1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miili zaidi ya wahanga wa ndege MH17 yasafirishwa Uholanzi

Admin.WagnerD24 Julai 2014

Miili zaidi ya wahanga wa ajali ya ndege ya Malaysia iliyodunguliwa wiki iliyopita mashariki mwa Ukraine inatarajiwa kuwasili leo Uholanzi huku umoja wa Ulaya ukijitayarisha kuiwekea Urusi vikwazo vipya

https://p.dw.com/p/1Chvl
Picha: Reuters

Makontena kadhaa yaliyo na miili ya wahanga wa ajali hiyo ya ndege ya Malaysia MH 17 yamepakiwa katika ndege mbili za kijeshi leo kwa siku ya pili mfululizo ya zoezi hilo ya kuisafirisha miili hiyo kutoka Ukraine hadi Uholanzi.

Hayo yanakuja huku serikali ya Australia ambayo iliwapoteza raia wake 37 katika ajali hiyo ikituma maafisa hamsini wa polisi kuelekea London leo kujiunga na kikosi maalum kilichopendekezwa na Umoja wa Mataifa kitachokuwa na jukumu la kulinda eneo la mkasa wa ndege hiyo mashariki mwa Ukraine.

Polisi wa kimataifa kupelekwa Ukraine

Waziri mkuu wa Australia Tony Abbott ametangaza kupelekwa kwa maafisa hao wa usalama na kuongeza kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa Australia na Uholanzi wanakwenda Kiev kutafuta makubaliano na serikali ya Ukraine kuridhia kupelekwa kwa kikosi hicho cha kimataifa cha usalama.

Waziri mkuu wa Australia Tony Abbott
Waziri mkuu wa Australia Tony AbbottPicha: picture-alliance/dpa

Huku hayo yakijiri,mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama 28 wa umoja wa Ulaya wamesema watakutana leo mjini Brussels kuorodhesha vikwazo vipya dhidi ya Urusi kwa kuendelea kuuchochea mzozo wa Ukraine

Umoja wa Ulaya ulikubali kuharakisha hatua hiyo ya kuiwekea Urusi vikwazo zaidi baada ya ndege hiyo ya Malaysia kudunguliwa wiki moja iliyopita ikiwa na watu 298 huku waasi wanaotaka kujitenga kwa eneo la Mashariki mwa Ukraine wakishutumiwa kuhusika na udunguaji huo kwa usadizi kutoka Urusi.

Umoja wa Ulaya kuiwekea Urusi vikwazo zaidi

Serikali ya Ujerumani imesema inaamini kuwa umoja huo utaziwekea sekta kadhaa za uchumi wa Urusi vikwazo ifikapo mwishoni mwa mwezi huu na hilo linaweza kuepukika iwapo Urusi itachukua hatua za haraka kupoza mzozo wa mashariki mwa Ukraine.

Mabaki ya ndege ya Malaysia MH17
Mabaki ya ndege ya Malaysia MH17Picha: imago/Xinhua

Inaripotiwa kuwa maafisa wa Ujerumani walioko Brussels wamesema wangependa kuwepo muda makhususi wa muda ambapo vikwazo dhidi ya Urusi vitadumu ili kutoa fursa ya uhusiano wa kawaida kurejea.

Maafisa wa kijasusi wa Marekani hapo jana walisema kuna ushahidi kuwa ndege hiyo ilidunguliwa na kombora aina ya SA 11 linalorushwa kutoka ardhini kuelekea angani na kudai Urusi ilichangia katika udunguaji huo lakini haikueleza bayana vipi.

Urusi kwa upande wake imeitaka Marekani kuthibitisha madai yake kwa kuutoa wazi ushahidi ulionao kuwa Urusi ilihusika katika udunguaji wa ndege hiyo.

Katika jimbo linalodhibitiwa na waasi la Donetsk, mapigano makali yameripotiwa kati ya wanajeshi wa serikali na waasi hao na kusababisha kukatizwa kwa nguvu za umeme baada ya kuharibiwa kwa kituo cha kusambaza umeme katika eneo hilo.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Ap/Afp

Mhariri: Sekione Kitojo