1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mikakati ya kusaka amani Uganda

Moahammed Abdu-Rahman6 Julai 2007

Wakaazi wa kaskazini wataka utolewe msamaha kwa waasi, licha ya maovu waliyoyafanya.

https://p.dw.com/p/CHBR
Kiongozi wa waasi wa Lord Resistance-LRA-nchini Uganda, Joseph Kony.
Kiongozi wa waasi wa Lord Resistance-LRA-nchini Uganda, Joseph Kony.Picha: AP Photo

Si jambo la kawaida kuona familia za watu waliouwawa katika eneo la migogoro, zikiziomba mahakama kuwasamehe wauaji. Lakini hayo yanatokea nchini Uganda ambako karibu kabila lote la waliopoteza jamaa zao katika mauaji na utekaji nyara watoto uliofanywa na waasi wa Lord Resistance nchini Uganda, wakitaka wahusika wasifikishwe mbele ya mahakama ya kimataifa.

Kiongozi wa kundi hilo la waasi la LRA aliye mafichoni Joseph Kony pamoja na wasaidizi wake watatu wakuu, wanatakiwa na mahakama ya jinai ya kimataifa mjini The Hague, wakikabiliwa na mashitaka ya mauaji, kuwakata watu viungo na kuwatumia watoto kama wapiganaji katika vita vyao. Lakini huko kaskazini mwa Uganda , ni wachache wanaotaka watu hao watupwe gerezani.

Walter Akena mwenye umri wa miaka 28 ambaye ni mkaazi katika kambi moja ya wakimbizi waliofikwa na maafa hayo ya vita kati ya LRA na majeshi ya serikali anasema, ni bora kumsamehe Kony kwa ajili ya amani akisisitiza kwamba msamaha hufungua njia ya maisha mapya na kuwaleta watu pamoja . Akena anasema kwa ajili ya amani, hana chuki wala hasira dhidi ya waasi pamoja na kwamba kaka zake wawili waliuwawa.

Mazungumzo kati ya serikali ya Uganda na waasi wa LRA yanaendelea katika mji wa Juba kusini mwa Sudan, ili kumaliza miaka 20 ya vita na wiki iliopita wali saini awamu katika mpango wa awamu tano wa kufikia amani. Vita hivyo vimesababisha watu milioni 1.7 kuyahama makaazi yao na janga hilo kugeuka moja wapo ya yake mabaya kabisa kwa binaadamu duniani.

Waasi wa LRA wamefanya vitendo vya kinyama wakiwakata watu midomo na masikio, kuwauwa, kuwateka nyara watoto na kuwatumia katika mapigano pamoja na vitendo vya ngono sawa na watumwa.

Takriban wakaazi wote wa kaskazini mwa Uganda–wote kutoka kabila la Acholi walilazimika kuwa wakimbizi katika kambi maalum ambako wengi walilalamika juu ya visa kadhaa vya kubughudhiwa vilivyofanywa pia na wanajeshi wa serikali ya Uganda.

Wachambuzi wanasema ni makubaliano tu yatakayowaruhusu wapiganaji wa LRA kuepuka vifungo, ndiyo yatakayoweza kuwashawishi watoke msituni wanakojificha na kumaliza janga la vita.

Waraka wa wamu ya tatu ya makubaliano kati ya pande hizo mbili, inahusiana na kukiri kwao uhalifu wa vita, lakini hayataji kuhusu adhabu wanaostahiki, zaidi ya kusisitiza tu kwamba “ Uganda ina taasisi zake chini ya sheria za taifa, zenye uwezo wa kushughulikia masuala ya ukiukaji wa haki za binaadamu, “ taarifa inayoashiria kuikataa mahakama ya kimataifa.

Kwa upande wa LRA ina maana kwamba serikali iliyoiomba mahakama ya jinai ya kimataifa iwafungulia mashitaka viongozi wakuu wanne wa LRA 2005, itahitajika kulifuta ombi hilo.

Akizungumza kwa simu na Shirika la habari la Reuters,kutoka eneo moja la msituni katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo wanakojificha,Naibu kamanda mkuu wa LRA Vincent Otti ambaye yumo katika orodha hiyo ya wanaosakwa, alisema “ changa moto sasa ni kwa serikali kuiarifu mahakama ya kimataifa kwamba haiihitaji.

Serikali ya Uganda inasema itaunda mahakama kushughulikia maovu yaliofanywa na waasi, kukiwa na uwezekano wa msamaha, lakini taarifa yake imeikasirisha LRA, iliposema kwamba wanajeshi wa serikali ambao pia walifanya maovu hawatafunguliwa mashitaka yoyote. Wataalamu mmoja akizungumzia utata unaoweza kusababishwa na msimamo kama huo alisema “ Haki kwa upande mmoja tu si jambo linaloweza kufanya kazi.”

Kuhusu suala la msamaha, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uganda Oryem Okello anasema msamaha kwa maovu ya kiwango kikubwa ni jambo lililofanyika kwengineko duniani katika njia za kuleta amani na kuutaja kama mfano mgogoro wa Ireland kaskazini, Afrika kusini na hata katika nchi jirani ya Rwanda ambako kuna mahakama za kijadi “Gacaca”,zinazotoa adhabu ndogo ukiwemo msamaha, kwa waliohusika na mauaji ya halaiki 1994, chini ya mpango wake wa ukweli na maridhiano. Akasema kama kwengine imewezekana , inawezekana pia nchini Uganda.