1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yaiomba mahakama ya kimataifa isitishe mwaka mmoja hatua ya kumshitaki kiongozi wa Sudan.

11 Novemba 2008

Ni kulipa nafasi suluhisho la mzozo wa Darfur kwa njia ya mazungumzo.

https://p.dw.com/p/FrnP
Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir.Picha: AP

Misri leo imeitaka mahakama ya uhalifu ya kimataifa icheleweshe kwa kipindi cha mwaka mmoja , kumfungulia mashitaka yoyote Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan, wakati juhudi zikiendelea kumaliza mapigano katika jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri Ahmed AbulGheit alitoa atamko hilo baada ya ziara Rais Husni Mubarak inayoangaliwa kuwa ni ya nadra kufanywa na kiongozi wa Misri nchini Sudan jana Jumatatu ambapo pamoja na mwenyeji wake Rais Omar Hassan al-Bashir walizungumzia mzozo wa Darfur.

Waziri Abul Gheit katika kuitaka mahakama ya kimataifa isitishe hatua ya kumfungulia mashitaka ya uhalifu wa kivita kiongozi wa Sudan, aligusia juu ya kifungu kinachoruhusu kusitishwa uchunguzi juu ya uhalifu wa kivita kwa mwaka mmoja, kwa pendekezo la Baraza la usalama la Umoja wa mataifa. Akikaririwa na Shirika la habari la Misri MENA,Bw Geit akaongeza "katika muda huo tunaweza pamoja na Misri ,Afrika na jamii ya kimataifa kuleta upatanishi nchini Sudan."

Rais Bashir alishutumiwa mwezi Julai na mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya uhalifu ya kimataifa Luis Moreno-Ocampo,kuviamrisha vikosi vyake kuwaandama wakaazi wasio na asili ya kiarabu akatika jimbo la Darfur,kuandaa mauaji, mateso,ubakaji na safisha safisha ya kikabila. Hata hivyo hadi sasa hakuna waranti uliotolewa dhidi ya Rais Bashir.

Rais Mubarak wa Misri aliwaambia awaandishi habari wakati wa ziara yake nchini Sudan jana kwamba njia bora zaidi ya kuasaka suluhisho la tatizo hilo la Darfur ni juhudi za nchi za kiarabu na kiafrika .Rais huyo wa Misri anaunga mkono msimamo wa Umoja wa Afrika kwamba Bashir apewe muda wa kutekeleza usimamishaji mapigano katika jimbo hilo. na umoja huo na ule wa nchi za kiarabu, zimelitaka baraza la usalama kuchelewesha uamuzi wa mahakama ya kimataifa, kuhusiana na suala la kumfungulia rasmi mashitaka kiongozi wa Sudan.

Mwaka jana mahakama hiyo ya uhalifu ya kimataifa ICC ilitoa waranti wa kukamatwa Waziri mmoja wa Sudan Ahmed Haroun na Kiongozi wa wanamgambo Ali Kosheib kuhusika na uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur. Sudan imedai imemtia nguvuni Kosheib na itamfungulia mashitaka, lakini imesema hakuna msingi wowote wa kumshitaka waziri wake Haroun, au kumkabidhi kwa mhakama hiyo.

Kwa upande mwengine Qatar inapanga kuwa mwenyeji wa mazungumzo ya upatanishi kati ya mahasimu nchini Sudan baadae mwaka huu, lakini tayari kundi kubwa kabisa huko Darfur linalojiita chama cha haki na usawa, limeshasema halitashiriki ingawa litatuma mjumbe kama muangalizi.

Umoja wa mataifa unasema hadi watu 300.000 wamekufa na zaidi ya milioni 2.2 kuyahama makaazi yao tangu mzozo huo wa Darfur uliporipuka Februari 2003. Sudan kwa upande wake inasema waliouwawa ni watu 10.000 .