1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpinzani aapishwa kuwa mkuu wa mkoa Tanzania

6 Juni 2017

Rais John Magufuli wa Tanzania ametetea hatua yake ya kumteua aliyekuwa mgombea wa urais na mwenyekiti wa chama upinzani cha ACT-Wazalendo, Bi Anna Mghwira, kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro.

https://p.dw.com/p/2eCBQ
Anna Mghirwa, Präsidentschaftskandidatin der ACT in Tansania
Picha: ACT/Wazalendo

Rais Magufuli, ambaye leo mchana (Juni 6) amwemwapisha mkuu huyo mpya wa mkoa, amesema mwanasiasa huyo wa upinzani ameweza kujipambanua na kuonyesha tofauti kubwa na wanasiasa wengine wa upinzani.

Huku akiwashutumu wanasiasa hao 'wengine' kama ni watu wa kupinga kila jambo, alimtaja Mghwira, aliyekuwa mgombea pekee mwanamke kwenye nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi wa 2015, kama mwanasiasa anayeona mbele na mwenye kujua kile anachokifanya.

"Nenda kafanye kazi ya kuwatumikia watu wa Kilimanjaro maendeleo. Najuwa wewe unaweza," alisema Rais Magufuli mara tu baada ya kumuapisha Mghwira katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Uteuzi huo wa Rais Magufuli umezusha gumzo kubwa kutoka kwenye makundi ya kisiasa, huku wengine wakihoji hatima ya chama cha ACT-Wazalendo ambacho miezi ya hivi karbuni kiliondokewa na mwanasiasa wake mwingine machachari, Profesa Kitila Mkumbo ,aliyeteuliwa na Rais Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Ingawa baadhi ya wachambuzi wameanza kudadisi kuwa wapinzani wote walioteuliwa katika uongozi wa awamu ya tano ni wale wanaotoka chama kimoja pekee, lakini Rais Magufuli aliwahi pia kumteuwa mgombea mwengine wa urais kwa tiketi ya chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, kuwa mkuu wa parole.

Bi Mgwira anakwenda kuwa bosi wa mkoa wa Kilimanjaro, mkoa ambao ni ngome muhimu ya chama cha upinzani, CHADEMA, kilichoshinda majimbo mengi ya ubunge na viti vya udiwani.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ameliona hilo na amewasihi wanasiasa wenzake kwenye eneo hilo kumuunga mkono akiamini kuwa kazi aliyotumwa ni kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wote.

"Mimi si mpinzani wa maendeleo na wala maendeleo hayana chama cha kisiasa. Nitajitahidi kutimiza wajibu wangu," alisema Mghwira baada ya kula kiapo.

Rais Magufuli amemtaka mteule wake huyo kwenda kusimamia vyema maendeleo kwa kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Picha zilizotolewa mchana wa leo na Ikulu zilimwonyesha Mghwira akikabidhiwa ilani ya CCM huku akishuhudiwa na viongozi wengine akiwamo Rais Magufuli mwenyewe na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Mkuu huyo wa mkoa amepangwa kuwasilini Kilimanjaro hapo kesho tayari kuwa kuanza majukumu yake mapya.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef