1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: 'Urusi bado mshirika muhimu'

Mohammed Khelef6 Juni 2015

Matarajio ni makubwa kuelekea mkutano wa kilele wa G7 nchini Ujerumani na Kansela Angela Merkel amezungumza na DW juu ya anachotegemea kitafikiwa akisisitiza dhima Urusi hasa kwenye suala la Syria.

https://p.dw.com/p/1FcVf
Kansela Angela Merkel (kushoto) akiwa kwenye mahojiano maalum na Mhariri wa DW, Dagmar Engel.
Kansela Angela Merkel (kushoto) akiwa kwenye mahojiano maalum na Mhariri wa DW, Dagmar Engel.Picha: DW/C. Strack

DW: Kansela, dunia itakuwa inaingalia Ujerumani kwa karibu ndani ya siku chache zijazo. Watu wana matumaini makubwa na mkutano huo wa kilele wa G7. Ajenda inaoekana kama ni "kuiokoa dunia ndani ya masaa 24." Kuna hatua gani madhubuti za kufikia mafanikio hayo ambazo ni mkutano wa G7 pekee ndio unaoweza kuzichukuwa?

Angela Merkel: Kwangu, kwanza jambo muhimu kabisa ni kuwa wakuu wa mataifa haya saba wanazungumzia masuala makubwa. Mbadilishano huu wa mawazo ni muhimu sana sana kabisa ili kuweza kujuwa namna mawazo juu ya masuala ya msingi yalivyo kwa mwaka mzima - wapi pana tafauti, wapi pana mfanano. Lakini pia inawezekana kusema, kwa uhakika kabisa, kwamba ningelipenda kupata majibu ya uhakika zaidi kwenye suala hili: "Vipi tutayashughulikia majanga huko twendako?" na yumkini tukapata njia ya kuchukuwa hatua bora zaidi huko mbele. Wakati Ebola iliporipuka, jumuiya ya kimataifa haikuchukuwa hatua muafaka: zilizochukuliwa zilichelewa sana na bila ya kuwa na uratibu wa kutosha. Hili halipaswi kutokea tena. Na nadhani kuwepo kwa viongozi wakuu wa Afrika, kama vile rais wa Liberia, kutatukumbusha tena umuhimu wa suala hili la kiafya. Vile vile, afya itaangaliwa kwenye mambo mengine, kwa mfano uwezo wa kukabiliana na madawa ya maradhi thakili, ambao tutakuwa na mipango ya kitaifa na kushirikiana na Shirika la Afya Duniani. Ninategemea hatua fulani kupigwa hapa, hata kama hakuna tatizo linaloweza kutatuliwa kwa masaa 24, jambo ambalo lenyewe ni tatizo kubwa.

Je, bado G7 inakwenda na wakati? Si kweli tena kwamba kundi hili linawakilisha mataifa yenye nguvu kubwa kabisa kiuchumi duniani, ikiwa utazichukuwa Italia, Ufaransa na Canada.

Yote ni mataifa ya kidemokrasia yenye maadili mamoja na bado ni mataifa yaliyo muhimu sana kiuchumi. Lakini tunahitaji muundo wa G20 kama kisaidizi. Kundi hili linajumuisha nchi zenye mifumo tafauti ya kijamii, lakini mataifa makubwa kabisa kiuchumi yanakusanywa pale. Hata hivyo, G7 inatoa nafasi kubwa na huru zaidi ya majadiliano kutokana kwa kiasi fulani kuwa haya ni mataifa ya kidemokrasia.

Kansela Angela Merkel akizungumza na vyombo vya habari.
Kansela Angela Merkel akizungumza na vyombo vya habari.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Ikiwa umuhimu mkubwa sana unawekwa kwenye maadili ya pamoja, je si mjadala mzima juu ya ama Urusi ishiriki ama la utakuwa hauna maana? Hata ukiondoa mzozo wa Ukraine, hivi unadhani kuwa Urusi ina maadili mamoja na waliobakia?

