1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mikakati kuelekea kura ya maoni, Sudan.

Halima Nyanza26 Oktoba 2010

Umoja wa Mataifa unazingatia kuongeza vikosi vya kulinda amani katika mpaka wa Sudan ya kaskazini na kusini, wakati nchi hiyo ikijiandaa kupiga kura ya maoni kwa ajili ya kujitenga kwa eneo la kusini.

https://p.dw.com/p/Po2s
Rais wa Sudan ya kusini Salva Kiir.Picha: AP

Akizungumza katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Alain LeRoy amesema wanapanga kuhamisha vikosi kutoka maeneo mengine ya Sudan na kuvipeleka katika eneo hilo la mpaka, huku akitoa wito pia wa jeshi hilo kuongezewa nguvu kimataifa.

Ameyasema hayo wakati wa kujadili uwezekano wa kuimarisha usalama katika kipindi hiki cha kuelekea katika kura ya maoni juu ya taifa la Sudan ya Kusini, itakayofanyika mapema mwaka ujao.

Amefahamisha kuwa Umoja wa Mataifa unalenga kuisaidia Sudan kutayarisha na kutoa ulinzi kwa ajili ya kura hiyo ya maoni iliyopangwa kufanyika Januari 9, mwakani juu ya kugawanywa kwa nchi hiyo na kuwa mataifa mawili ya Sudan ya kusini na kaskazini.

Kura hiyo ya maoni katika Sudan ya kusini na katika mkoa wa Abyei ni sehemu ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005 kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu nchini humo, takriban miongo miwili na kusababisha vifo vya watu zaidi ya milioni mbili.

Kwa upande wake, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Suzan Rice amesema kuna uwezekano kwa muda kuongeza wanajeshi 10,000. Hatua ambayo lakini mkuu wa Operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa ameiona kwamba haitasaidia.

Alain LeRoy amesema hata kama jeshi hilo la Umoja wa Mataifa nchini Sudan litaongezewa nguvu hakutaweza kuzuia uhasama kati ya kaskazini na kusini, iwapo hali ya wasiwasi juu ya kura ya maoni ikiwa bado ipo.

Amewaambia wajumbe kutoka mataifa 15 wanachama katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba njia nzuri iliyopo kuweza kuzuia kurudia tena kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo ni kujidhatiti ili kufikia makubaliano ya kisiasa katika kutekeleza masuala muhimu yaliyobakia.

Kwa upande wake, Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa Daffa-Alla Elhag Ali Osman ameonya kwamba hatua hiyo ya kukiimarisha kikosi hicho cha UNMIS inaweza kuwa ushauri mbaya.

Amewaambia waandishi wa habari ni muhimu kwanza kufikia makubaliano juu ya masuala ya kisiasa ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi, kama vile suala la mpaka.

Ameongezea kusema kuwa iwapo masuala yaliyobakia hayata patiwa ufumbuzi, kunatoa nafasi ya vita kutokea.

Hali ya wasiwasi imeongezeka katika kipindi cha mwezi huu, kwa pande zote mbili za kusini na kaskazini kulaumiana, huku kila upande ukiimarisha majeshi yake katika mpaka wa kaskazini na kusini.

Katika hatua nyingine Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon ameelezea wasiwasi wake na hali ilivyo katika mkoa wenye utajiri wa mafuta wa Abyei. Hakuna tume yoyote inayoshughulikia kura ya maoni iliyotumwa na viongozi katika eneo hilo bado hawajafikia makubaliano na serikali ya Khartoum juu ya nani anafaa kupiga kura au mipaka yake.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters, afp, ap)

Mhariri: Aboubakary Liongo