1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mipaka yafunguliwa Gaza

Ramadhani Yusuf, Saumu22 Januari 2008

Baada ya takriban siku nne za kufungwa mipaka katika ukanda wa Gaza, Israel imeamua kufungua mipaka yake miwili kwenye eneo hilo ili kuyawezesha mashirika ya kutoa misaada kuingia katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/CvtY
Maandamano ya wapalestina kufuatia vizuizi vya IsraelPicha: AP

Tayari malori yaliyobeba mahitaji muhimu ya kibinadamu na mafuta ya petroli yameruhisiwa kuingia eneo laGaza linalodhibitiwa na wanachama wa Hamas.


Israel imechukua hatua hiyo baada ya kuzidi kupata mashinikizo kutoka jumuiya ya kimataifa ifungue mipaka yake.



Israel imeyaruhusu malori yaliyobeba mahitaji muhimu ya kiutu kuingia ukanda wa Gaza leo hii baada ya nchi hiyo kufunga mipaka yake kwa siku nne kwa lengo la kukomesha mashambulio ya roketi aina ya Qassam yaliyokuwa yakifanywa na wanamgambo kutoka eneo hilo.


Israel pia imeruhusu usafirishaji wa mafuta ya Diesel katika mtambo pekee wa kusambaza umeme kwenye eneo hilo linalodhibitiwa na chama cha Hamas.


Hatua hii mpya ya Israel imekuja baada ya umoja wa mataifa na jumuiya ya kimataifa kwa jumla kuonya kwamba kufungwa kwa mipaka hiyo huenda kukasababisha matatizo makubwa ya kibinadamu kufuatia kufungwa kwa mtambo huo wa kusambaza nguvu za umeme.


Malori yalibeba vyakula na mahitaji mengine yalikubaliwa kupitia kusini mwa kivuko cha Kerem Shalom huku matanki ya mafuta yakiruhusiwa kuingilia upande wa Nahal Oz.


Tangu jumapili iliyopita wakaazi laki nane wa Gaza wamekuwa wakiishi katika giza totoro na hata wafanyikazi wa mahospitali walikuwa na matatizo ya kuwahudumia wagonjwa kukufuatia kufungwa kwa mtambo wao pekee wa kusambaza nguvu za umeme .


Kamishna wa umoja wa ulaya anayehusika na masuala ya nje Benita Ferrero Waldner aliikosoa hatua ya Israel ya kufunga mipaka yake akisema inasaidia tu kuzidisha hali ya mateso kwa watu wa Gaza.Aidha ni hali hiyo pia iliyolitia wasiwasi baraza la usalama la Umoja wa mataifa ambalo limeitisha kikao kujadili juu ya kuzorota kwa hali ya maisha katika eneo hilo.


Waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barack alitangaza kufunguliwa mipaka hiyo hapo jana jioni lakini akaonya kwamba Israel itaendelea kutia mbinyo dhidi ya wanamgambo katika ukanda wa Gaza wakomeshe mashambulio ya roketi ya kila siku kusini mwa Israel.

Ingawa wanamgambo wakipalestina leo asubuhi wamevurumisha tena roketi katika miji kadhaa na vijiji vya Israel vilivyo karibu na ukanda wa Gaza,

Jeshi la Israel linasema mbinyo wa siku nne zilizopita wa kijeshi na kiuchumi umepunguza sasa idadi ya mashambulio ya roketi chapa Qassam zilizokuwa zinafyatuliwa na wapalestina kutoka eneo hilo la Gaza.Hata hivyo mbinyo huo haujafurahikiwa na jumuiya ya kimataifa.

Hata hivyo Israel sasa imeuruhusu Umoja wa Ulaya kusafirisha mafuta ya petroli kiasi lita millioni 2.2 kila wiki katika Gaza ijapokuwa hali hiyo haijulikani itaendelea kwa muda gani kutokana na mivutano kati ya Israel na watawala wa Gaza yaani Hamas.Mashirika ya kutoa misaada pia yamefahamisha kwamba yataendelea kuifuatilizia hali ya mambo na kufanya kazi kwa mujibu wa hali ilivyo na pia huenda yakasimamishwa tena kupeleka misaada ikiwa wanamgambo wakipalestina wataendelea kufyatua roketi zaidi ndani ya Israel.