1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel : "Ndoto iliokuwa kweli " - Miaka 25 Kuanguka Ukuta wa Berlin

9 Novemba 2014

Kansela Angela Merkel Jumapili (09.11.2014) ameongoza sherehe za kuadhimisha miaka 25 ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin na kuuita huo kuwa mfano wa shauku ya binaadamu kwa uhuru.

https://p.dw.com/p/1Djfl
Kansela Angela Merkel akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya kuadhimisha miaka 25 ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin katika Kituo cha Kumbukumbu cha Bernauer Strasse. (09.11.2014)
Kansela Angela Merkel akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya kuadhimisha miaka 25 ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin katika Kituo cha Kumbukumbu cha Bernauer Strasse. (09.11.2014)Picha: Reuters/F. Bensch

Usiku wa Novemba 9 mwaka 1989 maelfu ya wananchi wa Berlin ya Mashariki walimiminika kwenye vituo vya mpakani ambavyo huko nyuma vilikuwa vimefungwa baada ya utawala wa kikomunisti kusalimu amri kutokana na shinikizo kubwa la umma na kukubali kuregeza vikwazo vya safari ambavyo vilikuwa vimewazuwiya raia wao kwenda Ujerumani magharibi kwa miongo kwa kadhaa.

"Kuanguka kwa Ukuta kumetuonyesha kwamba ndoto zinaweza kuwa za kweli". Merkel ametamka hayo katika eneo kuu la kumbukumbu ya Ukuta huo katika mtaa wa Bernauer Strasse mjini Berlin.

Kuanguka kwa Ukuta huo ilikuwa ni kilele cha wiki kadhaa za maandamano ya umma yaliyokuwa yamechochewa na mabadiliko ambayo yalikuwa tayari yametokea katika nchi nyengine za Ulaya mashariki.

Merkel ametaja mifano muhimu iliowekwa na makundi ya vuguvugu ya demokrasia nchini Poland,Czechchoslovakia na Hungary na kuwapongeza wananchi wa Ujerumani mashariki walioshajiishwa nao ambao walisimama kupambana na udikteta.

Heshima kwa wahanga

Pia ametowa heshima zake kwa wale walioteseka chini ya utawala wa kikomunisti wa Ujerumani mashariki wakiwemo watu 138 waliokufa kwenye Ukuta huo.

Kansela Angela Merkel akiweka uwa la waridi kwenye Ukuta. (09.11.2014)
Kansela Angela Merkel akiweka uwa la waridi kwenye Ukuta. (09.11.2014)Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Merkel anaona kuanguka kwa ukuta huo kuwa ishara ya matumaini kwa maeneo yenye mizozo na mfarakano duniani . Amesema ujumbe huo hususan umeelekezwa kwa watu wa Ukraine nchini Syria na Iraq na katika maeneo mengine mengi duniani ambapo uhuru na haki za binaadamu viko hatarini au hata kukandamizwa.

Maadhimisho hayo yalianza kwa maombolezo ya misa ya kanisani na ibada kuwaombea takriban wahanga 389 wa mpakani ambao aidha waliuwawa kwa kupigwa risasi, kuripuliwa na mabomu yaliotegwa ardhini au kuuwawa wakati wakijaribu kutoroka Ujerumani mashariki.

Kansela Angela Merkel mwenye umri wa miaka 60 ambaye alikulia chini wa utawala wa kikomunisti akiwa mtoto wa mchungaji aliungana na wageni wengine wa heshima katika kituo cha kumbukumbu cha mtaa wa Bernauer Strasse ambao umeshuhudia watu wakiruka kutoka kwenye madirisha ya nyumba wakati Ukuta huo uliposimamishwa kwa mara ya kwanza hapo mwaka 1961.

Mchango wa Gorbachev

Wageni wa heshima pekee wa kigeni ambao walikuwa wakongwe wa enzi hiyo ni pamoja na kiongozi wa mwisho wa muungano wa Kisovieti Mikhail Gorbachev mwenye umri wa miaka 83 ambaye sera zake za mageuzi za "glasnost" na "perestroika" zilichochea mfululizo wa matukio ya kihistoria.

Mikhail Gorbachev kiongozi wa zamani wa Muungano wa Kisovieti.
Mikhail Gorbachev kiongozi wa zamani wa Muungano wa Kisovieti.Picha: AP

Gorbachev ambaye ni mtu mashuhuri kabisa nchini Ujerumani ameonya hapo jana kwamba dunia iko kwenye ukingo wa Vita Baridi vipya kutokana na mvutano wa mataifa ya mshariki na magharibi juu ya suala la Ukraine.

Ujerumani mashariki iliujenga Ukuta huo hapo mwaka 1961 na kuelezewa kwamba utakuwa wa muda lakini ulikuja kubakia kwa miaka 28.Umekuja kuanguka baada ya Gorbachev kiongozi wa Muungano wa Kisovieti kuregeza hatamu zake kwa majimbo ya zamani yaliokuwa vibaraka wa muungano huo na wakati makundi ya vuguvugu la kudai demokrasia yakizidi ujasiri na kuongezeka kiidadi Ulaya mashariki.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP/dpa

Mhariri:Hamidou Oummilkheir