1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka kumi ya harakati za Jeshi la Ujerumani

Erasto Mbwana30 Agosti 2005

Shirika la Kujihami la Magharibi NATO, siku mbili baada ya soko la Sarayevo kushambuliwa na watu kadhaa kuuawa, siku kama ya leo Agosti 30 mwaka 1995, limeanza mashambulio ya angani dhidi ya Waserbia. Wanajeshi wa Ujerumani, kwa mara ya kwanza kabisa, walishiriki katika mashambulio hayo. Hilo lilikuwa tukio la kihistoria kwani Wanajeshi wa Ujerumani, licha ya Kosovo na Afghanistan, wako pia katika nchi nyingine. Maelezo yafuatayo yanachunguza kwa makini miaka kumi ya harakati za kimataifa za Wanajeshi wa Ujerumani, Bundeswehr.

https://p.dw.com/p/CHey
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Peter Struck
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Peter StruckPicha: AP

Wanajeshi wa Kijerumani siku hizi wanachukuliwa kitaifa na kimataifa kuwa ni jeshi la uvamizi. Haya yote yanaweza kuthibitishwa na harakati zao katika Bosnia, Kosovo, Afghanistan na Pembe ya Afrika.

Lakini kusema kweli kutokana na mgawanyiko wa madaraka katika Jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, sura ni nyingine kabisa. Jukumu kubwa la theluthi mbili ya Wanajeshi wa Kijerumani linaendelea kuwa ulinzi wa nchi yao. Isipokuwa Wanajeshi 35,000 kati ya 250,000 wanaendesha harakati zao nje ya Ujerumani na katika nchi za Shirika la Kujihami la Magharibi (NATO).

Hapa lazima ikumbwe kuwa Wanajeshi wa Ujerumani kwa muda wa miaka kumi iliyopita walikuwa wakijishughulisha pia na harakati za kimataifa zinazohitaji silaha. Kupamba moto kwa vita vya Bosnia majira ya kiangazi mwaka 1995, mauaji ya kiholela ya Srebrenica na kushambuliwa kwa soko la Sarayevo kumesababisha mageuzi makubwa ya kihistoria katika jeshi la Ujerumani.

Wanasiasa wa Ujerumani kwa muda mrefu walikuwa wakikabiliwa na uamuzi mgumu kuhusu Wanajeshi wa Ujerumani kupelekwa katika harakati za kulinda amani. Wanajeshi wa Ujerumani walioko nchi za nje kutumia silaha bila ya Ujerumani yenyewe kushambuliwa kutokana na historia yake hakuruhusiwi. Kwa mfano kama vile Balkani eneo ambalo limeathirika kutokana na kukaliwa na Wajerumani wakati wa vita vya pili vya dunia.

Kuna masuala mawili hatimaye yaliyojitokeza baada ya miaka mingi ya mwenendo wa mazungumzo ya siasa za ndani ya nchi. Kwanza: wenye hatia siyo wale peke yao wanaofanya vitendo viovu isipokuwa pia wanaotumbua macho na kutofanya chochote kile wakati haki za Umma zinapokanyagwa.

Pili: Usalama na uimara wa Ujerumani unaweza pia kusambaratishwa na matokeo ya nchi nyingine. Kwa mfano, vita vya Bosnia vimesababisha Wakimbizi wengi kukimbilia nchini humu.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Peter Struck, miaka kumi baadaye leo anawachukulia Wanajeshi wa Ujerumani walioko Bosnia, Kosovo na Afghanistan kuwa ni jambo la kawaida.

Bila ya kujikanyagakanyaga anatumia maneno kama haya, „Usalama wa Ujerumani utalindwa pia Hindukush, Afghanistan“ au anafikiria siku zijazo uwezekano wa Wanajeshi wa Ujerumani kupelekwa barani Afrika.

Yule anayekumbuka maandamano ya Umma dhidi ya kuanzishwa Jeshi la Ujerumani miaka 50 iliyopita au upinzani mkubwa uliokuwako dhidi ya vita vya kuikomboa Kuwait mwaka 1991 lazima akumbushwe kuwa Wajerumani sasa wanayakubali majukumu mapya ya jeshi lao tokea miaka kadhaa iliyopita.

Kushiriki katika harakati za Bosnia mwaka 1995, Kosovo mwaka 1999 au Afghanistan mwaka 2001 hakujagubikwa na upinzani mkali au swali gumu kuhusu malengo ya Ujerumani kushiriki katika harakati kama hizo.

Kuna swali linalo washangaza Wajerumani na watu wengine ambalo mpaka hivi sasa bado halijajibiwa nalo ni hili: Je, Wanajeshi wa Ujerumani watarudi lini nyumbani kutoka Bosnia, Afghanistan au Kosovo ambako mpaka hivi sasa bado kuna Wanajeshi wengi?

Wanajeshi hao huenda wakarudi nyumbani hivi karibuni.

Lakini kutokana na ujuzi wa miaka kumi iliyopita tokea kuanza kwa harakati za Bosnia kuna somo tulilojifunza nalo ni hili: Anayewapeleka Wanajeshi wake katika harakati za kimataifa licha ya kuwa na nguvu za kijeshi anahitaji pia uvumilivu.