1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo Mwishoni mwa Juma

4 Mei 2009
https://p.dw.com/p/HjYe
Grafite wa Wolfsburg anayeongoza katika orodha ya wafungaji bora wa Bundesliga akishangiria bao. Ameshafunga mabao 23.Picha: AP

Ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga: Bayern Munich sasa imerudi tena kutoa kitisho kwa Wolfsburg inayoshikilia usukani wa ligi hiyo ikiwa ni baada ya Bayern kumfukuza kazi kocha wake, Jurgen Klinsmann, wiki iliopita, na nafasi yake kuchukuliwa na Jupp Haynckes aliyeteuliwa kuwa Kocha wa mpito. Bayern ilirudisha tena matumaini kwa mashabiki wake ilipoifunga Borussia Monchengladbach mabao 2-1 mwishoni mwa juma. Wolfsburg, kwa upande wake, iliendelea kutamba. Kilabu hiyo inayoongozwa na Kocha Felix Magath ambaye aliwahi pia kuifundisha Bayern Munich kabla ya kutimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Klinsmann iliibwaga Hoffenheim mabao 4-0 kuongezea Pointi 3 mbele ya Munich ikiwa sasa na jumla ya pointi 60.

Gumzo lote wakati huu ni kuihusu Bayern Munich. Mwenyekiti Karl Heinz Rummenige alisisitiza tena jana kwamba mtu anayetafutwa na kilabu hiyo kuchukua hatamu kama Kocha ni mwenye maarifa na kivutio-hizo zikiwa sifa mbili kubwa . Rummenige alikua akizungumza katika mahojiano yaliochapishwa katika toleo la jana Jumapili la gazeti la Die Welt. Miongoni mwa majina ambayo yanatajwa ni pamoja na makocha watatu wa Kiholanzi, Louis van Gaal, Frank Rijkaard, na Martin Jol.

Hata hivyo, Van Gaal anatajwa kuwa ndiyo mwenye uwezekano wa kuchukua nafasi hiyo, baada ya Meneja wa Bayern, Uli Hoeness, kusema kuna kifungu katika mkataba wa kocha huyo anayeiongoza kilabu ya Uholanzi, AZ Alkmaar wakati huu , kinachompa nafasi ya kuweza kuondoka mapema. Mkataba wa Gaal na Alkmaar unamalizika mwaka ujao.

Katika msimamo wa Bundesliga kwa upande mwengine . Nyuma ya Wolfsburg na Bayern ni Hertha Berlin katika nafasi ya tatu baada ya sare ya bao moja kwa moja na Hamburg jana. Hata hivyo kilabu hizo mbili ilioweza kuondoka na ushindi na kuziba mwanya. Pindi Hertha Berlin ingeshinda mchezo huo ingepanda hadi nafasi ya pili na kuiandama Wolfsburg kwa tafauti ya pointi 1 tu, Lakini sasa ina pointi 56, pointi moja nyuma ya Munich , wakati Hamburg iko nafasi ya tano pointi sawa na Stuttgart , lakini Stuttgart ikitangulia kwa wingi wa magoli.

FC Köln hatimae iliwafurahisha mashabiki wake katika uwanja wa nyumbani baada ya kufanikiwa kuibwaga Werder Bremen bao moja kwa bila.

Kilabu zinazokabiliwa na kitisho cha kushuka daraja ni Karlsruhe katika nafasi ya mwisho ya 18 kwenye msimamo wa matokeo jumla, Borussia Monchen gladbach nafasi ya 17 na Armenia Bielefeld katika nafasi ya 16.

Wanaongoza kwa ufungaji mabao mengi hadi sasa ni Grafite wa Wolfsburg akiwa na jumla ya magoli 23, Edin Dzeko pia wa Wolfsburg ,Mario Gomez wa Stuttgart na Patrick Helmes wa Bayer Leverkusen wote wana magoli 19 kila mmoja na Vedad Ibisevic kutoka Hoffenheim ameuona wavu mara 18.

Katika ligi nyengine za Ulaya, nchini Uhispania sasa ni dhahiri kwamba miamba Real Madrid wana nafasi ndogo ya kuweza kunyakua ubingwa msimu huu, baada ya kukiona kilichomtoa kanga manyoya walipoonja machungu ya kipigo cha mabao 6-2 mbele ya mahasimu wao, Barcelona, ambayo imejiimarisha zaidi kileleni na matumaini ya kutwaa ubingwa huo wa La Liga. Pambano hilo lililokua likisubiriwa kwa hamu lilipewa jina la El Klasico.

