1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kukutana na Cameron jijini London

Josephat Nyiro Charo7 Januari 2015

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel leo (07.01.2015) anafanya zaira yake ya kwanza ya kigeni mwaka huu. Atazungumza na Cameron kuhusu mipango ya kuratibu upya uhusiano wa Uingereza na Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/1EFwn
Angela Merkel und David Cameron in London
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kushoto) na waziri mkuu wa Uingereza, David CameronPicha: Reuters

Ziara ya Merkel jijini London ni sehemu ya msururu wa ziara atakazozifanya katika miji mikuu ya mataifa ya kigeni kuandaa mkutano wa kundi la nchi zilizostawi kiviwanda za G7 uliopangwa kufanyika Ujerumani katika kasri la Elmau jimboni Bavaria kati ya Juni 7 na 8 mwaka huu. Katika kikao chao cha faragha Merkel anataka kuzungumza na Cameron kuhusu mzozo wa Ukraine, uhusiano na Urusi na hali ngumu ya kiuchumi inayoukabili ulimwengu.

Viongozi hao watazungumzia pia masuala ya ushirikiano kati ya Ujerumani na Uingereza na sera ya Ulaya ambayo imeuweka uhusiano kati yao kwenye mtihani katika miezi ya hivi karibuni. Masuala hayo yanajumuisha azma ya Cameron kupunguza wimbi la wahamiaji kutoka mataifa ya Umoja wa Ulaya wanaoingia Uingereza, kuwa chini ya 100,000 kwa mwaka, suala ambalo alikiri mwezi Novemba mwaka uliopita litahitaji mageuzi ya mikataba ya Umoja wa Ulaya.

Kansela Merkel amesema atapinga changamoto yoyote kwa kanuni ya uhuru wa kutembea kwa nguvu kazi ndani ya Umoja wa Ulaya na anapinga hatua ya kuifanyia mageuzi mikataba, ambayo huenda itahitaji kura za maoni katika mataifa kadhaa wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Jean Claude Junker Premierminister Luxemburg
Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jean Claude JunkerPicha: picture-alliance/ dpa

Cameron anaonekana ametengwa katika vita vyake huku rais wa halmashauri kuu ya Umoja huo Jean Claude Junker akimuonya mwezi Desemba mwaka uliopita dhidi ya kuwashambulia raia wa nchi masikini za Ulaya mashariki wanaofanya kazi kihalali nchini Uingereza.

Huku Merkel akiunga mkono harakati za kuzuia utumiaji vibaya wa fedha za jamii na wahamiaji, mmoja wa washirika wake amesema wazi hatokubali kubadili msimamo wake kuhusiana na haki ya wafanyakazi wa Umoja wa Ulaya kutafuta ajira popote wanapotaka katika umoja huo wenye nchi 28 wanachama. "Wakati Merkel alipozuru London mwaka jana kulikuwa na matarajio angetimiza masharti ya waziri mkuu wa Uingereza kuhusu mageuzi ya mkataba wa Umoja wa Ulaya. Hakufanya hivyo wakati huo na bila shaka hatafanya hivyo wakati huu," alisema Gunther Krichbaum, mkuu wa kamati inayoshughulikia masuala ya Ulaya katika bunge la Ujerumani, Bundestag.

Merkel azuru Uingereza uchaguzi ukikaribia

Ziara ya Merkel inafanyika miezi minne kabla uchaguzi mkuu wa Uingereza mwezi Mei. Kama Cameron atabaki kuwa waziri mkuu baada ya uchaguzi huo, kiongozi huyo anapania kujaribu kuratibu upya uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya na baadaye atafute ridhaa ya raia kupitia kura ya maoni mwishoni mwa mwaka 2017.

Huku Cameron akitaka Uingereza ibakie katika Umoja wa Ulaya ameshasema kama hatopata kinachohitajika, hafutilii mbali chochote. Akizungumza na gazeti la The Mail toleo la Jumapili Cameron alisema maeneo muhimu ni kulinda soko moja, kuondokana na umoja wenye ushirikiano wa karibu, kuweza kuzuia sheria kupitia kura ya veto na sera muhimu kuhusu jamii.

Nigel Farage UKIP Parteichef
Kiongozi wa chama cha UKIP, Nigel FaragePicha: Getty Images

Chama cha kihafidhina cha Cameron kinatarajiwa kupoteza kura kwa chama kinachoupinga Umoja wa Ulaya na uhamiaji cha United Kingdom Party, UKIP, kilichoongoza uchaguzi wa Ulaya mnamo mwezi Mei mwaka jana. Kiongozi wa UKIP Nigel Farage alisema hakuna uwezekano wa Merkel kumsaidia Cameron kupata anachokitaka. "Ujerumani inakabiliwa na matatizo yake wakati huu na haitotaka Uingereza kuwafukuza raia wa Umoja wa Ulaya wanaotafuta ajira, na pengine kuwaelekeza watafute kazi kwingineko," alisema Farage.

Cameron na Merkel wanatarajiwa kuyatembelea maonyesho yaliyopewa jina "Ujerumani:Kumbukumbu za Taifa" katika jumba la makumbusho la Uingereza, yaliyoandaliwa kuielezea historia ya Ujerumani ya miaka 600 iliyopita.

Kabla ya ziara ya leo Merkel na Cameron walitoa taarifa ya pamoja wakisema hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa kuufanya Umoja wa Ulaya kuwa imara zaidi na wenye ushidani. Viongozi hao wana matumaini ya kufikia mkataba wa biashara huru kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani mwaka huu.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/REUTERS

Mhariri:Hamidou Oummilkheir