1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 80 tangu kuanzishwa Jeshi la Ukombozi la Umma wa Uchina.

31 Julai 2007

+ Jeshi la Umma wa Uchina, chini ya uongozi wa chama cha kikominsiti, ni jeshi la wananchi na ni nguzo ya taifa.+ Hayo aliyasema rais wa nchi hiyo, Hu Jintao, wakati wa kuadhimishwa mwaka wa 80 tangu jeshi hilo liundwe.

https://p.dw.com/p/CHAG
Rais Hu Jintao wa Jamhuri ya Umma wa Uchina.
Rais Hu Jintao wa Jamhuri ya Umma wa Uchina.Picha: AP

Muda mfupi kabla, waziri wa ulinzi wa Uchina alipendekeza jeshi la nchi hiyo lisiwe tena chini ya uongozi wa chama, lakini liwe chini ya serekali, jambo ambalo lilikataliwa. Wakati huo huo, Uchina inapiga kasi katika kujirundikizia silaha, jambo ambalo linakwenda sambamba na uchumi wa nchi hiyo kupanda juu sana. Hali hiyo inazitia wasiwasi nchi za Magharibi. Bajeti ya kijeshi ya nchi hiyo kwa mwaka huu, kwa mujibu wa tarakimu rasmi, inafikia dola bilioni 45, hilo ni ongezeko kubwa kabisa kuwahi kuonekana katika miaka kumi iliopita. Lakini Wamarekani wanaamini matumizi ya kijeshi ya Uchina yanagharimu mara mbili hadi mara tatu ya kima hicho kilichotajwa.Kwa umbali gani kuna ukweli wa kitisho hicho kinachozungumziwa juu ya Uchina?

Historia ya kijeshi ya Uchina ya kikoministi inaanzia Agosti Mosi mwaka 1927 pale huko Nanchang, katikati ya Uchina, pale majeshi ya kizalendo yaliokuwa yanawapendelea Wakoministi yalipoasi na kujiunga na Mao Zedong. Kutokana na huo ulioitwa uasi wa Nanchang, yalianza mapambano ya kisilaha baina ya Wakoministi na Wazeldno waliokuwa wanungwa mkono na Wamarekani, chini ya Chiang Kaishek. Kutokana na wananchi kuwaunga mkono, jeshi la kikoministi, au jeshi jekundu kama lilivokuwa linaitwa lilishinda mwaka 1949 na kuyalazimisha majeshi ya Kuomintang kukimbilia hadi kisiwani Taiwan.

Kwa muda mrefu jeshi la Umma, lilielezewa kama makumbusho ya zamani ya kijeshi, kutokana na silaha zake kongwe. Mwanzoni mwa miaka ya 90 serekali ya Uchina huko Beijing ilianza kwa dhati kulifanya jeshi la nchi hiyo liwe la kisasa. Kwa vile nchi hiyo ilijionea uchumi wake ukikuwa kwa haraka, pia matumizi yake ya kijeshi yalipanda kila mwaka kwa zaidi ya asilimia 10, jambo ambalo lililaumiwa huko Washington. Marekani walidai kwamba Uchina inajirundikizia silaha katika mazingira yalio ya amani, tena bila ya sababu. Lakini Profesa Eberhard Sandschneider, bingwa wa masuala ya Uchina katika Taasisi ya Ujerumani juu ya siasa za kigeni, anaiona lawama hiyo kuwa sio ya haki:

+Mtu anapoangalia gharama za ulinzi za Uchina na kuzilinganisha na zile za Marekani, basi ataona tafauti kubwa kwa maslahi ya Marekani. Mtu, hata kwa makisio ya juu kabisa, akisema kwamba Uchina inatumia dola bilioni 100 kwa mwaka katika kuufanya mfumo wake wa ulinzi uwe wa kisasa, basi Marekani inatumia dola bilioni 500. Mtu ataona kwamba tafauti baina ya gharama za matumizi za Marekani na Uchina sio inapungua, bali inazidi kupanuka. Huo upande mmoja. Upande mwengine ni kwamba nchi ambayo inaendelea, kiuchumi, hujenga pia uwezo wake wa kijeshi, hilo sio jambo lisilokuwa la kawaida.+

Pia huko Uchina kunatolewa hoja ambayo kwamba serekali ya nchi hiyo haichoki kuisisitiza kwamba juhudi zinachukuliwa katika sekta ya kijeshi ili kutimiza kwa uzuri zaidi majukumu yake ya kimataifa. Kati ya nchi tano zilizo wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Uchina ndio iliopeleka ngambo wanajeshi wengi kabisa wa kulinda amani. Katika kitabu kilichochapishwa mwisho wa mwaka 2006 juu ya kupunguza na kudhibiti silaha, Uchina iliashiria juu ya nia yake ya kutaka kuweko amani duniani. Waziri mkuu Wen Jiabo alisema:

+Tuna siasa ya kiulinzi ambayo inatumika tu kwa ajili ya ulinzi. Silaha zenye mipaka ambazo Uchina inazo ni za kutumika tu kwa ajili ya kulinda usalama, uhuru na heshima ya utawala wa nchi.+