FC Barcelona Samuel Eto'o Thierry Henry Andres Iniesta Lionel Messi,
Iniesta,Eto'o na Henry wakimpongeza Messi (namba 10) baada ya kupachika bao.Picha: AP

Nchini Italia ligi kuu serie A iliendelea mwishoni mwa juma, huku mashabiki wa Juventus na Roma wakigeuza hasira zao kwa makocha wa kilabu zao. Juventus ililazimishwa sare na Lecce ambayo iko nafasi moja tu kutoka mkiani. Juve hadi sasa imeshindwa kushinda mechi tano zilizopita na hawana matumaini ya kunyakua tena ubingwa. Mashambulizi ya maneno yaliwaandama rais wa Juventus Giovanni Cobolli Gigli na Kocha Claudio Ranieri.

mashabiki wa Roma nao walisikika wakiimba nyimbo za kuikashifu kilabu yao baada ya sare ya bila kwa bila na kilabu dhaifu ya Chievo. Matokeo hayo yana maana Roma haina pia hata nafasi ya kufanikiwa kucheza ligi ya kilabu bingwa Champions league msimu ujao.

Ligi ya Italia : Ni Inter Milan inayoongoza. Milan ilijiimarisha kileleni ilipoilaza Lazio 2-0. Inter ina pointi 7 zaidi kuliko AC Milan inayoshika nafasi ya pili kukisalia mechi nne na ligi kumalizika. AC Milan, kwa upande wake, ikaibwaga Catania mabao 2-0, wakti Torino ilishindwa kutamba mbele ya Forentina ilipofungwa bao 1-0. na Genoa kuilaza Sampdoria 3-0 .

Ligi ya England Premier League bado ni Manchester inayokamata usukani, pointi 3 zaidi ya Liverpool na mechi moja ya ziada. Manchester United, au Manu kama inavyofahamika, iliilaza Middlesbrough 2-0 Jumamosi.

Fußball Ryan Giggs Manchester United Champions League
Ryan Giggs wa Manchester United mwenye umri wa miaka 35, ni mkongwe wa kutegemewa katika nafasi ya kiungoPicha: picture-alliance / dpa

Liverpool jana ikaitandika New Castle United 3-0 . Nafasi ya tatu ni Chelsea iliyotamba nyumbani na kuibwaga Fulham mabao 3-1. Wakati Gunners au Arsenal wako nafasi ya nne. Arsenal ilishinda ugenini mwishoni mwa juma mabao 3-0 dhidi ya Portsmouth.

Duru ya tatu ya mashinadano ya kandanda ya kombe la Shirikisho la soka barani Afrika, CAF, imemalizika baada ya michuano ya marudiano ya duru hiyo. Miongoni mwa kilabu zinazosonga mbele ni Santos ya mjini Luanda Angola iliyoitoa Union Douala ya Cameroun. Sfaxien ya Tunisia ilioiondoa, Abidjan Treichville ya Ivory Coast, Stade Malien ya Mali imeiondoa JSM Bejaia ya Algeria kwa mikwaju ya Penalty 13- 12 baada ya kutoka sare 1-1. Red Arrows ya Zambaia inasonga mbnele kwa kuiondoa ENPPI ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini imeyaaga mashindano hayo ikitolewa na Vita ya Kinshasa -Jmhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Riadha:Mkenya Justus Kipchirchir Kiprono ameshinda mbio ndefu za marathon za mjini Roma akinyakua ushindi huo kwa muda wa saa mbili dakika 14 na sekunde 48. Mkenya mwenzake, Philip Kipkoech, alimaliza wa pili na Cherkaoui Laalami wa Moroko nafasi ya tatu.

Mshindi wa mbio hizo za Roma upande wa wanawake jana alikua Nadir Sabino de Siqueira wa Brazil aliyetumia muda wa saa mbili dakika 47 seunde 2, akifuatwa na Wataliani Stefania Satini na Paola Pillon nafasi ya pili na ya tatu.

Naye Mkenya Micah Kogo akanyakua ushindi wa mbio za barabarani za masafa ya kilomita 10 mjini Edinburgh, akimuacha nafasi ya pili bingwa wa mwaka jana, Mkenya Bernard Kipyego, na Mhispania Chema Martinez, katika nafasi ya tatu.

Ndondi:Katika ringi ya mabondia Bingwa wa zamani wa dunia uzito wa Feather Barry McGuigan amemtaka Ricky Hatton hatimae astaafu akisema enzi za bondia huyo mwenzake zimekwisha, baada ya Hatton kupigwa katika raundi ya pili tu na Mfilipino Manny Pacquiao mwishoni mwa juma. McGuigan alisema hapana shaka yoyote Hatton alikua mmoja kati ya mabondia bora kabisa wa Uingereza, lakini sasa wakati wake wa kustaafu umefika.

Mwandishi: Mohamed Abdul-Rahman /RTRE/AFPE

Mhariri:Othman Miraji