1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka miwili ya uongozi wa Angela Merkel

Maja Dreyer21 Novemba 2007

Kila mwezi, gazeti moja maarufu la kila wiki la Ujerumani linachapisha uchunguzi wa maoni, wanasiasa gani wanapendwa zaidi na wananchi. Kwa muda mrefu sasa, Kansela Angela Merkel yuko kileleni mwa orodha hiyo.

https://p.dw.com/p/CQ7v
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani
Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: AP

Pia viongozi wa nchi nyingine wanamsifu bibi huyu ambaye ni Kansela wa kwanza wa kike katika historia ya Ujerumani. Hata hivyo serikali yake ya muungano inakabiliwa na hatari ya kupasuka. Maja Dreyer ana maelezo zaidi.

Akiwa msomi wa utaalamu wa fizikia na mwanasiasa wa kihafidhina, Bibi Angela Merkel aliingia katika cheo cha kansela mnamo mwezi wa Novemba mwaka 2005. Si tu Kansela wa kwanza wa kike bali pia kiongozi wa kwanza kutoka upande wa Mashariki mwa Ujerumani. Chama chake cha kihafidhina cha Christian Demokrats CDU kilipata wingi wa kura lakini si zaidi ya nusu ya kura zote, kwa hivyo ilibidi kiungane na chama kingine. Serikali basi iliundwa na CDU na chama kingine kikubwa cha Social Democrats, SPD.

Katika muungano huu, mpango wake wa kutekeleza mageuzi makali aliyoiahidi katika kampeni yake ya uchaguzi ilidhoofishwa kwa msimamo wa mshirika wake SPD - chama ambacho kinawapendelea wafanyakazi wa kawaida. Hata hivyo, uchumi iliimarika katika miaka ya hivi karibuni, lakini sifa inapewa hasa mtangulizi wa Angela Merkel, Kansela Gerhard Schröder wa SPD ambaye alitekeleza mageuzi makali licha ya upinzani kutoka kwa wanachama wenzake. Tangu hapo, idadi ya watu wasio na ajira ambayo kabla ya uchaguzi uliopita ilifika kiwango cha millioni tano imepungua hadi kufikia watu Millioni 3.4. Kiwango hiki ni cha chini kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 12 iliyopita. Pia bajeti ya Ujerumani inatarajiwa kuwa sawa baada ya miaka mingi ya kasoro.

Wadidisi wengi wanasema mafanikio ya Bibi Merkel yanatakana na uwezo wake wa kuzuia kuchukua msimamo wazi juu ya masuala muhimu kabla ya dakika ya mwisho kabisa. Huo unaonekana kuwa ni ustadi utamsaidia kupata kura na kuonyesha ushujaa wa kisiasa. Anajionyesha kama mama wa taifa na anawaachia mawaziri wa baraza lake kugombana juu ya masuala kabla ya yeye kujiingiza, kutathmini na kutoa uamuzi, mchambuzi mmoja alisema.

Mtaalamu mwingine wa chuo kikuu cha Berlin, Bw. Nils Diederich, anasema, Kansela Merkel anafuata desturi ya kisiasa iliyoibuka Ujerumani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia ya kupendelea masikilizano kuliko migogoro. Wapigaji kura wa Ujerumani wanataka nchi yao itawaliwe bila ya fujo, anasema Bw. Diederich.

Mtaalamu huyu anataraji msuguano utaonekana zaidi katika miaka miwili ijayo ya muhula wa serikali hii, hususan pindi chama cha SPD kitapoteza kura katika chaguzi nne za mikoa zitakazofanyika mwaka ujao wakati Kansela Angela Merkel ataweza kuimarisha uongozi wake.

Pamoja na ukuaji wa uchumi, Kansela Merkel ambaye mara mbili mfululizo gazeti la kichumi la Marekani “Forbes Magazin” lilimchagua kuwa mwanamke mwenye mamlaka zaidi duniani – nyumbani Ujerumani anajipatia vilevile sifa kutokana na sera zake za nje.

Aliweza kurekebisha mahusiano kati ya Ujerumani na Marekani baada ya mtangulizi wake Gerhard Schröder kumkasirisha rais Bush wa Marekani kwa kusema wazi anapinga kabisa vita vya Iraq. Merkel pia aliweza kuwashawishi viongozi wenzake wa Umoja wa Ulaya na nchi nane tajiri za dunia za kundi la G8 kujiwekea masharti ya kupunguza utoaji wa gesi chafu. Vilevile, alimkosoa rais Putin wa Urusi kwa ukiukaji wa haki za binadamu na uhuru wa wananchi kinyume na mtangulizi wake Bw. Schröder ambaye alimuita Putin “mwanademokrasia asiye na dosari”.

Hata hivyo, nyumbani mafanikio ya kisiasa siyo mengi ila tu mageuzi katika malipo ya wazazi, kuongeza umri wa kustaafu na kubadilisha mfumo wa afya. Kulingana na wachunguzi wa maoni, vyama vyote viwili vya serikali ya muungano ya Ujerumani havina haja ya kuita uchaguzi wa mapema. Ni kama katika ndoa isiyo na matatizo, wanasema. Wazazi wanakaa kwa pamoja kwa ajili ya watoto wao. Muda tu mpenzi mwingine anajitokeza, ndoa imekwisha.