1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michel Djotodia aachia ngazi

10 Januari 2014

Michel Djotodia ambaye alichukua hatamu za uongozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kufuatia shinikizo la kikanda. Aliingia madarakani baada ya muungano wa waasi aliouongoza kuvishinda vikosi vya serikali.

https://p.dw.com/p/1AoOt
Michel Djotodia, rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliejiuzulu
Michel Djotodia, rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliejiuzuluPicha: Getty Images/Afp/Miguel Medina

Rais Djotodia anayekosolewa na jumuia ya kimataifa kwa kuyafumbia macho mapigano kati ya waumini wa dini tofauti nchini mwake amejiuzulu hii leo kutokana na shinikizo la viongozi wa jumuia ya Uchumi ya nchi za Afrika ya kati walioitisha mkutano wa dharura katika mji mkuu wa Chad-N'Djamena.Vikosi vya Ufaransa vinapiga doria karibu na kasri la rais.

Hata waziri mkuu,Nicolas Tiangaye ambaye hakuwa na uhusiano mzuri na rais Michel Djotodia, amejiuzulu.Ripoti za kujiuzulu kiongozi wa zamani wa muungano wa makundi ya wanamgambio wa Seleka zimepokelewa kwa shangwe na furaha miongoni mwa wakaazi wa mji mkuu Bangui ambako milio ya hapa na pale ya risasi ilisikika.

Viongozi wa jumuia ya uchumi ya nchi za Afrika ya kati waliokuwa wakikutana tangu jana katika mji mkuu wa Chad,Ndjamena wamesema katika taarifa yao mwishoni mwa kikao chao cha dharura hii leo,"wanatilia maanani uamuzi wa kujiuzulu rais na waziri mkuu wa jamhuri ya Afrika kati wanaoutaja kuwa ni wa kizalendo ili kuikwamua nchi hiyo."Majadiliano kuhusu uongozi mpya wa mpito yatafanyika Bangui mnamo tarehe itakayopangwa baadae .

Rais wa Chad aweka shinikizo

Awali Rais wa Chad, Idriss Deby Itno, ambaye ndiyo mwenyekiti wa jumuiya hiyo, alifungua mkutano huo wa kilele kwa matamshi makali yanayoshinikiza Djotodia kuondoka madarakani au angalau atumie mamlaka yake vizuri. Deby ametaka hatua madhubuti zichukuliwe ili kumaliza mzozo huo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius na Rais Idriss Deby wa Chad
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius na Rais Idriss Deby wa ChadPicha: Getty Images

Katibu Mkuu wa ECCAS, ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Chad, Allami Ahmat alisema suluhisho la mzozo huo linapaswa kutoka kwa watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wenyewe. Ahmat amesema sio ECCAS wala jumuiya ya kimataifa itakayobadilisha utawala, bali ni jukumu la wenye nchi kuamua hatma yao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius amesema viongozi wa Afrika ndio wangechukua maamuzi kuhusu mustakabali wa Djotodia na siyo jukumu la Ufaransa kutoa maamuzi, kwani wao wako kwa ajili ya kutoa tu msaada. Thierry Vircoulon, kutoka taasisi ya kimataifa inayoshughulikia na mizozo, anazungumzia zaidi iwapo Jamhuri ya Afrika ya Kati itakuwa na utulivu kama Djotodia ataachia madaraka.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika vita baada ya kundi la waasi wa Seleka kuuangusha utawala wa Francois Bozize mwezi Machi mwaka uliopita na tangu wakati huo, zaidi ya watu 1,000 wameuawa na wengine wapatao milioni moja hawana makaazi kutokana na mapigano kati ya waasi Waislamu wa Seleka na wapiganaji wa Kikristo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Gakuba Daniel