1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel apania kuing'oa AfD bungeni

Sekione Kitojo
15 Machi 2018

Chama cha  siasa kali  za  mrengo  wa  kulia  cha Chaguo Mbadala kwa Ujerumani - AfD kimekuwa  mkosoaji mkubwa  wa  kansela  Angela  Merkel  na  mara  kadhaa kimetoa  mwito  wa  kutaka  aondolewe kutoka  madarakani.

https://p.dw.com/p/2uOqU
Deutschland Vereidigung der Bundeskanzlerin
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Wakati  akianza kutumikia  muhula  wake  wa  nne madarakani, Merkel ameweka  wazi  kwamba  analenga kukiondoa  pia  chama  hicho. 

Katika mahojiano yake  ya  kwanza  makubwa  tangu alipochaguliwa  tena  siku  ya  Jumatano , kansela  Angela Merkel  alisema  moja  ya lengo  lake  kuu  katika  serikali mpya  ni  kuwavutia  wapiga  kura  kurejea  katika  kukipigia kura  chama  chake  ambao  wamepotelea  katika  chama hicho  cha  siasa  kali  za  mrengo  wa  kulia cha  Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD.

"Lengo  letu  ni  kutatua  matatizo  ya  wale  wapiga  kura waliopiga  kura  kwa  misingi  ya  upinzani," Merkel alisema katika  mahojiano  na  kituo  cha  televisheni  ya  taifa  cha ARD. 

"Hii  ina  maana , bila  shaka, nia  yake  ni  kupunguza idadi  yao  na  kuwaondoa  kutoka  bungeni," aliongeza.

Deutschland Bundestag Kanzlerwahl
Kansela Merkel akiwapokea mauwa kama ishara ya kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa kanselaPicha: Getty Images/AFP/O. Andersen

Alisisitiza, hata  hivyo, kwamba  lengo  kuu  la  serikali yake  ni  kutatua  matatizo  yanayowakumba  wapiga kura wa  Ujerumani.

Merkel apingwa

Merkel alichaguliwa  tena  kwa  muhula  wa  nne  kuwa kansela  kwa  wingi wa  kura  tisa  tu.

Licha  ya  kuwa  kura  ni  siri, matokeo yanaashiria  kwamba wabunge ndani  ya  muungano  wa  serikali  yake  pamoja na  kundi  la  wahafidhina  anaowaongoza  pamoja  na chama  cha  siasa  za  wastani  za  mrengo  wa  kushoto cha  Social Democratic SPD  walipiga  kura kumpinga.

Chama  cha  Merkel  cha  Christian Democtaric Union  CDU na  chama  cha  SPD vilipata  vipigo  katika  uchaguzi mkuu  wa  mwezi  Septemba , vikipoteza  wapiga  kura  kwa chama  cha  AfD. Chama  hicho  cha  siasa  kali  za mrengo  wa  kulia  kiliingia  katika  bunge , Bundestag kwa mara  ya  kwanza  baada  ya  kupata  asilimia  12.6 ya kura. Kwa  hivi  sasa  ndio  chama  kikuu cha  upinzani bungeni.

Wanasiasa  wa  chama  cha  AfD hususan  hawapendelei sera  za Merkel  kuhusu  wakimbizi  na  mara  kadhaa wametoa  mwito  wa  kuondolewa  Merkel  kutoka madarakani.

Deutschland Bundestag Kanzlerwahl
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akizungumza na makamu kansela anayeondoka madarakani Sigmar Gabriel Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Wakati  wa  upigaji  kura  bungeni  siku  ya  Jumatano, msaidizi  wa  mbunge  wa  chama  cha  AfD  alifukuzwa kutoka  katika  eneo  la  watazamaji  baada  ya  kufungua bango  ambalo  lilikuwa  limeandikwa  "Merkel  lazima aondoke."

Mbunge  mwingine  wa  chama  cha  AfD alitozwa  faini kwa  kutuma  picha  katika  mtandao  wa  kijamii  wa Twitter  wa  kura  yake  aliyopiga, akionesha  kwamba alipiga  kura  dhidi  ya  Merkel, pamoja  na  ujumbe : "Sio kansela wangu." Sheria  za  bunge  zinaeleza  kwamba kura ni  lazima  zibakie  kuwa  siri.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / English page

Mhariri: Daniel Gakuba