1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel amwonya Trump dhidi ya kuchochea vita vya biashara

Zainab Aziz
4 Julai 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel leo amemwonya rais wa Marekani Donald Trump baada ya rais huyo kutishia kwamba ataongeza ushuru kwa vipuri na magari yanayoingia nchini Marekani kutoka nchi za Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/30q8U
Kanada, Quebec: G7-Gipfel: Merkel kritisiert Trump
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Katika hotuba ya bungeni leo hii kansela Merkel alisema pande zote mbili zimo katika vita vya biashara tangu uamuzi wa Trump kuongeza ushuru ambao ni kama adhabu kwa uagizaji wa bidhaa za chuma na bati.

Bi Merkel amesema ni muhimu kuhakikisha kwamba mzozo uliopo kwa sasa kati ya pande hizo haupanuki na kuwa vita kamili.

Mnamo siku ya Jumapili Trump alidai kwamba Ulaya ni kama China kwa ubaya katika masuala yanayohusiana na biashara, huku akisema anatafakari kuongeza kodi ya asilimia 20 kwa magari yanayoingizwa Marekani kutoka nchi za Umoja wa Ulaya. Kwa upande wake Umoja wa Ulaya nao umesema utaongeza ushuru wa bidhaa za Marekani zikiwa ni pamoja na mvinyo wa bourbon, nguo za jeans na pikipiki za Harley and Davidson kujibu ushuru uliyowekwa na Marekani kwa bidhaa za chuma na bati kutoka Umoja wa Ulaya.

Bi Merkel akipinga malalamiko ya Turmp kuwa Umoja wa Ulaya na hasa nchi yake ya Ujerumani yenye nguvu kiuchumi, kwamba inapata ziada kubwa ya biashara dhidi ya Marekani, bibi Merkel amesema hesabu za Trump hazina muelekeo kwa sababu kimsingi anaangalia tu upande wa bidhaa, lakini hapigi hesabu za huduma.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/S. Gallup

Mahusiano kati ya Marekani na mataifa mengine yenye nguvu kiviwanda yamo kwenye mikwaruzo mikubwa tangu Trump alipoanzisha mpango wake wa "Marekani Kwanza" na kuwaadhibu washirika wake wa biashara, bila ya kujali kama wao ni washirika au wapinzani.

Huku kukiwa hakuna ishara ya kupatikana afueni katika mgogoro huo wa biashara kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya, rais wa halmashauri kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker anajiandaa kwenda mjini Washington mwishoni mwa mwezi huu wa Julai kutafuta njia ya kuondokana na vita hivi.

Wakati huo huo wizara ya fedha ya China imesema haitakuwa ya kwanza kufyatua risasi katika vita hivi vya biashara na Marekani na wala haitanza pia kuiwekea Marekani ongezeko la ushuru kabla haijafanyiwa hivyo na Marekani.

Marekani ilisema kwamba itatekeleza hatua yake ya kuongeza ushuru kwa bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 34 zinazoingizwa nchini mwake kutoka China ifikapo tarehe 6 mwezi huu na China imeapa kulipiza kisasi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Lu Kang amesema nchi yake iko tayari kutekeleza hatua hiyo, ingawa hakuthibitisha tarehe ya kuanza kwa ushuru mpya wa China dhidi ya Marekani.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFP/RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga