1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ziarani Kenya

Halima Nyanza11 Julai 2011

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anawasili leo nchini Kenya kwa ziara rasmi ya siku moja. Kansela Merkel ambaye pia atazitembelea nchi nyingine barani Afrika, atakutana kwa mazungumzo na viongozi wa serikali.

https://p.dw.com/p/11std
Kansela Angela MerkelPicha: AP

Kwenye ziara hiyo itakayokuwa na shughuli nyingi, Kiongozi huyo wa Ujerumani hapo kesho amepangiwa kuwa na  mazungumzo na Rais Mwai Kibaki katika ikulu ya Nairobi mwendo wa saa tatu asubuhi na baadaye kukutana na waziri mkuu Raila Odinga saa nne unusu kabla kuwahutubia waandishi wa habari katika Hoteli ya Intercontinental hapa mjini Nairobi saa tano na dakika 40

Miongoni mwa maswala mbayo kiongozi huyo wa ujerumani anarajiwa kuyagusia ni amani katika eneo la Mashariki na Pembe ya Afrika hasa ukosefu wa usalama nchini Somalia.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi, Balozi wa Ujerumani nchini Kenya, Bi Margit Helwig-Boette amesema “Tuna lengo la pamoja la kupambana na uharamia ambapo Kenya ni mshirika muhimu katika lengo hili kwa hivyo ziara ya Kansela Merkel imejumuisha malengo ya kisiasa na kiuchumi yanayohusu eneo hili”.

Ziara ya Kansela Merkel inafanyika wakati ambapo Kenya iko katika harakati za kutekeleza mageuzi ya kisiasa na mfumo mpya wa uongozi ambapo Ujerumani imechangia kwa kiasi kikubwa mageuzi hayo ikiwemo katiba mpya.

Da lacht Kohls Mädchen wieder
Kansela Angela MerkelPicha: AP

Balozi wa ujerumani nchini Kenya Margit Helwig-Boette akifafanua juu ya ziara ya Merkel amesema, “Hii ni ziara ya kwanza ya Kansela Merkel nchini Kenya na nina hakika kwamba atatumia nafasi hii ya mazungumzo ya moja kwa moja kati yake na Waziri Mkuu na Rais kupata msimamo kamili wa serikali ya Kenya katika utekelezaji agenda ya mageuzi na hasa utekelezaji wa katiba”.

Balozi Margit amesisitiza wito uliotolewa hivi karibuni na Tume ya Umoja wa Ulaya kwamba viongozi wa Kenya wanapaswa kushirikiana kuhakikisha katiba mpya inatekelezwa ili kuandaa mazingira bora ya kisiasa kabla uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Ni kutokana na swala hilo ambapo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amepangiwa kufanya mashauri na spika wa bunge Keneth Merende hapo kesho.

Kibaki zur Verfassungsverkündung in Kenia
Rais wa Kenya Mwai Kibaki akila kiapo.Picha: AP

Ziara ya Kansela huyo wa Ujerumani nchini Kenya bila shaka itatoa fursa nzuri ya kuimarisha Biashara kati ya nchi hizo mbili.

Uhusiano wa Kenya na Ujerumani ulianza mwaka 1950 na tangu wakati huo hadi sasa Kenya imepokea msaada kutoka serikali ya Ujerumani wa jumla ya Euro Bilioni 1.4 . Mwaka uliopita pekee, serikali ya ujerumani iliipa Kenya msaada wa Euro milioni 140 fedha ambazo zilipangiwa kutumika katika sekta ya kilimo na Nishati.

Baada ya kukutana na viongozi wa serikali ya Kenya Kansela Angela Merkel atazuru Taasisi ya Kimataifa ya utafiti wa Mifugo iliyoko mjini Nairobi na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP kabla ya kuondoka kuelekea nchini Angola hapo kesho jioni.

Mwandishi: Alfred Kiti

Mhariri: Yusuf Saumu