya serikali za mitaa ambayo wanasema yamezama katika rushwa.

Katika uchaguzi wa mwisho wa serikali za majimbo mwaka 2008, ambapo ulishuhudia idadi ndogo sana ya wapiga kura, NDP ilijizolea 99% ya kura.

Hatimaye Bashir atua China

Rais Omar al-Bashir of Sudan (kushoto) akimkaribisha Rais Hu Jintao mjini Khartoum
Rais Omar al-Bashir of Sudan (kushoto) akimkaribisha Rais Hu Jintao mjini KhartoumPicha: AP

Rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir, amewasili Beijing mapema leo asubuhi ikiwa ni karibu saa 24 kuliko ilivyotarajiwa, baada ya ndege yake kulazimika kuruka kupitia anga ya Pakistan na kuepuka anga ya Turkimenistan.

Gazeti moja la Sudan, Tribune, limezinukuu duru za kibalozi zikisema kuwa huenda Turkmenistan ilishinikizwa na nchi za Magharibi kuizuwia ndege hiyo, endapo ingepita kwenye anga yake, kwa minajili ya kumkamata Bashir ambaye anatakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kujibu mashitaka ya uhalifu wa kivita.

Hata hivyo, Turkemistan haijasaini Mkataba wa Roma, ambao ungeilazimisha kumkamata Bashir kwa mujibu wa sheria za ICC.

Kiongozi huyo wa Sudan anatakiwa na mahakama hiyo kujibu mashitaka ya uhalifu wa kivita, mauaji na maovu dhidi ya binaadamu katika jimbo la magharibi mwa nchi hiyo la Darfur.

Huko mjini Beijing, wizara ya mambo ya nchi za nje ya China imesema Rais Bashir atakuwa na mazungumzo na Rais Hu Jintao na viongozi wengine wa China, juu ya masuala yanayozihusu nchi zao mbili, mchakato wa amani unaoendelea kati ya Kaskazini na Kusini mwa Sudan na pia suala la Darfur.

Rais wa Nigeria ateua baraza jipya la mawaziri

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria
Rais Goodluck Jonathan wa NigeriaPicha: AP

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amewasilisha majina 34 kwa ajili ya baraza lake jipya la mawaziri ili yaidhinishwe na Baraza la Seneti la nchi hiyo.

Katika majina hayo wamo waziri wa zamani wa mafuta, Deziani Alison-Madueke, na waziri wa zamani wa fedha, Olusegun Aganga.

Rais wa Baraza la Seneti, David Mark, amesoma orodha hiyo ya majina, ambayo haikujumuisha nyadhifa za mawaziri hao kwa baraza hilo la bunge la Nigeria leo.

Rais Jonathan anatarajiwa kutuma orodha nyingine ya majina ili kukamilisha kundi la serikali yake baadaye.

Jeshi laimarisha ulinzi Senegal

Rais wa Senegal, Abdoulaye Wade
Rais wa Senegal, Abdoulaye WadePicha: picture-alliance/dpa

Serikali ya Senegal imeweka vikosi zaidi vya jeshi katika majengo ya wizara mbali mbali, magari ya deraya karibu na ikulu ya rais pamoja na helikopta moja yenye silaha katika mji mkuu, Dakar, baada ya ghasia kuzuka kutokana na ukosefu wa muda mrefu wa umeme.

Nyumba za watu na sehemu nyingi za kibiashara mjini Dakar zimekuwa haina umeme kwa zaidi ya saa 30 sasa, jambo lililosababisha hasira kali dhidi ya serikali.

Usiku wa kuamkia leo, waandamanaji walichoma matairi na kuharibu ofisi za Shirika la Umeme na nchi hiyo (Senelec) pamoja na nyumba ya waziri wa mambo ya ndani.

Ghasia zilizuka wiki iliyopita baada ya Rais Abdoulaye Wade kujaribu kubadilisha katiba ili kumrahisishia kuweza kuchaguliwa tena mwezi Februari.

Senegal imejipatia sifa kuwa nchi yenye amani na demokrasia katika mataifa ya Afrika Magharibi, lakini imeshuhudia kuporomoka sana kwa huduma za jamii, hususan katika sekta ya umeme, tangu Wade alipochukua madaraka mwaka 2000.