1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mike Pence akataa kumuondoa Trump madakarakani

13 Januari 2021

Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence amewaambia viongozi katika bunge la nchi hiyo kwamba haungi mkono mchakato wa marekebisho ya ibara ya 25 ya katiba ya Marekani ili kumuondoa madarakani Rais Donald Trump.

https://p.dw.com/p/3nqxs
US-Vizepräsident Pence
Picha: Susan Walsh/AP/dpa/picture alliance

"Zikiwa zimebaki siku nane tu katika muhula wa uongozi wa Rais Donald Trump, wewe na wabunge wa Democratic mnanitaka mimi na baraza la mawaziri kuitumia ibara ya 25 ya katiba ya Marekani," amesema Pence katika barua aliomuandikia spika Nancy Pelosi, akimaanisha mchakato ambao ungemtangaza Rais Donald Trump kutokuwa tena na uwezo wa kutekeleza majukumu yake na hivyo basi kumfanya Pence kama kaimu rais kwa muda uliosalia.

Soma pia: Trump, Pence waahidi kushirikiana kumaliza muhula wao

Pence amesema haamini kuwa huo ni uamuzi sahihi kwa faida ya Marekani au kuambatana na katiba ya nchi hiyo. Wabunge wa chama cha Democratic wamekubaliana kwa sauti moja kuanza mchakato wa kumuondoa madarakani Rais Trump baada ya kuwachochea wafuasi wake Jumatano iliyopita kuandamana hadi katika majengo ya bunge la Marekani na kupigania haki yao.

USA US-Vizepräsident Mike Pence und Donald Trump
Rais Trump akiwa na makamu wake Mike Pence.Picha: Carlos Barria/REUTERS

Uvamizi wa wafuasi hao ulisababisha vurugu na hali ya mshikemshike baada ya wafuasi hao kuonekana kuwazidi nguvu polisi na kuingia kwa nguvu ndani ya majengo ya bunge. Wafuasi hao aidha walitatiza kikao cha bunge kilichokuwa kinaendelea na kusimamisha mchakato wa kuthibitisha ushindi wa Rais mteule Joe Biden.

Pence ambaye alikuwa anasimamia kikao hicho cha bunge, pamoja na Pelosi na wabunge wengine walilazimika kujificha. Watu watano walifariki akiwemo afisa mmoja wa polisi katika ghasia hizo. Pelosi amesema uamuzi wa Pence unafungua njia ya kuandaliwa kwa kura ya kutokuwa na imani na Trump Jumatano.

Soma pia: Trump asema hatahudhuria kuapishwa kwa Biden

''Vitendo vya rais vinaonyesha wazi kuwa hana uwezo wa kutekeleza majukumu ya kimsingi ya ofisi yake. Kwa hivyo, rais lazima aondolewe ofisini mara moja. Kuondolewa kwa rais ni hatua ambayo huwa si kawaida, lakini inahitajika kwa sababu ya hali ilivyo sasa si kawaida pia. Hali hii itakuwa historia kwa sababu ya hatari aliyo nayo,'' amesema Pelosi.

Viongozi duniani walaumu uvamizi wa majengo ya bunge na seneti nchini Marekani

Hata hivyo, Pence ametetea uamuzi wake kwa kusema wito wa Pelosi kumtaka aitumie ibara ya 25 ya katiba ya Marekani ili kumuondoa madarakani Trump una nia mbaya na kuwa uamuzi huo haufai kuchukuliwa kama adhabu. Kwa upande wake, Rais Trump amesema hatishwi na hatua ya kutaka kumuondoa madarakani.

Chanzo: Mashirika