Ni kweli kwamba Urusi haijapiga hatua sana kwenye miaka ya hivi karibuni kuelekea utekelezaji wa mawazo mengi ambayo sote tunayo kwenye G7. Wakati Urusi ilipokubaliwa kuingia kwenye kundi hili, ilikuwa inadhaniwa labda kulikuwa na mambo zaidi ya pamoja - hasa kwenye masuala ya ulinzi, kwa mfano suala la ushirikiano wa NATO na Urusi. Hata hivyo, Urusi bado ni mshirika muhimu kwenye majadiliano mengine. Tuna mfumo wa Nomandy katika kuutatua mzozo wa Ukraine, tuna mazungumzo ya mataifa 6 juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, na Urusi itashirikishwa na lazima ishirikishwe kwenye juhudi za kuutatua mzozo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria. Labda nikukumbushe tu kwamba ilikuwa ni kwa msaada wa Urusi tu ndipo silaha za kemikali ziliweza kuondolewa Syria. Kwa hivyo, tutajadiliana pia namna ambavyo Urusi inaweza kushirikishwa.

G7 ilianza kama mkutano wa kilele wa kilimwengu juu ya uchumi. Sasa masuala ya kiuchumi yako tena mstari wa mbele: biashara huria, ukuwaji na juu ya yote namna ya kuufanya ukuwaji uwe endelevu, lakini mzozo wa Ugiriki unaweka kiwingu juu ya yote haya. Je, Ugiriki inayapiku matatizo mengine makubwa makubwa ya kiuchumi?

Hapana, sifikirii hivyo. Hapana shaka, tutakuwa tunazungumzia hali kwenye eneo la sarafu ya euro kwa kuhusisha na hali ya uchumi wa dunia. Na bila ya shaka kutakuwa na majadiliano juu ya matatizo gani tumeyatatua. Tutaweza kuonesha kwamba sasa Ireland, ambayo pia ilikuwa na mpango wa uokozi, ni nchi yenye ukuwaji mkubwa wa uchumi, na kwamba uchumi unakuwa pia nchini Ureno na Uhispania. Na vile vile tutazungumzia Ugiriki, lakini hilo halitakuwa kabisa suala kuu kwa sasa; tutatoa tu ripoti juu ya wapi mambo yalipo na kuelezea matarajio yetrz kwamba mazungumzo yanaweza kumalizika kwa mafanikio.

Mara ya mwisho kulipofanyika mkutano kama huu nchini Ujerumani, ni miaka minane iliyopita wakati huo kundi hili likiitwa G8. Sasa kumekuwa na mzozo wa euro. Mkutano huo wa mwisho wa kilele nchini Ujerumani ulikuwa kabla ya Mapinduzi ya Umma kwenye Nchi za Kiarabu, kabla ya vita vya Syria, kabla ya mzozo wa Ukraibe. Ukiuangalia mkutano huu wa kilele sasa, vipi jukumu lako limebadilika, na vipi jukumu la Ujerumani limebadilika kwenye dunia hii inayobadilika kwa kasi ya ajabu?

Lazima isemwe kwamba hapo katikati kulikuwa na mzozo mkubwa wa kimataifa wa kifedha na kiuchumi ambao kwa hakika umebadilisha mambo mengi. Hali ya kiuchumi duniani hivi leo inaelezeka kupitia sera ya kupunguza riba hadi kiwango cha chini kabisa. Sera hii imeinua ukuwaji wa uchumi kufikia kiwango fulani, lakini tutakabiliwa pia na suala la vipi tunaweza kurejea kwenye hali ya kawaida. Tuna utaratibu mzuri wa uendeshaji benki. Na ukiulizia jukumu la Ujerumani, basi ninaweza kukumbuka kwamba hata Heiligendamm tulikuwa na masuala kama vile mabadiliko ya tabia nchi, ambayo hadi leo tunayashughulikia. Na kuna kiwango fulani cha muendelezo kenye masuala ambayo tunayashughulikia kwenye mikutano ya kilele ya G7, au hiyo iliyokuwa G8. Suala la ulinzi wa mazingira daima limekuwa muhimu kwa Ujerumani, na bado ni muhimu tukilihusisha na kongamano la Paris mwezi Disemba. Na masuala mapya pia yamezuka. Suala la afya halikuwa na nafasi kubwa hapo mwanzoni. Hivyo, nimefurahi kwamba Ujerumani itakuwa tena mwenyeji, lakini bado tuko pamoja kama jamii na pia sote tuna masuala maalum ambayo tunataka kuyaangazia.

Ahsante sana Kansela kwa mahojiano haya.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW
Mhariri: Abdu Mtullya