1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo mwishoni mwa wiki

1 Juni 2009

Bremen mabingwa wa DFB wakati Chelsea ni wa FA.

https://p.dw.com/p/I1UA
Bremen na DFB-PokalfinalePicha: AP Graphics/DW

Vita ya J.K.Kongo imeitimua Conton sport Garoua ya kamerun nje ya Kombe la Shirikisho la dimba la Afrika-

Chelsea yamuaga kocha wake Mdachi Guus Hiddink kwa Kombe la FA.Kocha mpya ni Ancelotti hadi jana kocha wa AC Milan ya Italłi.

Werder Bremen yaipiga kumbo Bayer Leverkusen , na kutwaa kwa mara ya 6 Kombe la Shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB) Pokale.

Werder Bremen, ilirekebisha madhambi iliofanya katika msimu wa mwaka huu wa Bundesliga kwa kutwaa Kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB Pokale).Bremen iliopokonywa taji la Kombe la ulaya la UEFA na Shakhtar Dontesk ya Ukraine, ilifuta machozi jumamosi ilipoikomea Bayer Leberkusen bao 1:0 na kutoroka na Kombe mjini Berlin.

Mesut Ozil aliuona wavu mnamo dakika ya 58 ya mchezo kufuatia pasi maridadi aliopewa na mbrazil Diego.

Mwishoe, mbele ya mashabiki 74,000 katika Uwanja wa Olimpik wa Berlin,Frank Baumann-nahodha wa Bremen alikabidhiwa Kombe .

Kocha wa werder Bremen Thomas Schaaf mwishoe alisema:

"Kwa jumla, tulijionea mchezo mzuri kabisa na pirika pirika nyingi-timu zote mbili zilicheza uzuri kabisa,lakini kila mmoja aliona kuwa sisi tulivinjari kuondoka na Kombe."

Nae kocha wa Bayer Leverkusen Bruno Labadia ambae hatima yake kabla ya finali hii ilikuwa mashakani alisema,

"Mwishoe, matokeo yalikuwa bao 1:0.Kwa Bremen mambo ni mazuri kabisa na kwetu ni msiba mkubwa."

Sasa hatima ya kocha wa Bayer Leverkusen, haijulikani.Kunai uvumi lakini kwamba anaachana na Leverkusen na kuwa kocha mpya wa Hamburg.Hatima ya Bruno Labadia,mshambulizi hatari wa zamani,inatarajiwa kukatwa kesho Jumaane baada ya mazungumzo na Kiongozi wa Leverkusen, Wolfgang Holzhaueuser na mkurugenzi Rudi Voeller.

Wakati Kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani limeelekea Bremen na taji la ubingwa la Bundesliga Wolfsburg,timu ya mwisho kati ya 3 zinazopanda daraja ya kwanza msimu ujao sasa inajulikana: nayo ni Nuremberg ilioitoa katika duru ya nyumbani na ugenini Energie Cottbus.Baada ya kuilaza kwa mabao 3 katika duru ya kwanza huko Cottbus, Nuremberg iliikomea jana mabao mengine 2 na kukata tiketi ya mwisho kurudi Nurmberg daraja ya kwanza.

Mchezaji mmoja wa Nuremberg aliueleza ushindi wao hivi:

"Tumefurahi kutekeleza leo na katika duru ya kwanza kibarua kikubwa tulichopewa dhidi ya Energie Cottbus.Kwahivyo, tuna furaha sote na hasa mashabiki wetu."

Baada ya kujulikana timu ya mwisho itakayopanda msimu ujao wa Bundesliga,kinyanganyiro cha wachezaji stadi kinaendelea huku klabu zikijiwinda kwa msimu ujao: Biashara kubwa ya kuuza wachezaji majira haya ya kiangazi itategemea wapi stadi wa Ufaransa Franck Ribery anacheza ? Bundesliga iko nyuma ya Ligi mashuhuri za Ulaya hasa zile za Uingereza ,Spian na hata Itali.Hatahivyo, hata hatima ya mchezaji bora wa dimba wa mwaka wa dunia Cristiano Ronalndo wa Manu anabidi kusubiri uamuzi wa Bayern Munich na stadi wake Ribery.

Ribery amehusishwa na kujiunga na Chelsea kwavile,kocha wao mpya mtaliana Ancelotti anamtaka sana Ribery.Vyombo vya habari vya Uingereza vimehanikiza jana kwa kuidai Chelsea haimpati Ribery na kwamba anaelekea Real madrid,Spian.Hii itakuwa na maana kuwa Ronaldo hataweza kuhamia Real na atabaki Manu kwa mwaka mwengine.Hii pia itamaliza kiu cha Manu kwa mfaransa Ribery.

Chelsea,kufuatia ushindi wake wa Kombe la FA la Uingereza ilipoilaza Everton mabao 2:1, imetangaza leo kuwa kocha wake mpya msimu ujao atakuwa mtaliana Carlo Ancelotti.Kocha aliewatawaza juzi mabingwa wa Kombe la FA,mdachi Guus Hiddink ,anarejea kuwa kocha wa timu ya taifa ya Urusi inayojiandaa kufuzu kwa Kombe lijalo la dunia. Ancelotti,mchezaji wa zamani wa kiungo wa Itali,alijiuzulu jana kama kocha wa AC Milan kufuatia miaka 8 huko San Siro na kuitawaza AC Milan mabingwa mara 2.

Tumalizie kwa kinyanganyiro cha mwishoni mwa wiki cha Kombe la shirikisho la dimba barani Afrika :Confederationbs CUP : Katika kinyanganyiro cha kombe hilo Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ilinguruma mjini Kinshasa ilipoikandika Contonsport Garoua ya Kamerun kwa mabao 2:0.Vita inasonga mbele duru ijayo kwa wingi wa magoli.

Mjini Luanda, Santos ya Angola ilitamba mbele ya Al Ahly ya Misri kwa mabao 3:0.santos imeipiga kumbo Al Ahly kufuatia changamoto za mikwaju ya penalty baada ya kuwa sare mabao 3:3.Santos ilishinda kwa mabao 6-5.

Na kwa taarifa hiyo, ndio sina budi bali kuishia hapo kwa leo.

Muandishi : Ramadhan Ali/DPAE

Mhariri : M.Abdul-Rahman