1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mhariri Mkuu DW: Rwanda ilikuwa na makovu mazito

8 Aprili 2014

Rwanda ilikuwa ni nchi yenye makovu mazito. Anasema hivyo Mhariri Mkuu wa DW Alexander Kudascheff ambaye alikuwako Rwanda mwaka 1994 akiwa mwandishi wa kwanza wa DW kurepoti baada ya mauaji ya halaiki nchini humo

https://p.dw.com/p/1BdyG
Mhariri Mkuu wa DW Alexander Kudascheff .
Mhariri Mkuu wa DW Alexander Kudascheff .Picha: DW/Matthias Müller

Katika mahojiano na Dirke Köpp wa DW anazungumzia juu ya fikra zake kuhusu mauaji hayo na dhima ya jumuiya ya kimataifa wakati huo na hivi sasa. Muda mfupi baada ya kutokea kwa mauaji hayo ya halaiki Kudascheff aliripoti kutoka Rwanda kwa ajili ya Deutsche Welle ambapo alizunguka nchini kote kwa kutumia gari na hadi Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakati huo ikijulikana kama Zaire kuona hali ya wakimbizi. Wakati huo waandishi wengi wa habari wa kigeni walikuwa hawako Rwanda bali walikuwa wakirepoti juu ya kile kilichokuwa kikitajwa kama balaa la wakimbizi huko Goma. Wale waliokuwa Rwanda utashi wao mkubwa ulikuwa msako wa wauaji wa Kihutu ambao walikuwa wamekimbilia mafichoni.

Akiwa na dereva wake kutoka Uganda wameitembelea nchi nzima na hadi hii leo jambo moja limekuwa na mvuto wa kudumu kwake:kwamba Rwanda ni nchi zuri ajabu na kujuwa kwamba watu wake ni wa kupendeka kweli licha ya kuwa kwenye hali ya kuathirika vibaya.

Umegunduwa kwamba watu nchini humo walikuwa wanapendeka ....jambo ambalo wasafiri wengi wamelizungumzia. Lakini wakati huo huo Wanyarwanda wengi wakati wa mauaji ya halaiki walidiriki kutenda unyama usiosemeka Uliweza kuitafakari vipi hali hiyo?

Yumkini tulikutana na wale waliokuwa wahanga.Kwa vyo vyote vile ni vigumu pia hata kufahamu vipi Wajerumani walithubutu kuwapeleka watu milioni sita ili wakauwawe kwenye vyumba vyenye gesi ya sumu.Nafikiri wakati huo nililiona jambo hilo kama aina fulani ya mripuko wa machafuko na wakati ulipomalizika watu walirudi tena kwenye fahamu zao.Rwanda ilikuwa ni nchi yenye makovu mazito.Wakati unapozunguka na gari unapishana na mrundiko wa mabufuru na unawasikia watu wakizungumzia juu ya jinsi ndugu zao walivyokufa au kuuwawa.Kila unapokuweko unagunduwa kwamba watu walikuwa wakitaka kuzungumzia juu ya kile kilichowakumba. Ulikuwa ukiona kile kiliomo mawazoni mwao,mchanganyiko wa furaha na aibu kwa kuweza kunusurika halikadhalika hofu juu ya mustakbali wao.Kipi kiko mbele yetu ?

Hata hivyo wakati wa mauaji hayo ya halaiki macho ya ulimwengu yalikuwa hayako kwa Rwanda. Pia kwa kuangalia yaliyopita kama mwandishi habari, mtu inabidi aone aibu kwa kutoweka nadhari kubwa juu ya kile kilichokuwa kinatokea nchini humo wakati huo.Lakini walioko kwenye nafasi za uwajibikaji wakati huo wana sababu ya kuona aibu zaidi:hususan Umoja wa Mataifa ambayo ilishindwa kabisa kuchukuwa hatua.Lakini vivyo hivyo kwa mataifa ya magharibi,Jumuiya ya Kujihami ya NATO na hasa Ubelgiji mkoloni wa zamani wa Rwanda.Ubelgiji ina uhusiano wa muda mrefu na Rwanda na pia walijiuliza wapi tulipokosea?Kwa nini hawakuweza kuyakomesha mauaji hayo ya halaiki au angalau kuyazwiya?

Paul Kagame amekuwa rais wa Rwanda tokea mwaka 200. Amekuwa akijaribu kuleta upatanishi,miongoni mwa mambo mengine kwa kupiga marufuku watu kujitambulisha kwa misingi ya ukabila. Una fikra gani kuhusu mtizamo huo?

Nakubaliana na fikra ya msingi kutofikiria kwa kuzingatia makundi ya kikabila.Kwa njia hii mtu huondokana na mila za kibaguzi. Lakini je hiki ni kitu kinachoweza kuamrishwa kutoka juu kwenda chini?Nchi za Kisoshalisti zimelijaribu jambo hilo mara kwa mara bila ya mafanikio kwa sababu mara tu ujamaa unapokuwa umeondoka matatizo yote ya utaifa huibuka upya.

