1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mikakati ya kupambana na ukimwi Afrika.

Nyanza, Halima6 Agosti 2008

Baadhi ya Viongozi wastaafu wa mataifa ya Afrika, wakiongozwa na Rais mstaafu wa Botswana Festus Mogae wamezindua mkakati wa pamoja kushawishi serikali za Afrika kuchukua hatua zaidi katika kupambana na ukimwi.

https://p.dw.com/p/ErJB
Ugonjwa wa ukimwi uliokumba nchi kadhaa barani Afrika, umesababisha ongezeko la watoto yatima.Picha: dpa

Viongozi hao wastaafu wakiongozwa na Rais mstaafu wa Botswana Festus Mogae, wamesema kunahitajika hatua zaidi kuchukuliwa na serikali, pamoja na kampeni ya elimu kwa jamii kutolewa, ili kuweza kuzuia maambukizo mapya katika nchi ambazo mmoja kati ya watu wanne wameambukizwa virusi vya ugonjwa huo.

Miongoni mwa wanachama waanzilishi wa kundi hilo ni pamoja na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano, Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda pamoja na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Askofu Desmond Tutu wa Afrika kusini.

Wengine ni Mkuu wa Tume ya Taifa la kudhibiti ukimwi nchini Kenya Miriam Were pamoja na Jaji Edwin Cameron wa Mahakama ya Rufaa ya Afrika kusini.

Akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu ukimwi, unaofanyika Mexico, Rais wa zamani wa Botswana, Festus Mogae amesema baadhi ya nchi zimeonekana kudharau tatizo hilo.

Hata hivyo ameshukuru juhudi kubwa zilizofanywa, ambapo amesema mamilioni ya watu sasa, wanaweza kupata dawa za kuongeza maisha.

Wakati wa uongozi wa Rais Mogae, Botswana pia ilipunguza maambukizo ya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kutoka wastani wa asilimia 40 hadi asilimia 4.

Rais huyo mstaafu wa Botswana ameelezea wasiwasi wake katika maambukizo mapya yanayotokea na kusema kuwa wameweka malengo ya kutokuwepo kwa maambukizo mapya ifikapo mwaka 2016.

Botswana nchi ambayo asilimia 23 ya watu wake, wana ukimwi, imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi chache zilizofanikiwa katika mapambano hayo, ambayo ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika kutoa bure dawa za kuongeza maisha pamoja na zoezi la upimaji.

Kwa upande wake Jaji Edwin Cameron kutoka Afrika kusini alielezea katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano huo kwamba binafsi anaishi na virusi vinavyosababisha ukimwi, lakini ana bahati kutokana na uwezo wa kifedha alionao kununua dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo.

NayeKwa upande wake Miriam Were kutoka Kenya, amesema msisitizo wake upo katika ubaguzi, miiko na usawa wa kijinsia, mambo ambayo katika nchi nyingi za Kiafrika yanachangia kuenea kwa virusi hivyo vinavyosababisha vifo.

Amesema jamii inahitaji kuzungumza kuhusu HIV, fedheha za ugonjwa huo na tabia za watu kwa sababu kubaki kimya na kuzubaa kunaendelea kuua.

Nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara zimeathiriwa zaidi na ugongwa huo, hususan katika nchi za Botswana, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Namibia, Afrika kusini, Swaziland na Zimbabwe.

Afrika kusini inaongoza kwa kuwa na watu milioni 5.7 walioambukizwa virusi vya ugonjwa wa ukimwi, ikiwa ni kiwango cha juu duniani.

Karibu watu laki tano huambukizwa kila mwaka na karibu watu elfu moja hufariki kila siku kutokana na magonjwa yanayohusiana na ukimwi.