Mgomo wasimamishwa Nigeria | Matukio ya Afrika | DW | 13.01.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Mgomo wasimamishwa Nigeria

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyakazi nchini Nigeria amesema kwamba mgomo utasimamishwa kwa siku mbili ili kuwapa watu muda wa kumpumzika, huku Ujerumani nayo ikisema inayafuatilia matukio ya Nigeria kwa wasi wasi.

Maandamano ya kupinga kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta nchini Nigeria.

Maandamano ya kupinga kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta nchini Nigeria.

Mwenyekiti huyo, Abdulwahed Omar, amesema leo (13.01.2012) kwenye mkutano wa hadhara mjini Abuja kwamba mgomo ambao umekuwa unaendelea kwa siku ya tano nchini kote utasimamishwa kwa muda hapo kesho na Jumapili ili kuwapa watu muda wa kupumzika.

Mwenyekiti huyo amesema viongozi wa jumuiya ya wafanyakazi wamepitisha uamuzi huo baada ya kutafakari hoja kadhaa. Ameeleza kuwa baada ya kumpumzika, watu watarejea katika mgomo wakiwa na nguvu mpya.

Leo ni siku ya tano tokea watu nchini Nigeria waanze kufanya mgomo ili kupinga hatua ya serikali ya kuondoa ruzuku iliyokuwa inafidia bei ya mafuta .

Omar amesema ikiwa serikali ya Rais Goodluck Jonathan haitaubadilisha uamuzi wake wa kuondoa ruzuku ulioanza kutekelezwa tarehe 1 Janauri, jumuiya yake itarejea mitaani Jumatatu na nguvu kubwa zaidi kwa maandamano yatakayokuwa makubwa kuliko yote yaliyowahi kufanyika hadi sasa.

Wawakiishi wa vyama vya wafanyakazi wanatazamiwa kukutana tena na Rais Jonathan hapo kesho kwa ajili ya mazungumzo zaidi baada ya mkutano wa kwanza kushindwa kuleta mapatano.

Mwandishi: Mtullya Abdu/RTRE/
Mhariri: Othman Miraji