Ningelichukuwa mtizamo tafauti kwa Paul Kagame.Kwa upande mmoja sera yake za kiuchumi ni za mafanikio makubwa.Kwa upande mwengine yeye ni kiongozi kutoka mojawapo ya makundi ya kikabila na sio rahisi kwa wengine kumkubali. Katika mahojiano niliyofanya na Kagame miaka mitano au sita iliopita alinipa hisia kuwa ni mtu mwenye amani na nafsi yake. Alionekana kuwa ni mtu ambaye yumkini alihisi kuwa yeye pia alikuwa amefanya makosa lakini aliamini kwamba sera zake zilikuwa muhimu na sahihi. Aidha hii iwe ndio hali ilivyo au iwapo makundi mawili ya kikabila yameondokana na tafauti zao ni jambo ambalo yumkini likadhihirika katika kipindi cha baada ya Kagame.

Wakati ilipokabiliwa na mauaji hayo ya halaiki hapo mwaka 1994 Jumuiya ya Kimataifa ilishindwa vibaya sana kuyakabili. Kutokana na kushindwa huko kukaibuka kanuni ya wajibu wa kutowa ulinzi.Kwa kiasi gani Jumuiya ya Kimataifa hivi sasa inatimiza wajibu huo?

Haitimizi wajibu huo. Kibahati sambamba na mauaji hayo ya halaiki tulikuwa na mzozo huko Balkan ambapo tulijiuliza masuali hayo hayo.Tamko mashuhuri la Katibu Mkuu wa zamani wa NATO Manfred Wörner kufuatia shambulio la kuvizia lililofanyika kwenye uwanja wa soko huko Sarajevo - "Wakati wa kuchukuwa hatua umefika" imekuja kuzama kwenye mawazo ya watu wengi.

Kiuadilifu nafikiri hakuna chochote cha mjadala hapa.Ilibidi kila kitu kifanyike kuwasaidia watu hao.Pia tulijiuliza wenyewe suala hili kwa kuangalia nyuma historia yetu. Je majeshi ya Muungano yalipaswa kushambulia njia za reli zinazoelekea kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz?

Ukiniuliza kama mwandishi habari mwangalizi kwa kutumia busara kutowa maoni ya dhati iwapo nafikiri kuingilia kati kungelisaidia na kuwa na maana kwa kuzingatia kipindi cha muda mrefu au kwa hatua ya kujenga taifa ingelinibidi niseme 'Hapana siamini ingelisaidia'. Unaweza kuingilia kati kwa muda mfupi kujaribu kutuliza hali, kujaribu kuzuwiya mripuko wa volkano wenye maafa.Lakini baada ya hapo inabidi uondoke haraka kadri inavyowezekana ili kwamba wale wanaoishi kwenye volkano hiyo waweze kukabiliana na hali hiyo wao wenyewe.Mwanzoni mambo yalikwenda vizuri Afghanistan na hata kwa wafanya kazi wa misaada lakini baadae katika mwaka 2004 au 2005 hali ilibadilika kabisa.

Kulikuwa na hatua za kuingilia kati zilizoshindwa kabisa kama vile Somalia na nyengine kushindwa kwa kiasi fulani kama vile Bosnia na mahala pengine ambapo matokeo yake bado hayako wazi mfano Kosovo.Hatuwezi kusema mambo yatakuwaje Jamhuri ya Afrika ya Kati au nchini Mali.

Baadae Jumuiya ya Kimataifa ilikuja kuendeleza uchunguzi kuhusu mauaji ya halaiki na kurudisha haki kwa kupitia Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa ajili ya Rwanda. Nchini Ujerumani na hata Ufaransa kesi za mauaji ya halaiki zimekuwa zikiendeshwa. Una mawazo gani juu ya majaribio haya yaliochelewa kukabiliana na kile kilichotokea?

Nafikiri ni vyema kwa dunia hii kwamba watu wanaohusika na uhalifu wa ukubwa huo wanakuwa hawana sababu ya kuamini kuwa wanaweza kuachiliwa bila ya kuadhibiwa.Hiyo ndio sababu kwa mfano kwa nini nafikiri kwamba mlinzi wa zamani wa kambi ya mateso ya Auschwitz mwenye umri wa miaka 90 bado anapaswa kushtakiwa.Kwani wakati fulani aliwahi kuwalazimisha hata watoto wadogo wa miaka miwili wakauliwe kwenye vyumba vya gesi ya sumu ........kwa hiyo kwangu mimi umri haujalishi.Kwa hiyo fikra ya kuwepo kwa Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu kuona kwamba dunia haitomuachilia mtu akwepe kuhukumiwa kwa uhalifu wa aina hiyo ni sahihi.Aidha mahakama hiyo ni ya mafanikio au la hilo ni suala jengine.Kwa vyovyote vile wengi wa wahalifu hao wako huru na wanakwenda watakako tena chini ya uwezo wa Jumuiya ya Kimataifa kuwatia nguvuni. Wengi hawashtakiwi hadi pale hali zao zinapodoofika. Wengine katu hawakuwahi kabisa kufunguliwa mashtaka.

Mwandishi : Dirke Köpp/Mohamed Dahman
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman