1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yamtimua balozi wa Qatar

Lilian Mtono
5 Juni 2017

Misri imetoa masaa 48 kwa balozi wa Qatar kuondoka nchini humo na kuwaita nyumbani wawakilishi wake waandamizi waliopo Doha. Hii ni kulingana na duru za wizara ya masuala ya kigeni ya Misri

https://p.dw.com/p/2e9NF
Ägypten Präsident al-Sisi
Picha: Getty Images/Afp/K. Desouki

Mwito huu unafuatia hatua ya mataifa kadhaa ya Kiarabu, kutangaza kukata ushirikiano wa kidiplomasia na Qatar.

"Balozi wa Qatar amerifiwa rasmi leo na kupewa taarifa rasmi za kumalizika kwa utambulisho wake kama balozi wa Qatar  nchini humo na kupewa masaa 48 ya kuondoka, imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa iliyotolewa awali na wizara hiyo ilisema Misri pia inasimamisha mahusiano ya anga na maji na Qatar, wakiangazia masuala ya usalama wa taifa kwa kufunga anga lake kutumiwa na ndege za Qatar. Mahusiano ya nchi hizo yamekuwa katika hali ya wasiwasi tangu jeshi lilipomuondoa madarakani aliyekuwa rais na mshirika wa Qatar, Mohamed Morsi mwaka 2013.  

Katar Doha Skyline
Baadhi ya maeneo ya Mji wa Doha, QatarPicha: Getty Images/M. Runnacles

Katika hatua nyingine, Kisiwa cha Maldives nacho kimekata mahusiano ya kidiplomasia na Qatar, kufuatia tuhuma kwamba inaunga mkono makundi ya Kiislamu. Imeungana na Bahrain, Misri, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu na kuanza kuondoa watumishi wake wa ubalozi. Duru za kibiashara zimearifu kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia zimesimisha kupeleka sukari nyeupe Qatar.

Uturuki na Iran zataka suluhu ya Kidiplomasia.

Taarifa ya wizara ya masuala ya kigeni imesema Maldives imetekeleza sera ya kuhamasisha amani na utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati na hatua hiyo imefikiwa kutokana na upizani wake thabiti dhidi ya shughuli zozote zonazohusiana na ugaidi.

Iran, yenyewe imesema kuongezeka kwa hali ya wasiwasi miongoni mwa mataifa jirani ya Kiarabu katika ukanda wa Ghuba kunatishia maslahi ya kila mmoja katika ukanda huo na kutaka njia ya kisiasa na mazungumzo kusaka suluhu.

Waziri wa masuala ya kigeni wa Iran, Bahram Ghasemi alinukuliwa katika tovuti ya wizara hiyo akitaka mazungumzo ya wazi miongoni mwa mataifa hayo yanayovutana kwa muda mrefu sasa.

Foadi Izadi, mchambuzi wa masuala ya kisiasa mwenye makao yake mjini Tehran anasema haoni sababu ya nchi yake kuingia kwenye mzozo na Qatar.

Türkei Referendum
Waziri Mkuu wa Uturuki, Mevlut Cavusloglu ametaka suluhu ya mazungumzoPicha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Uturuki pia imeeleza kusikitishwa na hatua hiyo na kutaka mazungumzo, kwa kuahidi kusaidia kurejesha tena mahusiano kati ya mataifa hayo. Waziri wa masuala ya kigeni wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu leo hii ametaka pande zinazokinzana kuanzisha mazungumzo ili kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani.

Huko nchini Libya, moja kati ya serikali tatu zinazounda serikali ya kitaifa nayo imetangaza kukata mahusiano yake ya kidiplomasia na Qatar. Kulingana na shirika la habari la serikali LANA, waziri wa masuala ya kigeni wa serikali ya mpito ya Libya Mohammed al-Deri pia ameituhumu Qatar kwa kuunga mkono ugaidi.

Aidha, shirikisho la soka duniani, FIFA limesema linafanya mawasiliano na kamati ya maandalizi ya kombe la dunia  linalotarajiwa kufanyika Qatar mwaka 2022, ingawa halikuzungumzia chochote kuhusu hali ya kidiplomasia katika mataifa ya Ghuba. 

Mwandishi: Lilian Mtono/Rtre/Ape
Mhariri: Iddi Ssessanga