1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo mwishoni mwa Juma

Sekione Kitojo31 Julai 2009

Kinyang'anyiro cha kombe la chama cha kandanda nchini Ujerumani chaanza leo.

https://p.dw.com/p/J11f
Mchezaji wa Werder Bremen Diego, kati, akipambana na Sebastian Kehl, wa Dortmund , kulia, katika mchezo wa kombe la DFB.Picha: AP

Kinyang'anyiro cha kombe la chama cha kandanda Ujerumani DFB Pokal chaanza kutimua vumbi , kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza Bobby Robson afariki dunia .

Kinyang'anyiro cha kuwania kombe la chama cha mpira cha Ujerumani DFB Pokal kimeanza rasmi jana Ijumaa katika kulikuwa na michezo sita ambapo mabingwa wa ligi ya Ujerumani VFL Wolfsburg walikuwa wakipambana na Wehen.

Leo Jumamosi jioni viwanja mbali mbali vitawaka moto pale michezo tisa itakapofanyika, ambapo timu za daraja la kwanza za Borussia Dortmund , Borussia Monchengladbach , FC Koln na Schalke 04 zitakuwa uwanjani katika duru hii ya kwanza ya kombe la chama cha kandanda nchini Ujerumani.

Kesho Jumapili kutakuwa na duru nyingine ya michuano ya kombe hilo ambapo Werder Bremen , Hoffenheim na FC Bayern zitakuwa na kibarua kuziondoa timu za madaraja ya chini katika kinyang'anyiro hicho, lakini ambazo ni ving'ang'anizi na mara nyingi vigogo huumbuka na kuachwa hoi.

Bobby Robson
Kocha Bobby Robson aliyefariki dunia siku ya Ijumaa.Picha: AP

Kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza na klabu ya Newcastle Sir Bobby Robson amefariki dunia siku ya Ijumaa akiwa na umri wa miaka 76 baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa saratani.

Robson ambaye amekuwa akiugua ugonjwa huo kwa muda wa miaka kadha , aliiongoza Uingereza hadi katika nusu fainali ya kombe la dunia katika mwaka 1990 kabla ya kuacha wadhifa huo na kuwa kocha wa timu kadha katika bara la Ulaya ikiwa ni pamoja na PSV Eindhoven, Sporting Lisbon, Porto, Barcelona na hatimaye Newcastle.


Mahakama ya usuluhishi katika michezo, imekataa rufaa ya mshambuliaji wa Romania Adrian Muttu dhidi ya amri ya kulipa kitita cha Euro milioni 17.17 kama malipo ya fidia kwa Chelsea, mahakama hiyo imesema katika taarifa.

Mutu , ambaye hivi sasa anachezea katika timu ya Fiorentina nchini Italia, ameamriwa kulipa kitita hicho na FIFA mwaka jana baada ya kupigwa faini na klabu hiyo ya Premier League katika mwaka 2004 kwa kukutikana anatumia madawa ya kulevywa.


Nyota wa soka wa Uingereza David Beckham amekosa mazoezi siku ya Alhamis kutokana na maumivu ya mgongo, na kuleta shaka iwapo nyota huyo wa Los Angeles Galaxy ataweza kushiriki katika mchezo kati ya timu hiyo na FC Barcelona leo Jumamosi.

Beckham amepata maumivu hayo siku tatu zilizopita lakini hakutilia maanani sana maumivu hayo, akisema kuwa anatarajia kufanya mazoezi kabla ya mchezo huo.


Nae Frank Ribery hatakuwa fit vya kutosha kuweza kuchezea timu yake ya taifa ya Ufaransa katika mchezo wa kuwania kukata tikiti ya fainali za kombe la dunia dhidi ya visiwa vya Faroe mjini Torshavn, alinukuliwa akisema na vyombo vya habari vya Ufaransa siku ya Ijumaa.

Mchezaji huyo wa Bayern Munich , ambaye anaendelea kupona maumivu ya goti, ameongeza kuwa pia hataweza kushiriki katika mchezo wa kwanza wa timu yake katika msimu huu dhidi ya Hoffenheim hapo tarehe 8 August.


Maafisa wa chama cha soka nchini Australia wameanzisha sheria kali mpya zenye lengo la kuwazuwia wachezaji kujaribu kuwahadaa waamuzi kwa kujiangusha.

Shirikisho la soka la Australia FFA limetangaua jana Ijumaa kuwa itaweka adhabu ya kutocheza michezo miwili kwa wachezaji ambao wanapatikana na hatia ya kujiangusha, ama kujidai wameangushwa katika eneo la adhabu ya penalt ama kusababisha mpizani kutolewa kwa kadi nyekundu.

Nayo kamati ya kimataifa ya Olimpiki jana Ijumaa imefungua maombi ya nchi zinazotaka kuwa wenyeji wa michezo ya majira ya baridi ya olimpiki katika mwaka 2018.


Mwandishi Sekione Kitojo/AFPE/DPAE/RTRE


Mhariri Mohammed Abdul-Rahman