1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel: EU haipaswi kuwa Umoja wa madeni

John Juma
3 Juni 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amempongeza waziri mkuu mpya wa Italia Giuseppe Conte. Hata hivyo ameonekana kupuuza wito ya Italia kutaka Umoja wa Ulaya kuisamehe madeni yake

https://p.dw.com/p/2yrRA
Deutschland Bundestag Angela Merkel
Picha: Reuters/H. Hanschke

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alifanya mazungumzo na waziri mkuu mpya wa Italia Giuseppe Conte jana Jumamosi na kumkaribisha mjini Berlin kwa mazungumzo zaidi kuhusu mustakabali wa uhusiano wa nchi zao.

Kwenye tarifa, ofisi ya kansela imesema Merkel alimpongeza Conte kwa kuwa waziri mkuu. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Merkel na Conte walizungumza kwa njia ya simu, walitilia msisitizo umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa pande zote mbili.

Conte ambaye ni profesa wa shera asiyejulikana sana, amekuwa kimya tangu alipoapishwa Ijumaa. Lakini alitangaza kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa, kando na Merkel pia alizungumza na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron siku ya Jumamosi.

Amesema atakutana na viongozi hao wiki ijayo katika mkutano wa kilele wa G7 utakaofanyika Canada, ambapo pia atazungumzia masilahi ya raia wa Italia.

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte
Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe ContePicha: picture-alliance/AP Photo/E. Ferrari

Bibi Merkel amesalia miongoni mwa sauti za chini kuhusu serikali mpya ya mseto nchini Italia yenye vyama viwili visivyopendelea Umoja wa Ulaya, vuguvugu la Nyota-5 na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia League.

Vyama hivyo vilifanya kampeni ambazo zilijawa ukosoaji mkubwa kwa Umoja wa Ulaya na kanda ya yuro.  Kinachosubiriwa ni kuona jinsi ambavyo vyama hivi ambavyo sasa viko madarakani vitaendeleza vita vyao Brussels na Frankfurt.

Katika toleo la hivi karibuni la jarida la Der Spiegel lililochapishwa Ijumaa, kwenye ukurasa wake wa mbele, jarida hilo lilikuwa na mchoro wa uma uliojaa spaghetti huku imefungiwa kamba ya kujitia kitanzi. Kichwa cha jarida kiliandikwa "Italia yajiangamiza yenyewe- na inavuta Umoja wa Ulaya  pia.

Merkel kuhusu miito ya kusamehea Italia madeni

Je Italia yajiangamiza?
Je Italia yajiangamiza?Picha: Der Spiegel

Punde baada ya kuzungumza na Conte, ripoti ziliibuka kuwa Merkel anaonekana kuondoa uwezekano wowote wa Umoja wa Ulaya kuiondolea Italia madeni.

Katika gazeti la Jumapili Frankfurter Allgermeine, Merkel amesema ushirikiano wa Umoja wa Ulaya haupaswi kuugeuza umoja huo kuwa wa kugawana madeni bali unapaswa kusaidia wanachama ili wajisaidie wenyewe.

Merkel alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa na jarida hillo alipoulizwa kuhusu ripoti katika shirika moja la habari kuwa vuguvugu la nyota tano linalopinga utawala nchini Italia pamoja na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia League nchini Italia, zilipanga kuomba benki kuu ya Umoja wa Ulaya kuisamehe Italia deni lake la euro bilioni 250.

Benki kuu ya Umoja wa Ulaya ilitoa taarifa ikisema makubaliano ya Ulaya hayataweza kuruhusu hatua kama hiyo kufanyika.

Serikali ya muungano nchini Italia yenye vyama viwili visivyopendelea Umoja wa Ulaya, ilichukua usukani Ijumaa na kuepusha kura ya mapema nchini humo.

Mwandishi: John Juma/DW

Mhariri: Sekione Kitojo