1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Misri yaongeza vikosi rasi ya Sinai

Jeshi la Misri limepeleka vikosi vingine katika rasi ya Sinai kupambana na wanamgambo wa Kiislamu huku viongozi wa kabila la mabedui wakiahidi kuunga mkono operesheni hiyo.

Vifaru vya jeshi la Misri vikipakizwa katika magari kuelekea rasi ya Sinai.

Vifaru vya jeshi la Misri vikipakizwa katika magari kuelekea rasi ya Sinai.

Magari ya kijeshi yakiwa yamebeba zana za kivita yalionekana katika mji wa El-Arish yakielekea upande wa mashariki ambapo wanamgambo wa kiislamu kutoka kabila la mabedui wameweka kambi katika vijiji vilivyoko karibu na mpaka wa ukanda wa Gaza.

Hatua hii ya jeshi la Misri inakuja baada ya televisheni ya taifa kuripoti kuwa helikopta za jeshi na wanajeshi wa Misri waliwaua wanamgambo 20 siku ya Jumatano katika operesehni ya kwanza ya namna hiyo katika miongo kadhaa, kufuatia mauaji ya wanajeshi 16 na wanamgambo hao.

Rais wa Misri Mohamed Mursi.

Rais wa Misri Mohamed Mursi.

Israel ilisema siku ya Alhamis kuwa ilitoa ruhusa kwa serikali ya Misri kutumia ndege katika rasi ya Sinai, na hivyo kulegeza vikwazo vya kutopelekwa wanajeshi katika eneo hilo vinavyobainishwa na mkataba wa amani kati ya nchi hizo mbili, uliosainiwa mwaka 1979.

Viongozi wa kikabila wataka kuona miili ya waliouawa
Katika mkutano uliofanyika usiku wa manane na waziri wa mambo ya ndani wa Misri Ahmed Gamal al-Din mjini El-Arish, umbali wa kilomita 50 magharibi mwa mpaka wa Gaza, viongozi wa kabila la mabedui walitaka kuona miili ya wanamgambo waliouawa siku ya Jumatano.

Moja wa viongozi hao aliyeshiriki kikao hicho, Eid Abu Marzuka alisema wanataka kuona angalau mwili mmoja au miwili ili kujiridhisha. Wengine walionyesha wasiwasi wao juu ya ripoti ya kuuawa kwa wanamgambo hao, ambayo ilithibitishwa na kamanda moja wa kijeshi kutoka Sinai.

Viongozi hao wa kikabila walisema wamekubaliana kusaidiana na jeshi na polisi kurejesha usalama katika rasi hiyo na kufunga njia za chini ya ardhi zinazotumiwa kuingiza magendo na silaha katika ukanda wa Gaza wa Palestina. Marzuka alisema makabila yamekubaliana kuharibu njia hizo za chini, bila kujali kama hatua hii itawaudhi viongozi wa Hamas, na kuongeza kuwa Misri sasa itawashughulikia Wapalestina kupitia mpaka wa Rafa. Alisema wao wanapinga kufanya magendo lakini pia wanapinga vizuizi vilivyowekwa katika eneo hilo na Israel baada ya kutekwa na Hamas.

Rais wa Misri Mohamed Mursi.

Helikopta ya kivita ya Misri.

Waziri atumaini ushindi lakini changamoto zipo
Waziri wa mambo ya ndani alisema polisi na jeshi watawashinda wanamgambo hao kwa msaada wa watu wa makabila ya mabedui, ambao wakuwa na uadui na serikali ya Misri kwa madai kuwa inawabagua. Lakini Afisa moja mwandamizi wa usalama aliyeko Sinai alisema wanakabiliana na adui mwenye uzoefu na mazingira magumu ya eneo hilo lenye milima na jangwa.

Wakati huo huo, gazeti la serikali la Al-Ahram limeripoti leo kuwa watu wenye silaha waliwarushia risasi maafisa usalama katika kituo kimoja mjini El-Arish, ambao ndiyo mji mkuu wa mkoa wa Sinai Kaskazini. Maafisa hao wa usalama walijibu uvamizi huo lakini hakukuwa na taarifa za vifo au majeruhi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpa,afpe
Mhariri: Saum Yusuf