1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Afghanistan na Pakistan wahitaji suluhisho la dharura

18 Machi 2009

Mzozo wa mpakani kati ya Pakistan na Afghanistan si mpya,kwani unaendelea tangu kuundwa taifa la Pakistan miaka 62 iliyopita. Kwa hivyo kuna dharura ya kutafutwa suluhisho la kisiasa.

https://p.dw.com/p/HEkN

Mgogoro huo wa mpakani unaoendelea tangu wakati huo, unahusika na eneo lililo kati ya nchi hizo mbili na kujulikana rasmi kama Wilaya ya Kakazini-Magharibi ya Pakistan.Eneo hilo lina sifa mbaya ya kujulikana kama ni kitovu cha makundi ya kigaidi yenye sera kali kama vile Taliban na Al-Qaeda. Walio na usemi katika wilaya hiyo ni mkuu wa Taliban Mullah Omar na wafuasi wake. Mashambulio yanayofanywa dhidi ya Pakistan na hata huko Afghanistan hupangwa katika eneo hilo la mpakani. Waafghanistani wengi wanaamini amani haitopatikana katika kanda hiyo ya Asia ya Kusini ikiwa mgogoro kati ya Afghanistan na Pakistan hautopatiwa ufumbuzi.

Kiasi ya watu milioni 22 wanaishi katika Wilaya ya Kaskazini-Magharibi nchini Pakistan,wengi wao wakiwa wa kabila la Pashtu. Eneo hilo linajulikana kutumiwa kama maficho ya wakuu wa magaidi wanaosakwa- Mullah Omar na Osama Bin Laden. Huko Wataliban wanazidi kujiimarisha na hivi sasa si kitisho kwa mchakato wa amani nchini Afghanistan pekee bali wanahatarisha umoja wa kitaifa nchini Pakistan vile vile. Wakati huo huo,Kabul na Islamabad zinalaumiana kuzuia maendeleo kupatikana katika kanda hiyo.Lakini mtaalamu wa masuala ya Pakistan na Afghanistan, mwandishi wa habari Rahimmullah Samandar anazilaumu pande zote mbili.

O-TON: SAMANDER:

"Hali ya kutoaminiana daima imeathiri uhusiano kati ya Pakistan na Afghanistan. Rasmi,pande hizo mbili husema kuwa zinashirikiana na zinafanya majadiliano lakini kisiri mara nyingi hutenda vingine kabisa."

Mgogoro huo umezuka mwaka 1947 lilipoundwa taifa jipya la Pakistan. Kwani Afghanistan ilikataa kulitambua eneo lililokuwepo kati ya mataifa hayo mawili baada ya mkoloni Muingereza kulitenga kiholela eneo la Wapashtu katika karne ya 19 ili liweze kudhibitiwa bora zaidi. Serikali ya Afghanistan ya wakati huo,ilijaribu kuwachochea Wapashtu waliokuwepo upande wa pili wa mpaka kuasi dhidi ya serikali ya Islamabad. Juhudi hizo hazijafanikiwa na badala yake ni wakaazi wa pande zote mbili za mpaka wanaoteseka hadi hii leo. Mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan Profesa Sayfuddin Sayhun anasema kuwa njia pekee ya kujitoa katika janga hilo ni kutafuta suluhisho la kisiasa kuumaliza mgogoro huo wa mpaka ama sivyo, kanda hiyo kamwe haitokuwa na amani.

Mwandishi: R.Shamel/P. Martin( ZR)

Mhariri: Miraji Othman