Kuhusu heshima ya utawala, waziri mkuu huyo aliikusudia hasa Taiwan. Hiyo ilikuwa Machi mwaka 2005 pale ilipopitishwa na bung la Jamhuri ya Umma wa Uchina sheria ya kupinga kusambaratishwa Uchina na ambayo iliitishia Jamhuri ya Kisiwa cha Taiwan kwamba itashambuliwa, pindi itajitangaza kuwa huru. Hiyo itakuwa na maana ya kupigana na Marekani ambayo inajihisi inalazimika kuilinda Taiwan, pindi kisiwa hicho kitashambuliwa na Jamhuri ya Umma wa Uchina. Kwa hivyo Marekani inaingiwa na wasiwasi pale inapoiona Uchina inaufanya mfumo wake wa ulinzi, hasa wa baharini, kuwa wa kisasa. Jambo hilo linafanya wizani wa kiulinzi katika ujia wa bahari kati ya Taiwan na Uchina Bara kuwa kwa maslaha ya Jamhuri ya Umma wa Uchina. Kilichogonga vichwa vya habari karibuni ni zoezi la kufzianya za kisasa nyambizi zinazoendeshwa kwa nguvu za kinyukliya, maroketi ya masafa baina ya bara moja hadi jengine, aina ya Dongfeng 5, pamoja na satelite za Bedou. Zaidi ya hayo, pale Wachina mwezi Januari walipoifyetua hewani satelite kongwe ya kuchunguza hali ya hewa kwa kutumia roketi, gazeti la hapa Ujerumani, DIE WELT, lilizungumzia juu ya mfumo wa dunia unaosimamiwa na madola makuu mawili. Lakini bingwa wa Kijerumani wa masuala ya Uchina, Eberhard sandschneider, anahoji vingine:

+Satelite hiyo iliofyetuliwa haibadilishi hata kidogo mfumo wa nguvu za kijeshi duniani. Uchina imeujaribu uwezo wa kiteknolojia wa satelite hiyo, na kwa upande mwengine imetoa ishara ilio wazi, nayo: Tunaweza katika siku za mbele kulifanyia kazi jambo hilo na kuimiliki teknolojia hiyo. Lakini hiyo haina maana kwamba wizani wa nguvu za kijeshi umebadilika, ila ni kwamba mwenendo ulivyo ni kwamba hali hiyo itajitokeza. Hiyo ina maana kwamba Uchina haifuati siasa ya kujirundukizia silaha na kuubadilisha wizani ulioko ili kuwa ina nguvu za kijeshi, kama vile ilivyo Marekani. Lakini inafanya, kwa mfano, pale manuwari za Marekani zinapoweza kushambuliwa na nguvu za nyambizi, basi hapo Uchina inajaribu kujenga nguvu zake ili kufidia, kwa namna moja au nyingine, ule umbele wa nguvu za kijeshi za Marekani.+

Nguvu za Marekani ziko katika ule ukweli kwamba Uchina karibu imezungukwa kabisa na Wamarekani. Marekani ina ushirika wa asili na Japan, inaiunga mkono India ilio na nguvu za kinyukliya, ina ushirikiano wa kijeshi ulio wa karibu na Thailand, inaboresha uhusiano na Vietnam na ina vituo vya kijeshi katika Asia ya Kati. Kwa hivyo, siasa ya usalama ya Uchina inalazimika kushindana na ile ya Marekani.

Ndani nchini Uchina kwenyewe, Jeshi la Ukombozi wa Umma lililo na askari milioni 2.2 pia linapambana katika sekta nyingi. Ulaji rushwa umeenea ndani ya jeshi hilo. Rais Hu Jinatao hawezi na hataki kujiingiza kulizuwia jambo hilo, kwani kwanza anahitaji kuhakisha na kuimarisha mamlaka yake ndani ya jeshi. Kumetolewa miito pia kutoka jeshini kwamba kufanyike marekebisho nchini humo. Mazungumzo kwamba jeshi lisiwe tena chini ya chama, lakini liwajibike kwa dola, yalipata nguvu sana katika mkutano mkuu wa 17 wa chama tawala cha kikoministi. Mkosaji maarufu wa serekali ya Uchina, Chen Ziming, aliyaelezea hivi madai yanayotolewa:

+Kwanza, chama cha kikoministi lazima kijondoe kutoka jeshi. Pili, lazima iwekwe wazi nani anayewajibika ndani ya jeshi. Jeshi liwe taasisi ya dola ambapo wanasiasa watakuwa chini yake. Hiyo ina maana tume kuu ya kijeshi ya chama ivunjwe na pia tume ya kijeshi ya dola. Rais wa nchi au waziri mkuu atakuwa moja kwa moja mkuu wa jeshi. Hivyo katiba itabidi ibadilishwe kufuatana na matakwa hayo.+

Kwa hivyo jeshi la Uchina lina wakati mgumu mbele yake. Lakini, kwa mujibu wa Eberhard Sandschneider, dunia haina haja ya kuwa na wasiwasi:

+ Kwa ujumla, Uchina haijajionesha kuwa ni dola ilio ya uchokozi. Lakini mtu lazima atambuwe kwamba katika wakati mfupi ujao Uchina itakuwa na maslahi ya kujipanua na sura yake ionekane katika sehemu mbali mbali za dunia, hasa katika uwanja wa kutafuta nishati, na itahitaji msaada kutoka uwezo wake wa kijeshi kuyalinda maslahia hayo. Huenda kukatokea mambo ambayo kwetu sisi kwa sasa hayafikiriki. Muhimu ni tu jambo moja: Pale mtu anapotaka kukabiliana na Uchina na kuiangalia nchi hiyo kama kitisho na baadae kujijengea sura kwamba Uchina ni adui, basi, kutokana na uzoefu wa kihistoria, mwishowe inatokeza kwamba mtu huyo ataipata Uchina kuwa ni adui.+