1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 65 baada ya maangamizi ya wayahudi - HOLOCAUST

Abdu Said Mtullya27 Januari 2010

Maadhimisho ya ukombozi wa kambi ya AUSCHWITZ ambapo mafashisi waliwaangamiza wayahudi-HOLOCAUST, miaka 65 iliyopita.

https://p.dw.com/p/LiBn
Rais wa Israel Shimon Peres akihutubia bunge la Ujerumanii.Picha: AP

Rais Shimon Peres  wa  Israel  leo amesema kwamba wote waliotenda uhalifu wa kifashisti lazima  waadhibiwe.

Rais Peres amesema hayo katika hotuba aliyoitoa  kwenye  bunge  la Ujerumani kuadhimisha siku  ya kimataifa  ya kukumbuka kukombolewa  kwa kambi Auschwitz  ambapo  mafashisti  walitenda uhalifu  dhidi  ya ubinadamu  miaka 65 iliyopita.

Katika hotuba  yake, rais Peres  amesema wote  waliotenda uhalifu wakati wa utawala wa  mafashisti lazima  wafikishwe mbele  ya sheria.

Bwana Peres  aliwaambia wabunge  wa Ujerumani kwamba  maangamizi ya wayahudi-Holocaust - ni onyo la daima  na wakati huo huo   yanawapa binadamu wajibu wa  kuutukuza  uhai.

Rais Peres  amesema watu  walioshiriki katika  kutenda uhalifu huo mkubwa-Holocaust-  bado    wanaishi  Ujerumani, katika  nchi nyingine  za  Ulaya  na  katika sehemu  zingine za  dunia.

Amewataka  wabunge  wa  Ujerumani wafanye  kila wanaloweza ili wahalifu  hao wafikishwe  mbele  ya sheria.

Ameeleza  kwamba   mwito  wake siyo kitendo  cha  kulipiza  kisasi,  bali  ni  funzo.

Siku  kama ya leo, miaka 65 iliyopita, muda mfupi kabla  ya  kumalizika  vita kuu  vya  pili, askari  wa  kisoviet -Urusi ya  zamani , walifika  kwenye  kambi ya  Auschwitz ambapo  wahalifu   wa  kifashisti  walifanya maangamizi. Askari  hao walifika  kwenye kambi hiyo  nchini Poland baada ya watu zaidi ya milioni  moja  kuangamizwa.

Naye akizungumza katika kuadhimisha mwaka   wa 65  tokea  kukombolewa kwa watu  waliokuwamo  katika kambi  ya Auschwitz, Spika   wa bunge  la Ujerumani, Nobert  Lammert, aliirudia tena ahadi ya Wajerumani, juu ya kutosahau  yaliyotokea.

Amesema wajerumani  wataendelea kutekeleza  wajibu wa kupambana kwa uthabiti wote,na  aina   zote za chuki, ubaguzi, na chuki dhidi  ya  Wayahudi.

Bwana Lammert, amesema  kwa  Ujerumani, kuendelea  kuwapo  kwa  Israel, siyo  suala la majadiliano. Amesisitiza kwamba Ujerumani ina  wajibu kwa Israel.

27.01.2010 dw-tv journal tt ausschwitz Schimon Peres Horst Koehler 1
Marais Shimon Peres wa Israel na mwenyeji wake Horst Köhler.

Katika maadhimisho yaliyofanyika bungeni kuwakumbuka  wahanga  wa uhalifu wa mafashisti, pia walishiriki Kansela  Angela Merkel na rais wa Ujerumani, Horst Köhler.

Siku ya leo ya kukumbuka kukombolewa  kwa kambi ya Auschwitz inaadhimishwa pia kwenye kambi hiyo ya zamani  nchini  Poland ambapo  watu  zaidi ya  milioni moja , na hasa wayahudi  waliangamizwa  na mafashisti wakati  wa  vita kuu vya pili. 

Mwandishi/Mtullya Abdu/DPAEIEPD/LPD/ZA.

Mhariri: Miraji Othman