1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi inaanza Sochi

Mjahida7 Februari 2014

Rais mpya wa kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach amesema hali ni shwari mjini Sochi katika maandalizi ya kufunguliwa rasmi michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi leo (07.02.2014) mjini humo.

https://p.dw.com/p/1B4e3
Michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridi
Michezo ya Olimpiki ya msimu wa baridiPicha: Reuters

Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa imefanya mkutano wake wa kwanza leo na waandaaji wote wa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi, ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa.

Rais mpya wa kamati hiyo Thomas Bach amesema kawaida ya kila ufunguzi wa michezo ya aina yoyote hakukosekani matatizo ya hapa na pale lakini kila kitu kwa sasa kinaendelea salama. Hata hivyo Bach hakueleza zaidi juu ya matatizo hayo.

Bach amesema anamatumaini makubwa kuwa ufunguzi unjaotarajiwa kufanyika leo jioni utafana na michezo hiyo ya Olimpiki ya msimu wa baridi itakuwa ya mafanikio.

Katika ufunguzi huo wanamuziki mashuhuri wa mtindo wa Pop nchini Urusi wanaojulikana kama tATu watashiriki kwa kuimba wimbo juu ya wasichana wawili wa shule walioko kwenye uhusiano wa kimapenzi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na Rais mpya wa kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na Rais mpya wa kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Thomas BachPicha: Reuters/Shamil Zhumatov

Wimbo huo kwa jina "Not Gonna Get Us" yani hamutotupata umenuiwa kuonesha sura ya Urusi mbele ya macho ya ulimwengu kama ambavyo wanaharakati, na viongozi wa dunia wanavyoipinga sheria ya taifa hilo dhidi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Mmoja wa watayarishaji wa sherehe za leo Konstantin Ernst amesema wamechagua wimbo huo "Not Gonna Get Us" kwa kuwa ndio wimbo pekee nchini Urusi unaoweza kutambulika kimataifa.

Shaka ya Ufanisi wa Michezo ya Sochi

Haki za mashoga, kukandamizwa kwa wanaharakati wa haki za binaadamu, uharibifu wa mazingira, ufisadi wa hali ya juu, hali duni za wafanyakazi na wajenzi wa eneo la michezo hiyo na hatua kali za ulinzi, haya yote yametilia shaka kufanikishwa kwa Michezo hiyo.

Huku hayo yakiarifiwa rais wa China Xi Jinping alionya juu ya kuingiza siasa katika michezo hiyo. Vyombo vya habari nchini humo vimesema hatua hiyo ni ya kumuunga mkono rais Vladimir Putin wa Urusi, kabla ya kuanza rasmi michezo hiyo ya olimpiki ya msimu wa baridi.

Mwanamichezo akiteleza kwenye theluji
Mwanamichezo akiteleza kwenye thelujiPicha: Reuters

Viongozi hao wawili walikutana hapo jana mjini Sochi katika ziara ambayo inapishana na ziara ya Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe ambayo huenda ikadhoofisha zaidi mahusiano ya nchi hiyo na China juu ya udhibiti wa visiwa fulani.

Baadhi ya Viongozi kutohudhuria Michezo

Licha ya hayo kuna wasiwasi juu ya kuyumba kwa usalama katika ufunguzi wa michezo hiyo, kutokana na hilo rais Putin ameamrisha mikakati maalum ya usalama kuwekwa nchini kote hasa baada ya kuuwawa watu 34 katika shambulizi la bomu mjini Volgograd mwezi Desemba, mwaka jana.

Ulinzi umeimarishwa nchini humo hasa mjini Sochi huku vikosi vikiwa katika tahadhari ya hali ya juu kufuatia kitisho cha kutokea mashambulizi ya kigaidi yanayodaiwa kupangwa na waislamu walio na itikadi kali.

Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Marekani kwa upande wake inahofu juu ya usalama katika michezo hiyo.

Rais wa Marekani Barrack Obama, Francois Hollande wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na rais wa Ujerumani Joachim Gauck hawatahudhuria michezo hiyo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/Reuters/AP

Mhariri: Yusuf Saumu