1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 60 tangu kukombolewa Kambi ya Mateso ya Auschwitz

25 Januari 2005

Auschwitz ilikuwa kambi kubwa kabisa ya mateso na ya kuwaangamiza watu, tena ya kutisha kabisa, iliojengwa na Wanazi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Katika kambi hiyo mauaji yalifanyika kwa ustadi wa kinyama. Vyumba vya gesi na matanuri makubwa ya kuchomea watu yalijengwa na kuwa viwanda vilivochukuwa si chini ya roho za watu milioni moja. Katika kilele cha mauaji hayo ya kiholela mnamo mwaka 1944, kila siku waliuliwa kwa gesi au kuchomwa moto hadi watu 6,000. Kwa mujibu wa kamanda wa kambi hiyo, Höss, hadi ya mabehewa mia moja ya gari moshi yalikuwa kila siku yakipita katika milango ya kambi ya Auschwitz, na mizigo iliobeba ilikuwa maelfu kwa maelfu ya wanadamu.

https://p.dw.com/p/CHhe
Elie Wiesel, mshindi wa tunzo la Nobel na aliyenusurika katika kambi ya Auschwitz, akiihutubia Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, New York.
Elie Wiesel, mshindi wa tunzo la Nobel na aliyenusurika katika kambi ya Auschwitz, akiihutubia Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, New York.Picha: AP

Ukimtajia mtu leo neno Auschwitz, basi moja kwa moja anayakumbuka mauaji ya kiholela na mateso yaliofanywa na Wanazi dhidi ya Wayahudi, Ma-Gipsy na makundi ya watu wengine wasiohesabika. Tarehe 27 Januari mwaka 1945, Ulimwengu unakumbuka kutimia miaka 60 tangu kambi ya Auschwitz ilipokombolewa.

Katika saa za asubuhi za tarehe 13 Januari, 1945, katika mstari wa medani yote ya vita ya Mashariki baina ya bahari ya Mashariki hadi Karpaten Warussi walianzisha mashambulio yao makubwa kabisa. Medani hiyo, iliokuwa na upana wa kilomita alfu moja, iliwaka moto.

Kila mita moja ambayo jeshi la Urussi liliweza kuikomboa, basi siku ya kuwa huru wafungwa 8,000 waliobakia katika Kambi ya Auschwitz ilikaribia.

Wiki mbili baadae, Januari 27 mwaka 1945 ilikuwa jumamosi. Ilikuwa mchana pale majeshi ya Urussi yalipowasili Auschwitz. Vikosi vya wanajeshi wa Kijerumani waliokuwa na vichwa ngumu waliendesha upinzani mkali. Wanajeshi 231 wa Kirussi waliuwawa katika kuikomboa kambi hiyo ya maangamizi. Watu walionusurika walikuwa zaidi ni wafu kuliko kuwa watu walio hai. 650 kati yao hawajaweza kushuhudia kukombolewa kwao.

Kile kilichofanyika Auschwitz hakijajulikana mara moja hadharani. Katikati ya April mwaka 1945, watu wengi walionusurika kutoka kambi hiyo waliripoti kwa Idhaa ya Kijerumani ya Radio ya Uengereza, BBC, namna mambo yalivokuwa katika kambi hiyo. Mmoja wao alikuwa ni Anita Lasker:Anasema:-

+ Walisimama daktari na kamanda wa jeshi pembeni pale mabehewa ya gari moshi yalipowasili, na mbele ya macho yetu watu waliotoka kwenye mabehewa hayo walikuwa wanachaguliwa. Watu haowaliulizwa umri wao na kuangaliwa hali zao za kiafya. Wale wasiojuwa nini kinafanyika walitaja magonjwa yanayowapatisha taabu, hivyo, kumbe walikuwa wanatia sahihi humu ya kuuliwa. Hasa katika kundi hilo walikuwemo watoto na wazee. Amri ilitolewa watu wajipange kwa mistrai, upande wa kulia na wa kushoto. Watu waliokuwa upande wa kulia maana yake wataishi, na wale waliokuwa upande wa kushoto maana yake watatiwa katika matanuri ya kuchomwa.+

