1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya UEFA:Bremen hoi bin taaban

30 Septemba 2010

Werder Bremen ya Ujerumani ambayo iko katika kundi A, jana ilikiona kilichomtoa kanga manyoya, pale ilipokandikwa mabao 4-0 na mabingwa watetezi Inter Milan katika michuano ya ligi ya mabingwa Ulaya

https://p.dw.com/p/PQFG
Kiungo wa Bremen Philipp Bargfrede,kushoto Sebastian Prodl, kulia na golikipa wao Tim Wiese wakiduwaa baada ya Samuel Eto'o kupachika baoPicha: AP

Alikuwa ni Simba kutoka Cameroon Samuel Etoo aliyeunguruma mara tatu peke yake katika mlango wa Bremen, kwenye dakika za 21, 27 na 81, huku Sneijder akipachika moja.Huo ni ushindi wa kwanza Inter kuupata nyumbani katika michuano hiyo ya Ulaya chini ya kocha Rafa Banitez.

Banitez akimuelezea Etoo alisema kuwa mchezaji huyo ni hatari sana anapokuwa karibu na lango, hivyo katika mfumo wake ameamua kumuweka katika safu ya mbele kabisa, tofauti na msimu uliyopita chini ya Jose Morinho ambapo alikuwa nyuma ya wapachika mabao wengine kama vile Milito.

Naye kocha wa Werder Bremen Thomas akizungumzia kipigo walichokipata, alisema si kwamba ni kama vile ilikuwa sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa Inter Milan na wao waliwapa zawadi nyingi, kwa maana kwamba mwanya wa kuweza kupachika mabao hayo.

Kundi hilo A jana pia lilishuhudia nyavu zikitikishwa mara nne jijini London pale Tottenham Hotspur ilipoishindilia Twente Enschede ya Uholanzi mabao 4-1.

Kwa matokeo hayo, Milan na Tottenham zinaongoza kundi hilo zikiwa na pointi 4 kila mmoja huku Bremen na Twenet Enschede zikiwa na pointi moja kila mmoja.

Champions League FC Schalke gegen Benfica Lissabon
Klaas-Jan Huntelaar (jezi nyeupe)wa Schalker akipachika bao dhidi yaPicha: AP

Katika Kundi B, Schalke 04, ikicheza nyumbani mjini Gelsenkirchen hapa Ujerumani iliichapa Benfica ya Ureno mabao 2-0, yaliyopachikwa na Jefferson Farfan na Klass-Jan Huntelaar.

Lilikuwa ni pambano kali ambapo iliwabidi Schalke wasubiri hadi katika dakika 73 pale Farfan mshambuliaji kutoka Peru alipolifumania lango la Benfica, kabla ya Huntelaar kufunga la pili.Hilo ni bao la kwanza kwa mshambuliaji huyo kuifungia Schalke katika michuani ya Ulaya tokea alipojiunga na timu hiyo August kutokea AC Milan kwa kitita cha Euro millioni 14.Schalke pia ilimnunua Raul kutoka Real Madrid.

Kocha wa Schalke Felix Magath alisema kuwa ameridhishwa na matokeo pamoja na mchezo wenyewe kwa ujumla, akisema ilikuwa mechi ngumu kutokana na uwezo mkubwa waliyokuwa nao Benfica

Ama Olympic Lyon ilijiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kwa raundi ijayo kutoka kundi hilo baada ya kuifunga Hapoel Tel Aviv ya Israel mabao 3-1 na hivyo kufikisha pointi 6.Schalke na Benfica zina pointi tatu kila mmoja.

Huko mjini Valencia Uhispania, Manchester United iliwabidi kumsubiri Javier Hernandez kutoka benchi kuweza kuipatia bao pekee dhidi ya wenyeji Valencia dakika 5 kabla ya kipyenga cha kuhitimisha mpambano.

Ni ushindi wa pili kwa Manchester United katika michuano ya Ulaya katika mechi 19 dhidi ya timu za Uhispania ugenini.Kocha wa timu hiyo Sir Alex Ferguson alisema kuwa wanastahili pongezi kwa jinsi walivyoweza kulinda lango lao na hatimaye kupata ushindi dhidi ya timu aliyoielezea kuwa ngumu na kali.

United sasa inaongoza kundi lao C ikiwa na pointi 4 sambamba na Glascow Rangers ambayo hiyo jana nayo ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bursaspor.Valencia vinara wa ligi ya Uhispania wao wana pointi tatu.

Katika mechi nyingine hiyo jana Barcelona walilazimishwa sare ya bao 1-1 na Rubin Kazan ya Urusi, huku FC Copenhagen ikitamba ugenini kwa kuichapa Panathinaikos mabao 2.0

Mwandishi:Aboubakary Liongo