1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Papandreou kukutana baadae leo

Abdu Said Mtullya5 Machi 2010

Ujerumani imesema mazungumzo ya leo jioni baina ya Kansela Merkel na Waziri Mkuu wa Ugiriki hayatahusu msaada wa fedha kwa Ugiriki.

https://p.dw.com/p/MLWV
Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou.Picha: AP

Waziri Mkuu wa Ugiriki, Georgios Papandreou, jioni hii anakutana na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, ili kufafanua mpango wa kubana matumizi uliopitishwa na nchi yake katika juhudi za kukabiliana na mgogoro wa bajeti.

Waziri mkuu wa Ugiriki amewasili Ujerumani wakati ambapo serikali ya Angela Merkel imesisitiza kwamba haitatoa Euro hata moja kuisaidia Ugiriki.

Hatahivyo, Kansela Merkel,ameipongeza serikali ya Ugiriki kwa kuupitisha mpango wa kubana matumizi katika juhudi za kukabiliana na matatizo ya bajeti ya nchi hiyo. Kansela Merkel amesema kwa kupitisha mpango huo, Ugiriki imechimba shimo kwa sururu.

Akizungumza kwenye mkutano na wawakilishi wa jumuiya za kiuchumi mjini Munich leo, Bibi Merkel alisema kuwa Ugiriki sasa imo katika njia nzuri.

Hatahivyo,kabla ya mkutano wake na waziri mkuu wa Ugiriki,imeelezwa wazi kuwa mazungumzo ya viongozi hao leo jioni hayatahusu msaada wa fedha, bali zaidi ni juu ya Ujerumani kuiunga mkono Ugiriki, kisiasa.Hapo awali waziri mkuu wa Ugiriki ,Papandreou, mwenyewe aliliambia gazeti la Ujerumani, Frankfurter Allgemeine Zeitung kwamba nchi yake inahitaji kuungwa mkono na Umoja wa Ulaya na washirika wake wengine wa bara hilo. Hata hivyo waziri mkuu Papandreou amesisitiza kwamba bila ya nchi yake kuungwa mkono kisiasa mgogoro unaoikabili unaweza kuwa wa gharama kubwa kwa bara zima la Ulaya.

Lakini amesema nchi yake lazima ipatiwe mkopo japo siyo kwa masharti nafuu kama yale yanayotolewa kwa Ujerumani. Amesema nchi yake inapaswa kupewa masharti nafuu zaidi kuliko ya wakati huu. Ameeleza kwamba ili kupatiwa Euro bilioni tano,Ugiriki inatakiwa ilipe Euro milioni 750 zaidi kuliko Ujerumani. Papandreou amesema hakuna nchi yoyote ya Ulaya inayoweza kubeba mzigo kama huo.Lakini msemaji wa serikali ya Ujerumani,Ulrich Wilhelm, amesisitiza kuwa Ujerumani itafanya kila linalowezekana, ili kuiunga mkono Ugiriki kisiasa.

Mwandishi/Mtullya Abdu/afp/dpa/ZA

Mhariri: Othman, Miraji

Hatahivyo