1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel awahutubia waandishi habari kwenye mkutano wa mwaka

Zainab Aziz
29 Agosti 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amezungumzia mambo kadhaa yakiwemo kuendeleza vizuizi katika mipaka ya nchi zote zilizo katika umoja wa Schengen na pia ameunga mkono kuanzishwa kwa shirika la fedha la Ulaya. 

https://p.dw.com/p/2j2bz
Deutschland PK Merkel
Picha: picture-alliance/AA/M. Gambarini

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alieleza kwa ujasiri katika hotuba yake ya kipindi hiki cha joto na katika hotuba yake bibi Merkel alielezea changamoto ambazo zinaikabili Ujerumani huku zikiwa zimebakia chini ya wiki nne kabla ya kufanyika uchaguzi wa tarehe 24 mwezi Septemba ambapo ushindi wa chama chake cha kihafidhina unaonekana mapema.

 Kuhusu suala la kudhibiti mipaka nchi za Ujerumani, Denmark, Austria, Sweden na Norway ambayo sio mwanachma wa Umoja wa Ulaya zilianzisha udhibiti huo katika mipaka yake mnamo mwaka 2015 kwa ajili ya kuzuia wimbi la wakimbizi.

 

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano huo unaofanyika kila mwaka, kansela wa Ujerumani Angela Merkel aligusia juu ya mgogoro wa wakimbizi na pia juu ya uhusiano ulioharibika kati ya Ujerumani na Uturuki.  Mbali na hayo Bi Merkel pia alizungumzia sera ya fedha ya wanachama wa nchi za Umoja wa Ulaya lakini pia hakutaka kuyajibu maswali kuhusu lini anatarajiwa kuacha shughuli za kisiasa na jinsi mchakato wa kampeni zake ulivyopooza.

Deutschland PK Merkel
Kansela Angela Merkel katika mkutano na waandishi wa habari.Picha: Reuters/F. Bensch

Baada ya miaka mingi ambayo imeliwezesha bara la Ulaya kupata ujuzi swali linalojitokeza ni jinsi gani watu wa bara hilo watakavyoweza kuonyesha kwamba wanaamini kuwa wanaweza kukabiliana na nyakati ngumu katika eneo lao. Merkel alisema hapo ndipo anapoamini kuwa wazo la waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble la kuitumia hali ya utulivu wa Ulaya na kuigeuza na kuwa shirika la kifedha ni wazo zuri kabisa ambalo litawezesha nchi za Ulaya kuendelea kuwa na utulivu na hivyo kuuonyesha ulimwengu kwamba wana miundombinu yote mikononi mwao ya kuweza kushughulikia hali yoyote.

Merkel amesema anaunga mkono pendekezo la Mfuko wa kudumu wa kufadhili uchumi wa nchi za Ulaya na mabenki. Amesema mfuko huo unaweza ukageuka kuwa shirika la fedha la Ulaya ambalo litajitegemea na kuwa huru kutoka kwenye Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). Kansela Merkel pia aliitetea hatua yake ya miaka miwili iliyopita ya kuwaruhusu maalfu ya wakimbizi kuingia nchini Ujerumani, akisema kuwa hatua hiyo ilikuwa ya kibinadamu na wala sio hatua ambayo serikali yake inapanga kuendelea nayo kwa muda mrefu.

Vile vile kansela Angela Merkel alizungumzia juu ya uhusiano wa Ujerumani na Uturuki ambapo alisema uhusiano wa nchi hizi mbili uko katika hali ya kutatanisha lakini yeye binafsi angependa kuona mahusiano mazuri baina ya nchi hizi ingawa yote haya yatawezekana tu iwapo sheria itapewa kipaumbele. Merkel alisema hakuna maendeleo katika mahusiano ya kibiashara baina ya Ujerumani na Uturuki.

Mwandishi: Zainab Aziz/ AFPE/DPAE

Mhariri:Josephat Charo