1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Yemen wazidi kuzusha wasiwasi Kimataifa

-21 Januari 2015

Taarifa zinasema rais Mansur Hadi amekutana na mwakilishi wa wapiganaji wa Houthi ikiwa ni siku moja baada ya wapiganaji wa kundi hilo la washia kuiteka ikulu

https://p.dw.com/p/1ENvw
Waasi wa Houthi wakivamia ikulu ya rais mjini Sanaa
Waasi wa Houthi wakivamia ikulu ya rais mjini SanaaPicha: REUTERS/Khaled Abdullah

►Hata hivyo duru hazijaeleza hadi wakati huu nini kilichozungumzwa kati ya rais Hadi na mwakilishi húyo.Pamoja na hayo kuna taarifa za kufungwa uwanja wa ndege mjini Aden kusini mwa Yemen pamoja na kutekwa nyara kambi ya kijeshi inayotumiwa kuhifadhi makombora ya masafa marefu.

Taarifa zimesema rais Mansur Hadi amempokea Saleh al-Samad katika makaazi yake huko magharibi mwa mji mkuu Sanaa huku ikitajwa pia rais huyo alikutana na washauri wengine pamoja na machifu wa kikabila,ingawa kilichozungumzwa hakikutajwa.

Mapambano makali ya kuidhibiti ikulu 19.01.2015
Mapambano makali ya kuidhibiti ikulu 19.01.2015Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com

Sammad alikuwa ni mshauri wa rais Hadi chini ya makubaliano yaliyotiwa saini septemba 21 wakati wahouthi walipotwaa mamlaka ya mji mkuu Sanaa. Hata hivyo kuna mkutano mwingine mkubwa zaidi utakaowajumuisha wawakilishi wa pande zote za kisiasa utakaofanyika baadae leo(21.01.2015) mbele ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa Jamal Benomar.

Mazungumzo hayo yanakuja katika wakati ambapo Jumanne yalishuhudiwa mapigano makali kati ya wanamgambo hao wahouthi na wanajeshi wanaolinda makaazi ya rais wakati huohuo ikitajwa kwamba wapiganaji hao waliiteka ikulu ya rais. Leo Jumatano pia washauri wawili wa rais Hadi wametoa taarifa zinazosema kwamba waasi hao wakishia wanaoendeleza mapambano ya kuwania madaraka wanamshikilia mateka rais Hadi nyumbani baada ya hapo jana kuidhibiti Ikulu.

Rais Abed Rabbo Mansur Hadi
Rais Abed Rabbo Mansur HadiPicha: picture-alliance/dpa

Jumuiya ya Kimataifa imeingiwa na wasiwasi juu ya ulipofikia mgogoro huu,baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha dharura jana jioni kulaani ghasia zinazotokea na kutoa mwito wa kufikiwa amani ya kudumu.Marekani imesema inaendelea kumuunga mkono rais Hadi na serikali yake na kutoa mwito wa kusitishwa vita mara moja.Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Mark Lyall Grant pia ametoa mwito kama huo.

Wanachama wa baraza la ushirikiano wa nchi za Ghuba limewataka waasi wa Houthi kuondoka mjini Sanaa.Wakati huohuo rais aliyeondolewa kwa nguvu madarakani nchini humo Ali Abdalla Saleh ambaye anatajwa kuwa nyuma ya waasi hao wa Houthi amemshauri rais Hadi kupitia taarifa fupi kuitisha uchaguzi wa mapema ili kuepusha balaa kubwa zaidi.Kiongozi wa waasi Abdel-Malek al-Houthi aliyehutubia taifa jana usiku alisema kinachotokea ni hatua ya mapinduzi inayolenga kumlazimisha rais Hadi atekeleze makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa ambayo yanatoa madaraka makubwa zaidi kwa wahouthi.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri:Iddi Ssessanga