1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ziarani Afghanistan

13 Mei 2013

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Ijumaa(10.05.2013)amefanya ziara ya ghafla kaskazini mwa Afghanistan kuvitembelea vikosi vya nchi yake siku sita baada ya kuuwawa kwa mwanajeshi wa kikosi maalum cha Ujerumani.

https://p.dw.com/p/18VHB
Merkel nchini Afghanistan
Merkel nchini AfghanistanPicha: picture-alliance/dpa

Kansela Merkel akiandamana na Waziri wake wa Ulinzi Thomas de Maiziere wamewasili Afghanistan asubuhi na kutembelea kambi za vikosi vya Ujerumani pamoja na kuzuru kumbukumbu ya wanajeshi 53 wa Ujerumani waliouwawa nchini humo.Walitembelea makao makuu ya vikosi vya Ujerumani yalioko katika mji wa kaskazini wa Mazar-e-Sharif kabla ya kusafiri kwa helikopta kuelekea kwenye kambi ya wanajeshi hao wa Ujerumani "Bundeswehr" ilioko Kunduz kilomita 150 mashariki ya makao makuu ya kikosi hicho ambapo walitowa heshima zao kwa wanajeshi waliouwawa.

Wakati wa ziara hiyo Merkel amesisitiza kwamba dunia haitoisahao Afghanistan kufuatia kuondoka kwa vikosi vya kimataifa nchini humo.Merkel amesema " Tutakuwa tuaangalia kuhakikisha kwamba mchakato wa kisiasa unaendelea kutekelezwa".Kansela ametaja kufanyika kwa uchaguzi nchini humo hapo mwaka 2014 na kukuza uchumi wa nchi hiyo ni mambo muhimu yanayoikabili nchi hiyo ambayo sio rahisi kutimilizwa na huchukuwa muda zaidi kuliko vile wangelitaka.Hata hivyo mafanikio ya mambo hayo amesema ni muhimu ili kwamba operesheni za kijeshi zisije kusitishwa.

Hapo tarehe 4 mwezi wa Mei waasi waliokuwa wakivurumisha maroketi wamemuuwa mwanajeshi mmoja wa Ujerumani na kumjeruhi mwengine katika jimbo la kaskazini la Baghlan. Hiyo ni mara ya kwanza kutokea kwa kifo cha mwanajeshi wa kikosi maalum cha Ujerumani kilioko Afghanistan.Kikosi hicho kinahesabiwa kuwa na ujuzi mkubwa ni kama kile cha Marekani kinachojulikana kwa jina la Navy SEAL ambapo wakati huo kilikuwa kikiongoza operesheni za kijeshi nchini Afghanistan.

Heshima kwa wanajeshi waliouwawa

Katika kambi ya kijeshi Kunduz ya Kaskazini,Merkel na de Maiziere wameweka shada la mauwa katika ukuta wa kumbukumbu ambao una majina ya wanajeshi wa Ujerumani waliouwawa nchiní Afghanistan tokea mwaka 2002.Shada kwa heshima ya mwanajeshi aliyeuwawa hivi karibuni jina lake lilikuwa linasomeka tu "Kikosi cha Kazi 47,Vikosi Maalum",kwa sababu wanajeshi wa vikosi hivyo majina yao yanakuwa hayatajwi hata wakati wa kifo.Kuhusiana na kifo cha mwanajeshi huyo Marekel amesema ni vigumu kupokea habari za vifo vya aina hiyo na kwamba kila mwanajeshi anayeuwawa kwao wao ni pigo.

Kansela Angela Merkel na Waziri wake wa Ulinzi Thomas de Maiziere wakitembelea vikosi vya Ujerumani vilioko Kundus. (10.05.2012)
Kansela Angela Merkel na Waziri wake wa Ulinzi Thomas de Maiziere wakitembelea vikosi vya Ujerumani vilioko Kundus. (10.05.2012)Picha: picture-alliance/dpa

Ikiwa na zaidi ya wanajeshi 4,000 waliowekwa nchini Afghanistan Ujerumani ni nchi ya tatu yenye wanajeshi wengi katika kikosi cha kimataifa kilioko Afghanistan na imeahidi kubakisha wanajeshi 800 nchini humo baada ya operesheni ya mapambano ya NATO kumalizika mwishoni mwa mwaka 2014.

Marekani inatarajiwa kubakisha wanajeshi 10,000 nchini Afghanistan baada ya mwaka 2014 lakini bado haukufikiwa uamuzi rasmi juu ya suala hilo.

Vikosi vya Ujerumani vitaendelea kubakia hadi hapo mwaka 2017 kwa ajili ya kutowa mafunzo,ushauri na msaada kwa vikosi vya usalama vya Afghanistan na vitawekwa katika mji mkuu wa Kabul na Mazar-e-Sharif. Baada ya mwaka 2017 Ujerumani imesema itakuwa tayari kuchangia wanajeshi 200 hadi 300.

Sharti la kubakisha vikosi

Uamuzi wa mwisho kuhusu vikosi vya Ujerumani vitakavowekwa nchini Afghanistan baada ya mwaka 2014 utatolewa na serikali mpya baada ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika hapo mwezi wa Septemba ambapo kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni Merkel anatarajiwa kushinda muhula wa tatu wa kipindi cha miaka mingine minne madarakani. Wakati mpango huo wa kuwekwa kwa vikosi vya Ujerumani nchini Afghanistan kwa kiasi kikubwa haungwi mkono na wananchi, unaungwa mkono na vyama vikuu vya kisiasa.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan.
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan.Picha: REUTERS

Suala la Ujerumani kuendelea kuweka vikosi vyake nchini Afghanistan pia linahitaji ombi la serikali ya nchi hiyo.Katika hafla iliofanyika katika mji mkuu wa Kabul hapo Alhamisi,Rais Hamid Karzai amesema alikuwa anataka kila nchi mwanachama wa nchi 28 za Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuzungumza moja kwa moja na serikali yake juu ya idadi ya wanajeshi inaotaka kuwaweka nchini humo,mahala pa kuwaweka na vipi vikosi hivyo vitakvyoweza kuinufaisha nchi hiyo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri :  Mohammed Abdul-Rahman