1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme wa Qatar aahirisha kuhutubia taifa

Lilian Mtono
6 Juni 2017

Mfalme wa Qatar ameakhirisha hotuba yake kwa taifa iliyotarajiwa leo hii kufuatia hatua ya ghafla ya kutengwa kidiplomasia na baadhi ya mataifa makubwa ya Kiarabu, ili kuipa nafasi Kuwait kuandaa mazungumzo ya upatanishi

https://p.dw.com/p/2eAzT
Katar Emir Scheich Tamim bin Hamad Al-Thani
Picha: picture-alliance/AP Photo/O. Faisal

Aidha, Rais wa Uturuki Recep Tayipp Erdogan kwa upande wake amezungumza na mataifa muhimu yaliyoitenga Qatar kama moja ya hatua za kusaka suluhu.

Katika ishara ya madhara yanayoweza kuukumba uchumi wa Qatar, mabenki kadhaa katika ukanda huo yalianza kujiondoa kufanya biashara na Qatar.

Waziri wa masuala ya kigeni wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al-Thani amesema Doha iko tayari kuunga mkono hatua za kutafuta upatanishi baada ya Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Bahrain kukata mahusiano ya kidiplomasia katika hatua ilioratibiwa kwa pamoja. 

Walisema wanavunja mahusiano hayo kwa madai kwamba Qatar inaunga mkono makundi ya wapiganaji ya Kiislamu na Iran, suala ambalo Qatar yenyewe imepinga vikali. Yemen, serikali ya Libya iliyojikita katika eneo la Mashariki la nchi hiyo na kisiwa cha Maldives walijiunga na mataifa hayo baadae na kukata mahusiano ya usafirishaji na Qatar.

Mfalme wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani alizungumza kwa njia ya simu usiku wa jana na mwenzake wa Kuwait, ambayo imeendeleza mahusiano yao na Qatar na kuamua kuahirisha hotuba yake, waziri huyo wa masuala ya kigeni amekiambia kituo cha Televisheni chenye makao yake Qatar cha Al-Jazeera. Lakini pia Qatar imeamua kutolipiza kisasi dhidi ya hatua hiyo ya majirani zake, amesema.

Rais Erdogan wa Uturuki aanzisha hatua za mazungumzo.

Türkei - AKP-Parteitag - Präsident Recep Tayyip Erdoğan
Rais wa Uturuki, Recep Tayipp Erdogan ataka mazungumzo kumaliza mzozo uliopoPicha: picture alliance/abaca/K. Ozer

Msemaji wa Rais wa Uturuki Racep Tayyip Erdogan pia amesema rais huyo ameanzisha hatua za kidiplomasia za kusuluhisha mvutano uliopo baina ya mataifa hayo rafiki katika wakati ambao pia wanaungana kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, amesema msemaji huyo Ibrahim Kalin katika taarifa iliyotolewa jana Jumatatu.

Hata hivyo Erdogan hajasema chochote kuhusu mzozo huo, ingawa siku ya jananaibu waziri mkuu Numan Kurtulmus alisema tayari Erdogan ameanza mawasiliano na baadhi ya mataifa muhimu. 

Alizungumza kwa njia ya simu na Mfalme wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani, Mfalme wa Kuwait Sheikh Sabah al-Ahmad al -Jaber al-Sabah an Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudi Arabia, hii ikiwa ni kulingana na taarifa zilizotolewa shirika la habari la serikali la Uturuki, Anadolu. 

Erdogan alijadili pia mzozo huo na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ambao unatajwa kuwa mkubwa zaidi kutokea katika ukanda huo baada ya miaka mingi.

Hatua hiyo iliyofikiwa jana Jumatatu, inawazuia raia wa Bahrain, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu kusafiri kwenda Qatar, kuishi huko ama kupitia nchi hiyo. Raia na wageni wa nchi hizo walitakiwa kuondoka Qatar ndani ya siku 14. Raia wa Qatar nao walipewa siku 14 kuondoka kwenye nchi hizo.

Hatua hii ni mbaya zaidi ikilinganishwa na iliyofikiwa katika mzozo uliodumu kwa miezi nane wa mwaka 2014, ambapo Saudi Arabia, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu waliwaondoa mabalozi wao Qatar, wakati huo pia wakiituhumu kwa kusaidia makundi ya wapiganaji. 

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri:Iddi Ssessanga