1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada ya kimataifa yaanza kuwasili Kenya

Oummilkheir6 Januari 2008
https://p.dw.com/p/Cl6V

Shehena ya mwanzo ya misaada ya umoja wa mataifa imewasili Kenya,kuwahui malaki ya watu walioyapa kisogo maskani yao kutokana na machafuko ya kisiasa.Misaada ya chakula itaanza kusambazwa katika mitaa ya mabanda mjini Nairobi na katika bonde la ufa mjini Eldoret.Akiba ya chakula na maji safi ya kunywa ni haba kupita kiasi hasa katika maeneo ya magharibi yanayouzunguka mji wa Kisumu” amesema mkurugenzi wa shirika moja lisilomilikiwa na serikali, WUBESHET WOLDERMARIAM,aliyetahadharisha dhidi ya hatari ya kuzuka kipindu pindu na maradhi mengine ya kuambukiza.Kwa upande wake-Sara Cameron wa shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia watoto UNICEF anazungumzia juu ya uhaba wa wauguzi na madawa kuweza kuwahudumiwa majeruhi katika hospitali kadhaa nchini Kenya.Tangu siku kadhaa shughuli za kusafirisha misaada ya chakula kuelekea magharibi ya Kenya zimekwama kutokana na ukosefu wa usalama-limesema kwa upande wake shirika la Umoja wa mataifa la mpango wa chakula linalokumbusha mzozo wa Kenya unaiathiri pia Uganda,eneo la mashariki la jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo na kusini mwa Sudan.