Miripuko yaua zaidi ya watu 200 Congo Brazzaville | Matukio ya Afrika | DW | 05.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Miripuko yaua zaidi ya watu 200 Congo Brazzaville

Miripuko mikubwa ilitokea jana jijini Brazzaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Congo, na kuua zaidi ya watu 200 huku zaidi ya 1,500 wakijeruhiwa.

majengo yaliyoathiriwa na miripuko

Majengo yaliyoathiriwa na miripuko

Miripuko hiyo ilitokea katika ghala ya kuhifadhia silaha na kubomoa nyumba nyingi jijini Brazaville, likiwemo kanisa kuu la Brazzaville ambapo misa ilikuwa ikiendelea. Katika maeneo mengine majengo yalitikiswa au vioo kupasuka. Athari za milipuko hiyo zilifika hadi Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemomkrasi ya Congo.

Bienvenue Okyemi, msemaji wa serikali ya Congo Brazzaville, ameeleza kwamba shoti ya umeme ndiyo iliyosababisha milipuko hiyo. Rais wa nchi hiyo, Denis Sassou-Nguesso, alizitembelea hospital zilnazowahudumia majeruhi wa milipuko hiyo na kusema kwamba serikali yake inafanya kila liwezekanalo ili kuokoa maisha ya majeruhi hao. Rais Okyemi aliongeza kuwa kambi zote za jeshi zilizomo jijini Brazzaville zitahamishiwa nje ya mji huo mkuu.

Maelfu kubaki bila maakazi

Msemaji wa shirika la Msalaba Mwekundu nchini Congo, Delphin Kibakidi, alieleza kwamba shirika lake limetengeneza kambi mbili katika makanisa yaliyopo jijini Brazzaville kwa ajili ya kuwahudumia majeruhi wapatao 600. "Tunakadiria kwamba mamia kwa maelfu ya watu wameachwa bila makaazi kutokana na nyumba zao kuharibiwa na miripuko," alisema Kibadiki. "Hivi sasa wapo wataalamu kutoka Urusi, Ufaransa na kutoka Congo wanaojaribu kuuzima moto uliozuka kutokana na miripuko. Lengo ni kuuzuia moto huo ili usiifikie ghala nyingine ambayo ni kubwa zaidi."

Shirika la habari la China, Xinhua News Agency, limeripoti kwamba miongoni mwa waliouwawa katika miripuko ya Brazzaville ni raia sita wa China waliokuwa wafanyakazi wa kampuni moja ya ujenzi. Wafanyakazi wengine wa shirika hilo walijeruhiwa.

Brazzaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Congo

Brazzaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Congo

Nchi mbalimbali zaahidi msaada

Serikali ya Congo imepokea salamu za rambirambi pamoja na ahadi ya kupewa misaada kutoka kwa nchi mbalimbali. Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, William Hague, alisema kwamba amesikitishwa sana na habari za maafa hayo. Nao ubalozi wa Marekani katika Jamhuri ya Congo umetoa tamko linalosema kwamba Marekani iko tayari kuisaidia Jamhuri ya Congo katika kuwasaidia wahanga wa maafa haya.

Mabalozi wa nchi mbalmbali, akiwemo balozi wa Ufaransa na wa Marekani, leo walikutana na maafisa wa serikali ya Jamhuri ya Congo kwa ajili ya kujadili namna ya kuendesha shughuli za uokozi. Juhudi hizo zilikwamishwa na miripuko iliyokuwa ikiendelea ambayo ilisababisha moto kutokea katika maeneo mbalimbali.

Sudi Mnette alizungumza na mwandishi wetu Saleh Mwanamilongo wa Congo Kinshasa ili kufahamu hali ilivyo jijini humo na huko Brazzaville. Mwanamilongo ameeleza kwamba miongoni mwa wale walioathirika na milipuko hiyo ni wanajeshi na vijana waliokuwa wakipewa mafunzo ya kijeshi.

(Bonyeza alama ya spika ya masikioni kusikiliza mahojiano baina ya Sudi Mnette na Saleh Mwanamilongo)

Mwandishi: Elizabeth Shoo/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Sauti na Vidio Kuhusu Mada