1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel atathmini uwenyekiti wake wa Umoja wa Ulaya

Bernd Riegert / Maja Dreyer28 Juni 2007

Kirasmi, bado zimesalia siku mbili hadi Ujerumani itakamilisha muda wake wa kuuongoza Umoja wa Ulaya. Tayari jana, Kansel Angela Merkel wa Ujerumani ameyatathmini mafanikio ya uwenyekiti wake mbele ya bunge la Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/CHBw
Kansela Merkel katika bunge la Umoja wa Ulaya
Kansela Merkel katika bunge la Umoja wa UlayaPicha: AP

Kama ilivyotarajiwa, Kansela Merkel alipiga debe juu ya uwenyekiti wake wa Umoja wa Ulaya. Kilele cha kipindi hiki cha miezi sita iliyopita kilikuwa kupata makubaliano juu ya mkataba mpya kwa Umoja huu mwishoni mwa juma lililopita. Katika hotuba yake, Bi Merkel alisema: “Tumeelekea njia ya kupata msingi mpya wa pamoja kwa Umoja wa Ulaya. Tumeweza kuendelea. Hatimaye tumeuhifadhi uaminifu katika Umoja huu. Tumezuia mgawanyiko.”

Dhidi ya upinzani mkali kutoka Poland na pia Uingereza, nchi 27 wanachama wa Umoja huu zilikubaliana juu ya mkataba badala ya katiba ambayo ilikataliwa na nchi kadhaa. Angela Merkel aliionya Poland kutouharibu uaminifu wa Umoja wa Ulaya ambao umechukua muda mrefu kujengwa. Baada ya tishio lake la kupitisha mkataba huu bila ya kuzingatia Poland, waziri mkuu wa Poland, Jaroslaw Kaczynksi ameyakubali masharti yaliyowekwa.

Katika hotuba yake ya jana, Merkel alisema, hii ilikuwa kazi ngumu sana na kutoa mwito kwamba lazima nchi zote zifanya bidii kushirikiana na kueneza Umoja huu. Inabidi kuzuia mgawanyiko katika sehemu mbili ya Umoja wa Ulaya, moja ikiendelea haraka kuliko nyingine: “Inapaswa kujitahidi na kujitolea kwa kazi hii ngumu kuziunganisha nchi zote wanachama zichukue njia ya pamoja. Kuna methali moja kutoka Afrika inayosema: Ukitaka kwenda haraka, nenda peke yako basi. Ukitaka kufika mbali, uende pmaoja na watu wengine.”

Angela Merkel amepigiwa makofi kwa muda mrefu na wabunge wa Ulaya. Hata hivyo, nusu tu ya wabunge walikuweko kumsikiliza.

Kansela huyu pia alisisitiza mafanikio ya Umoja wa Ulaya kukubali juu ya sera za pamoja za nishati na hali ya hewa mwezi wa Machi. Ni muhimu sana kuwa na Umoja wa Ulaya wenye msimamo wa pamoja kuhusu sera za kulinda hali ya hewa, Merkel alisema.

Mbunge wa chama cha Kiliberali katika bunge la Umoja wa Ulaya, Bi Silvana Koch-Mehrin, aliukosoa mkataba mpya wa kutokuwa na masharti ya muhimu, lakini alimsifu Kansela Merkel kwa njia yake ya kupatanisha. Amesema: “Haogopi kusimamisha mjadala na kusema: Hapana, hatuwezi kuendelea hivyo. Basi tutaendelea bila nyinyi, yaani serikali ya Poland, ikiwa mnakataa kukubali angalau kidogo.”

Mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, José Barroso, pia alimsifu Kansela wa Ujerumani akikumbusha pia kuwa wakaazi wa Ulaya watanufaika kutokana na sheria mpya kuhusu mazungumzo ya simu za mikononi kwenye nchi za kigeni. Kuanzia kesho, bei ya za mazungumzo haya itakuwa rahisi zaidi.