1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel amuonya Trump kuhusu kuhami masoko

Sekione Kitojo
15 Januari 2017

Kansela  wa  Ujerumani Angela  Merkel ameitaka  Marekani kuendelea  na  msimamo  wake  wa  ushirikiano  wa  kimataifa , akisema  utaratibu kuelekea kulinda  masoko  unahatarisha ufanisi.

https://p.dw.com/p/2Voya
Klausurtagung CDU-Bundesvorstand Angela Merkel
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Picha: Picture-Alliance/dpa/O. Dietze

Marekani  ni  mshirika  muhimu  sana  wa  kibiashara  wa  Ujerumani na  kauli  za  kuhami  masoko ya biashara  za  rais  mteule  wa marekani  Donald Trump zimewakera  wauzaji  wa  nje  katika  taifa hilo  lenye  uchumi  mkubwa  katika  bara  la  Ulaya.

Ujerumani  ni  rais  wa  kundi  la  G20  mwaka  huu  linalojumuisha mataifa 20  yenye  viwanda  na  yale  yanayoinukia  kiuchumi duniani, jukwaa  ambalo  Merkel  anataka  kulitumia  kulinda ushirikiano  wa  kimataifa.

Deutschland Auftakt Klausurtagung CDU-Bundesvorstand
Kansela Merkel akiwa na wajumbe waandamizi wa chama cha CDU Picha: picture-alliance/dpa/O. Dietze

Akizungumza  baada  ya  mkutano  wa  wajumbe  waandamizi  wa chama  chake  cha  siasa  za  wastani  za  mrengo  wa  kulia  cha CDU   katika  mji   wa  Perl-Nenning  magharibi  mwa  Ujerumani , Merkel  amesema  nchi  zote  zitafaidika  iwapo  zitafanyakazi  kwa pamoja  badala  ya  kujitenga.

USA Donald Trump Pressekonferenz in New York City
Rais mteule wa Marekani Donald TrumpPicha: Getty Images/AFP/D. Emmert

Mfano  mzuri  ulikuwa  juhudi  za  pamoja  za  kimataifa  baada  ya mzozo  wa  kiuchumi  duniani  ambao  ulianzia  nchini  Marekani mwaka  2008, Merkel  alisema.

Juhudi  za  pamoja

"Jinsi mzozo  wa  kifedha  ulivyoshughulikiwa  haikuwa jibu  ambalo lilikuwa  katika  misingi  ya  kujitenga, lakini  lilikuwa  jibu  ambalo lilikuwa  katika  msingi  wa  ushirikiano, sheria  za  pamoja  za udhibiti, ikiwa  ni  pamoja  na  masoko  ya  fedha," Merkel  alisema.

Akiulizwa  lini  atakutana  na  Trump  kwa  mara  ya  kwanza, Merkel alisema  mkutano unawezekana  wakati  wa  mkutano  wa  kilele  wa kundi  la  mataifa  saba   yenye  uchumi  mkubwa   duniani  yaani G7, ambao  utafanyika  Sicily  mwezi  Mei,  na  ule  wa  G20 utakaofanyika  nchini  Ujerumani  mwezi  Julai.

Deutschland G7-Gipfel 2015 in Elmau, Bayern
Mkutano wa kundi la G7 uliofanyika nchini Ujerumani 2015Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Katika  hotuba  yake  ya  kila  wiki , Merkel  alisema  uchumi  wa Ujerumani  unakwenda  vizuri, lakini  nchi  hiyo  haipaswi  kubweteka. Ameahimiza  makampuni  kuingia  katika  changamoto  ya  digitali.

"Pia  kuna  hatari  ya  kimataifa. Tunaona  hatua  za  kuhami masoko," Merkel  alisema , bila  kumtaja  Trump.

Viongozi  wa   makampuni  wamesema  uchumi  wa  Ujerumani unaweza  kuathirika  kutokana  na  sera  za  kibiashara  za  Marekani za  kuhami  masoko, na  kwamba  ukuaji  wa  kiuchumi  unaweza kuathirika.

Uchumi  wa  Ujerumani  umekua  kwa  asilimia  1.9  mwaka  2016, kasi  kubwa  kabisa  katika  miaka  mitano, wakati  ongezeko  la matumizi  ya  watu binafsi  na  serikali  vilisaidia  kuimarisha  nafasi yake  kama  injini  ya  ukuaji  wa  uchumi  katika  kanda  ya  sarafu ya  euro.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre / afpe

Mhariri: Zainab Aziz