1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo mwishoni mwa wiki

25 Septemba 2009

Bayern Munich ina miadi na Hamburg

https://p.dw.com/p/JowQ
Ze Roberto afurahia changamoto na Munich.Picha: AP

-Katika Bundesliga-jioni hii,macho yanakodolewa changamoto kati ya viongozi wa Ligi-Hamburg na Bayern Munich.

-Guus Hiddink-kocha wa Russia, ametangaza kikosi chake kwa mpambano wa kufuzu kombe lijalo la dunia na Ujerumani hapo Oktoba 10.

Katika kanda ya Afrika, kocha wa mabingwa wa Afrika-Misri, Hassan Shehata, ateua kikosi cha wachezaji 24 kwa miadi na Chipolopolo-Zambia pia Oktoba 10.

BUNDESLIGA NA PREMIER LEAGUE:

Macho leo (Jumamosi) yanakodolewa huko Hamburg-viongozi wa Ligi wakiwakaribisha nyumbani mabingwa mara kadhaa Bayern Munich ambao baada ya misukosuko ya awali, sasa wameanza kutamba.Mwishoni mwa wiki iliopita, Munich iliwazaba majirani zao Nüremberg mabao 2:1 na kutoroka na pointi 3 nyengine.

Duru ya mwishoni mwa wiki hii kwa kweli, ilianza jana usiku (ijumaa) kwa mpambano 1 kati ya Nüremberg na Bochum -timu 2 zilizopoteza pointi 3 mwishoni mwa wiki iliopita . Bochum ilimtimua kocha wake.

Mla, lakini wanasema, ni mla leo, mla jana kala nini ?Hamburg ndio iliopo kileleni mwa Bundesliga na Munich inanyatia nyuma kuparamia kileleni.Kati ya wiki katika kinyanganyiro cha Kombe la Shirikisho la dimba la Ujerumani,Hamburg iliteleza na ikapigwa kumbo nje ya Kombe hilo na timu ya daraja ya pili Osnerbrueck.

Kabla timu hizi mbili kuingia uwanjani ,kocha wa Munich, mdachi van Gaal alisema kwamba, amefurahi sana kuona Hamburg juzi, imetolewa jasho na kubidi kurefusha mchezo kabla kuaga Kombe hilo.Anatumai van Gaal pia kwamba, jioni hii, Hamburg itapungukiwa na kasi.Anaamini kwa muujibu wa falsafa yake ya dimba , ukishindwa mpambano uliopita ,kunakuathiri kiasi fulani katika mpambano ujao.Hatahivyo, van Gaal anawaonya watoto wake wachunge: "ukimuona simba kalala, usimuamshe."

Dortmund haitaidharau Schalke 04 katika mpambano wao leo wa timu 2 za mtaani mkoani Ruhr.Dortmund lakini, imefaulu mara moja tu kutamba kati ya mapambano yake 10 nyumbani ilipocheza na Schalke.

Changamoto nyengine ya kusisimua jioni ya leo, bila shaka, ni mjini Cologne kati ya mahasimu wengine 2 wa mtaani:FC Cologne na Bayer Leverkusen. Cologne, baada ya kuburura mkia wa Ligi kitambo kirefu,ilianza kujikomboa mwishoni mwa juma lililopita ilipoisangaza Stuttgart nyumbani kwao na kutoroka na pointi 3.Leo, Cologne, inacheza nyumbani -uwanja ule ule majuzi ilipowatia munda mabingwa VFL Wolfsburg na kuwachapa mabao 3-2 ili kuwatoa nje ya Kombe la Shirikisho la dimba la Ujerumani.

Chini ya hali hii, ni vigumu leo kwa Leverkusen kutoroka kwa urahisi kama kawaida yake na pointi zote 3 kutoka Cologne.Eintracht Frankfurt ilioanza vizuri msimu huu, inacheza na Stuttgart wakati mabingwa Wolfsburg ni wenyeji nyumbani wa Hannover.Werder Bremen inacheza na Mainz.

Kesho Jumapili, kalenda ya duru hii ya 7 itakamilishwa kwa changamoto 2: Freiburg itakuwa nyumbani kuikaribisha Borussia Moenchengladbach wakati hatima ya kocha wa Hertha Berlin, Mswisi Havre,huenda ikaamuliwa kesho na Hoffenheim.Berlin iliaibishwa mwishoni mwa juma lililopita na chipukizi Freiburg ilipozabwa mabao 4:0.

Ama katika Premier League-Ligi ya Uingereza:Baada ya zahama ya mahasimu 2 wa mtaani mwishoni mwa wiki iliopita-Manchester United na Manchester City, leo Manu ni wageni wa Stoke City.Manchester City ina muda wa kupumua hadi keshokutwa Jumatatu, itapoikaribisha nyumbani West Ham United.Chelsea iliopo kileleni mwa Premier League,inatazamiwa kutamba leo nyumbani mwa Wigan Athletic.Liverpool iko pia nyumbani maadui zao wakiwa Hull City.Portsmouth yapambana na Everton wakati Blackburn Rovers inakamilisha kalenda ya leo na Aston Villa.

Nje ya Ligi hizo 2 maarufu za ulaya,mapema mwezi ujao itakua zamu ya kinyan'ganyiro cha kufuzu kwa Kombe lijalo la dunia 2010 nchini Afrika Kusini.Katika kanda ya Ulaya, Ujerumani ina miadi na Russia, Oktoba 10 huko Moscow.Huo ni mpambano wa "kukata na shoka" kwa timu zote 2. Kocha wa Russia, Guus Hiddink ameshatangaza kikosi chake cha wachezaji 23 kikiegemea zaidi mastadi wa klabu ya Zenit St. Petersburg.Jogoo la Arsenal-Andrei Arshavin, litaongoza mashambulio ya warusi katika lango la wajerumani..

Katika kanda ya Afrika, mabingwa Misri nao pia wanajinoa kwa mpambano wao wa Oktoba 10 na Chipolopolo-risasi za Zambia. Langoni akiwa kipa Essam Al Hadari, usoni hujuma tena zitaongozwa na Mohamed Aboutrika na Amr Zaki wa Zamalek.

Muandishi : Ramadhan Ali /RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman