1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ziarani Marekani

Maja Dreyer9 Novemba 2007

Baada ya rais wa Ufaransa, Nikolas Sarkozy, amemtembelea rais George Bush wa Marekani, sasa ni zamu yake Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kukutana na kiongozi huyu wa Marekani. Badala ya kwenda mji mkuu Washington, Bi Merkel atamtembelea Bush kwenye shamba lake jimboni Texas.

https://p.dw.com/p/CH7A
Angela Merkel na George Bush wanasemekana wanaelewana vizuri
Angela Merkel na George Bush wanasemekana wanaelewana vizuriPicha: AP

Serikali ya Ujerumani na Marekani zinakubaliana kwamba lazima Iran izuiliwe kuweza kutengeneza silaha za kinyuklia. Lakini kuhusiana na mbinu bado hakuna maelewano.

Alipozungumza mbele ya mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa hapo Septemba, Kansela Merkel aliweka wazi msimamo wake: “Ujerumani pamoja na washirika wake inaunga mkono suluhu la kidiplomasia. Na iwapo Iran haitakubali, basi tutadai vikwazo viwe vikali zaidi.”

Wiki tatu baada ya hapo, serikali ya Ujerumani huko Berlin ilishtushwa na maneno yake rais Bush ambaye alisema: “Tumwona kiongozi wa Iran ambaye alitangaza anataka kuikandamiza Israel. Kwa hivyo niliwaambia viongozi wenzangu: Ikiwa mnataka kuzuia vita vikuu vya tatu vya dunia, mnapaswa kuwazuia Wairani kupata ujuzi wa utengenezaji wa silaha za kinyuklia.”

Kundi la wanasiasa wa Marekani wanaotaka hatua za kijeshi zichukuliwe dhidi ya Iran tayari limepata nguvu. Huenda basi, Angela Merkel atajaribu kumfahamisha rais Bush, hatua hiyo dhidi ya serikali ya Iran itakuwa na matokeo gani. Kabla ya kuondoka kwenda Marekani, Bi Merkel alisisitiza tena kutumika njia ya kidiplomasia kupita vikwazo. Bush lakini ataiuliza Ujerumani itafanyaje ikiwa China na Urusi hazitakubali kutumia njia hiyo ya kidiplomasia.

Afisa wa ngazi wa juu kwenye ikulu ya rais Bush alisema serikali ya Marekani haina madai yoyote kwa Ujerumani kupunguza zaidi biashara yake ya Iran. Marekani bado haijapata habari rasmi kwamba Ujerumani imekosoa vikwazo vilivyotolewa na Marekani dhidi ya benki na jeshi la Iran.

Suala hilo la Iran ndilo kama mtihani utakaoonyesha kwa kiasi gani Kansela Merkel anaweza kumshawishi rais Bush. Bila shaka, Kansela huyu alifuatilia kwa karibu ziara ya rais Sarkozy wa Ufaransa nchini Marekani wiki hii. Hata aliwahi kuhutubia bunge la Congress ambayo ni heshima kubwa kwa mgeni. Na rais Bush alimsifu sana Sakozy hapo alipomtaja kama mshirika ambaye yuko tayari kuchukua msimamo mkali ili kupata amani.

Suala lingine ambalo Bush na Marekani inawabidi walizungumzie ni lile la Kosovo. Hadi Disemba, Waserbia na Wakosovo wanatakiwa waafikiane juu ya hali ya kitaifa ya Kosovo. Ikiwa watashindwa kuna hatari ya kuwepo kwa mzozo mkali wakati wanajeshi na polisi wa Ujerumani bado wako Kosovo katika juhudi za kujenga upya eneo hili.

Afghanistan tena haitaleta utata kati ya Marekani na Ujerumani. Katika serikali ya Marekani inasemekana kwamba Bush hatadai Ujerumani ipeleke wanajeshi kwenye mapigano Kusini mwa Afghanistan.