1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Congo ulipuuzwa kabisa mwaka wa 2017

Bruce Amani
20 Desemba 2017

Huku mamilioni ya watu wakiwa ukingoni mwa maafa makubwa ya kibinaadamu na watoto wakikabiliwa na ukatili wa kinyama, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndio ulikuwa mgogoro uliopuuzwa zaidi katika mwaka wa 2017

https://p.dw.com/p/2pgS9
Angola Flüchtlingslager nahe Kakanda
Picha: DW/N. Sul d'Angola

Huku ikiwa imegubikwa na vita vya Syria na mmiminiko wa wakimbizi wa jamii ya Warohingya kutoka Myanmar, Congo haikugonga vichwa vya habari licha ya ukatili wa kinyama unaofanywa katika mkoa wa kati mwa nchi hiyo.

Katika uchunguzi wa Wakfu wa Thomson Reuters Foundation uliofanywa mashirika 20 makuu ya misaada, Jamhuri ya Afrika ya Kati, na Yemen – ambayo inakumbwa na vita na njaa – ziliifuata Congo kwenye orodha hiyo.

Mkuu wa shirika la World Vision Mark Smith anasema mgogoro mkubwa wa kibinadamu umekuwa ukijitokeza bila kutambuliwa.

Demokratische Republik Kongo Unterernährtes Kind
Wengi wanateseka na njaa katika jimbo la KasaiPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Uasi dhidi ya seikali katika jimbo la Kasai umesababisha zaidi ya watu milioni moja kupoteza makazi katika kile Baraza la Wakimbizi la Norway linaita kuwa ni „mgogoro mkubwa".

Uhaba wa chakula umewaacha mamilio ya watu wakiteseka kwa njaa, huku mamia kwa maelfu ya watoto wakiwa katika hatari ya kufa.

Mashirika yamepokea ripoti za mauaji ya watu wengi, ubakaji na watu kukatwa vichwa. Pia kumekuwa na ripoti za kufanywa mashambulizi ya kinyama kwa watoto wachanga.

Watoto wa hadi umri wa miaka 10 wameingizwa kwenye makundi ya wapiganaji, wakati wengine walioachwa yatima wanalala peke yao misituni.

Mashirika yanasema barabara mbovu na changamoto ya mawasiliano ya simu vimefanya hali kuwa ngumu kufika katika eneo hilo, hali inayochangia eneo hilo kutosikika.

Mikoa ya mashariki mwa Jamhuri ya Congo pia iko katika hali tete. Kote nchini humo, watu milioni 13.1 wanahitaji msada, ambapo karibu thuluthi moja wameachwa bila makazi.

Demokratische Republik Kongo UN Friedenstruppe in Kinshasa
Jeshi la kulinda amani likipiga doria KinshasaPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompeng

Shirika la Oxfam liliitaja Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa "mgogoro uliosahaulika kabisa kati ya migogoro iliyosahaulika” ambapo watu milioni 2.4 wanahitaji msaada katika nchi ambayo watu wengi hata hawaijui.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia wakimbizi – UNHCR limesema watu milioni 1.1 – ambao ni karibu robo ya jumla ya idadi ya watu nchini humo – wameathirika na mzozo wa nchini humo, na kuonya kuwa hali hiyo inaweza kuwa mbaya kabisa kama hakutakuwa na ufadhili mkubwa.

Ijapokuwa Yemen imegonga vichwa vya habari mwaka huu, mashirika yamesema kuwa uangaziwaji uliofanywa na vyombo vya habari haukuanza kuonyesha ukubwa wa kile kinachotokea. Shirika la Uingereza la Action Against Hunger – limesema ukosefu wa uhamasisho wa umma, unaogofya ikizingatiwa kiwango cha mateso wanayopitia raia.

Mashirika mawili yaliutaja mgogoro wa watu kupoteza makazi katika kanda ya Ziwa Chad. Uasi wa Boko Haram wa miaka nane umeathiri mamilioni ya watu. Wakati Nigeria ikiangaziwa sana, Shirika la Plan International liliitaja athari iliyopo kwa jirani yake aliyesahaulika Niger ambako watu 400,000 wanahitaji msaada.

Na huku uhaba wa chakula ukitishia mamilioni ya watu nchini Nigeria, Sudan Kusini, Somalia na Yemen, shirika la Mercy Corps lilisema njaa ndio mgogoro uliopuuzwa kabisa mwaka huu.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters
Mhariri: Caro Robi