Hapo Mei mwaka 1940, kambi ya kijeshi ya zamani, ilioko kilomita 60 kusini magharibi ya mji wa Krakau, huko Poland, ilikuwa ni makaazi ya wafungwa wa kisiasa. Mwaka 1941, kambi hiyo ilipanuliwa, na hapo ndipo ilipojengwa kambi ya Auschwitz- Birkenau. Katika mwaka huo, majeshi ya SS ya Wanazi yalijenga vyumba vya gesi ya Zyklon ambayo mwanzo ilikuwa ikitumika katika kuwauwa panya katika vumba kwenye meli. Akitumiwa dawa hiyo mwanadamu, basi huchukuwa dakika chache tu kabla ya kufa. Maiti za watu hao zilitiwa katika matanuri makubwa na kuchomwa. Nani yule ambayo anapofika tu pap hapo hutiwa katika chumba cha gesi na yule asiyefanyiwa hayo, ni jambo linaloamuliwa na madaktari pamoja na wanajeshi wa SS. Mmoja kati ya madaktari waliokuwa wanatoa uamuzi juu ya hatima ya watu hao ni Josef Mengele.

Yule ambayo aliishi, licha ya kufanyiwa vitendo hivyo, basi hufanyishwa kazi kwa nguvu. Kampuni ya IG Farben ilijenga kambi yake huko Auschwitz-Monowitz, na makampuni mengine, kama vile Krupps, yaliizunguka kambi hiyo. Watu wanaoingia katika kambi hiyo walikuwa hawaishi zaidi ya miezi mitatu. Charlotte Grunow, alitoka hai kutoka kambi hiyo, na pia akaelezea yale aliyoyaona kwa Idhaa ya Kijerumani ya Radio ya BBC. Ana haya ya kusimulia:-

+Kila wiki kulifanywa uteuzi. Kulitolewa mwito uliodumu saa nzima, watu wasimame mbele ya majengo hayo ya kutisha. Halafu huja daktari, mwenyewe Mengele, na huashiria kwa mkono mtu ambaye hamvutii; kwa mtu huyo huo ndio mwisho. Yeye hutafuta watu kwa ajili ya jengo Nambari Moja, Nambari Tatu na Nambari Tano. Watu hao hutakiwa wasimame kwenye mstari na hupelekwa kwenye jengo Nambari 25. Jengo Nambari 25 lilikuwa jengo la kuuliwa watu.+

Kufutilia mbali alama za mauaji ya kiholela yaliofanywa ili yasionekane na majeshi ya Warussi yaliokuwa yanasogea mahala hapo, majeshi ya SS ya Wanazi wa Kijerumani yaliviripuwa vyumba vya gesi na kuwahamisha wafungwa wengi wa Auschwitz. Kwa mfano, Charlotte Grunow na Anita Lasker walipelekwa Bergen-Belsen na huko walikombolewa na Waengereza katikati ya April , mwaka 1945. Majeshi ya SS ya Wanazi yaliwaacha nyuma yao huko Auschwitz wafungwa 65,000. Watu hao walikuwa wanaweza kusikia sauti za mizinga iliokuwa inafyetuliwa na wanajeshi wa Kirussi pale Janauri 18 walipopewa amri ya kusonga mbele.

Punde hivi, Umoja wa Mataifa umekumbuka kukombolewa kwa kambi ya Auschwitz. Ni wa-Israeli walioshikilia jambo hilo lifanyike. Bila ya shaka, walifanikiwa tu kwa kuungwa mkono na Marekani. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, John Danforth, alimuandikia katibu mkuu, Kofi Annan, na kumwambia kwamba ni muhimu kwa Umoja wa Mataifa kutoka majivu ya Vita vya Pili vya Dunia na Mauaji ya Kiholela kuikumbuka kambi iliowaangamiza Wayahudi milioni sita. Kanada, Australia, New Zealand, Russia, washirika katika ule Muungano ulipambana na Hitler katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na nchi za Jumuiya ya Ulaya ziliunga mkono kufanywa maadhimisho hayo ya kuikumbuka siku hiyo. Kofi Annan aliziandikia nchi wanachama ziamuwe, na Januari 11 mwaka huu msemaji wa Umoja wa Mataifa aliweza kutangaza kwamba nyingi ya nchi wanachama 191 wa Umoja wa Mataifa wamekubali kuitishwe kikao maalum cha Hadhara Kuu, zikiwemo nchi za Kiislamu kama vile Pakistan, Bagladesh, Oman na Moroko. Katika historia yake, Umoja wa Mataifa haujaikumbuka siku hiyo, licha ya kwamba utangulizi wa hati ya Umoja huo unataja juu ya kuamini haki ya kimsingi ya mwanadamu, heshima na thamani yake.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Joschka Fischer, amekwenda New York kuchanganyika na watu wengine kuikumbuka siku hiyo katika hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa, kuonesha huzuni yake na ya Wajerumani kwa unyama uliofanywa Auschwitz.

Miraji Othman