Mfumo wa elimu Ujerumani ulalamikiwa | Magazetini | DW | 22.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Mfumo wa elimu Ujerumani ulalamikiwa

Mada moja kwenye safu za wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo ni ripoti iliyotolewa jana na Umoja wa Mataifa ambayo inailalamikia Ujerumani kuhusiana na mfumo wake wa elimu. Ripoti hii inasema, kwa kuwa na aina tatu za shule baada ya shule ya msingi, watoto wa asili ya kigeni na watoto walemavu wanabaguliwa katika mfumo huu.

Tunaanza na maoni ya wahariri juu ya ripoti ya mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa, Vernor Munoz, juu ya hali ya elimu nchini humo. Gazeti la “Tageszeitung” kutoka Berlin linamuunga mkono Bw. Munoz likiandika:

“Sasa taasisi ya juu kabisa imedhibitisha yale ambayo mawaziri wetu wa elimu kawaida wanakanusha, yaani kwamba humu nchini watoto fulani wanabaguliwa kwa sababu tu wanatoka nchi nyingine. Hivyo, mfumo wetu wa elimu unawazuia wageni waweze kujijumuisha katika jamii hii.” - ni gazeti la “Tageszeitung”.
Tukienda lakini kwa mhariri wa “Frankfurter Allgemeine Zeitung”, yeye ana mashaka juu ya ukweli wa ripoti hiyo. Anaandika:
“Mwakilishi huyu wa Umoja wa Mataifa Bw. Munaz anaamini anaweza kuchunguza hali fulani katika muda wa wiki moja, pale ambapo uchunguzi kama huu unashughulisha wanasayansi miaka kumi au zaidi. Huo ni udanganyifu.”

Na hatimaye kuhusu suala hilo ni gazeti la “Märkische Oderzeitung”:

“Tatizo si ripoti ya Bw. Munoz, bali ni kwamba hali haiboreki hapa nchini. Hilo si kosa la walimu au wanasiasa tu. Lakini inaibidi jamii kwa jumla kufahamu umuhimu wa elimu na kuipa zaidi kipaumbele.”

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamezingatia pia siku ya maji duniani. “Obermain-Tagblatt” limeandika:

“Ikiwa mwanamke barani Afrika anatembea kilomita kadhaa kupata maji, anafahamu thamani ya maji ni kubwa. Lakini yule ambayo anafungua tu bomba la maji hajui hali ya kukosa maji ya kunywa au kuoga. Siku hii ya maji duniani ikumbushe basi thamani ya maji na isaidie kuleta mawazo mapya. Maji ya mvua kwa mfano yaweza kutumika kwa mahitaji ya chooni au kumwagilia mimea. Pia mabomba ya zamani mengi yamevunjika na hivyo maji yanatoka. Masuala ya maji yapewe kipaumbele katika siasa za mikoa.” - ni gazeti la “Obermain-Tagblatt”.

Na mwishowe tunaelekea siasa za kimataifa: Siku moja kabla ya waziri wa nchi za nje wa Marekani, Bi Condoleezza Rice, kuondoka kwa safari yake nyingine ya Mashariki ya Kati, gazeti la “Süddeutsche Zeitung” linachambua sera za nchi za Magharibi kuelekea Palestina. Laandika:

“Si Umoja wa Ulaya wala Marekani zinaweza kuendelea kuisusia serikali ya Wapalestina. Baada ya kugomewa kwa mwaka mmoja, serikali ya Hamas ililazimishwa kugawana mamlaka yake. Lakini gharama ya ususaji huu ilikuwa kubwa sana. Uchumi katika maeneo ya Palestina umeharibika, na hivyo, Wapalestina wamekatishwa tamaa na siasa. Kuendelea kuwasusia Wapalestina hakutaleta tena faida yoyote.”

 • Tarehe 22.03.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHTR
 • Tarehe 22.03.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHTR