1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro kisiwani Madagascar

Oumilkher Hamidou10 Machi 2009

Juhudi za upatanishi zashika kasi huku kiongozi wa upinzani akilindwa na Umoja wa mataifa

https://p.dw.com/p/H92U
Mkuu wa upande wa upinzani Andry RajoelinaPicha: AP


Umoja wa Mataifa umesema,mkuu wa upande wa upinzani kisiwani Madagascar,Andry Rajoelina,amewekwa chini ya ulinzi wao,katika nyumba moja ya kibalozi ,baada ya kuingia mafichoni kwa siku kadhaa,kwa hofu ya kukamatwa na vikosi vya usalama.


"Umoja wa mataifa umeamua kumlinda Rajoelina na kumuweka katika nyumba ya ubalozi" amesema hayo mpatanishi wa Umoja wa mataifa kisiwani Madagascar,Drame Tiebilé jana usiku.


Tiebilé,aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nchi zta nje wa jamhuri ya Mali,ameongeza kusema amehakikishiwa na rais Marc Ravalomanana kwamba Rajoelina hatokamatwa.


Mjumbe huyo wa Umoja wa mataifa hakutaka kufafanua wapi hasa anakutikana kiongozi huyo wa upande wa upinzani.


Mjumbe huyo wa Umoja wa mataifa ametoa taarifa hiyo wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari ulioitishwa na baraza kuu la makanisa ya kikristo ya Madagascar mjini Antananarivo.


Baraza hilo lenye ushawishi mkubwa kisiwani humo linasimamia juhudi za upatanishi za Umoja wa mataifa na mabalozi wa kutoka nchi kadhaa.


Taarifa ya pamoja iliyochapishwa na baraza  kuu la makanisa ya Madagascar na Umoja wa mataifa ,inazungumzia juu ya kuitishwa mkutano maalum kuanzia march 12 hadi 14 ijayo kujaribu kumaliza mzozo unaoikumba Madagascar.


Wawakilishi wa rais Ravalomanana na mpinzani wake Rajoelina,wawakilishi wa polisi,jeshi,sekta ya kiuchumi na kijamii wanatazamiwa kushiriki katika mkutano huo.


Baraza kuu la makanisa na Umoja wa mataifa umezitolea mwito pande zote zinazohusika zijizuwie ili kurahisisha kupatikana ufumbuzi wa mgogoro wao.


Mvutano kati ya rais Ravalomanana na mpinzani wake Meya wa zamani wa jiji la Antananarivo Rajoelina umebadilika na kuchukua sura nyengine kabisa.Watu wasiopungua 135 wameuwawa kufuatia machafuko yaliyoripuka tangu january 26 mwaka huu.


Mjini Antananarivo,afisa mmoja wa kijeshi na wafuasi wake amejifungia katika kambi ya CAPSAT na kulaani kile anachokiita vitendo vya"kuwakandamiza raia".Afisa huyo amekanusha hata hivyo uvumi kwamba kuna uasi jeshini


Jumapili iliyopita wanajeshi wanaoasi walizifunga njia zote kuelekea kambi ya CAPSAT inayoangaliwa kama moyo wa jeshi la Madagascar.


Waziri wa ulinzi Mamy RANAIVONIARIVO amejiuzulu hii leo kufuatia machafuko jeshini.


Jana wapinzani elfu tano walikusanyika kwa amani katika uwanja wa may 13.Hata hivyo maduka yalivunjwa katika mtaa mmoja wa kusini mwa mji mkuu.