1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel amkomalia Erdogan

Admin.WagnerD27 Juni 2013

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amesema ana furaha kuwa Uturuki inaweza kuanza tena mazungumzo ya kijuinga na Umoja wa Ulaya, lakini amesisitiza kuwa kwa Ulaya suala la haki za binaadamu halina mjadala.

https://p.dw.com/p/18xar
Merkel na Erdogan wakiwa mjini Berlin.
Merkel na Erdogan wakiwa mjini Berlin.Picha: Getty Images

Akizungumza bungeni hii leo, Kansela Merkel amesema Umoja wa Ulaya haukukaa kimya kana kwamba hakuna jambo lilitokea nchini Uturuki, na kuongeza kuwa matokeo ya mazungumzo baina ya Ankara na Umoja wa Ulaya, yameweka bayana kuwa Uturuki ni mshirika muhimu wa umoja huo, lakini haki za msingi zitaendelea kuheshimiwa daima.

"Uturuki ni mshirika wetu muhimu sana, lakini maadili yetu ya Ulaya - uhuru wa kuandamana, uhuru wa maoni, utawala wa sheria na uhuru wa kuabudu vinaheshimiwa daima, na havina mjadala," alisema Kansela Merkel.

Merkel na Erdogan wakiwa mjini Ankara, Uturuki.
Merkel na Erdogan wakiwa mjini Ankara, Uturuki.Picha: picture-alliance/dpa

Waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, anakabiliwa na changamoto kubwa zaidi katika utawala wake wa muongo mmoja, kufuatia maandamano ya kuipinga serikali yake, ambayo yameacha watu karibu 8,000 wakiwa wamejeruhiwa.

Uturuki ilianza mchakato wa kuomba uanachama wa umoja wa Ulaya mwaka 2005, lakini hadi sasa imeshakubaliana na umoja huo katika kipengele kimoja tu kati ya 35 vinavyohitajika ili kuiruhusu kujiunga na umoja huo. Ujerumani, ambayo ni dola yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, ni nyumbani kwa karibu watu milioni tatu wenye asili ya Uturuki, na pia ndiyo mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Uturuki.

Hakuna kutoa silaha kwa waasi wa Syria

Wakati huo huo, kansela Merkel amesema ingawa anafahamu haja ya kuwasaidia watu wa Syria wanaoteseka kutokana na vita vinavyoendelea nchini humo, nchini yake haiko tayari kutoa silaha kwa waasi. Merkel amesema mtu yeyote mwenye roho ya huruma anaweza kufahamu kwa nini mataifa ya magharibi yanataka kuwapatia silaha waasi, lakini alirudia msimamo wa nchi yake kutoshiriki zoezi hilo aliloliita la hatari.

Amesema aliweka wazi katika mkutano wa viongozi wa mataifa manane yalioendelea kiviwanda uliofanyika Ireland ya Kaskazini mwezi huu, kuwa Ujerumani itaendela kufanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuwasaidia watu wa Syria kuondokana na maafa yanayowakabili, na kubainisha kuwa serikali yake inatekeleza ahadi yake ya kutoa kiasi cha euro milioni 360 katika misaada ya kibinaadamu kwa watu wa Syria.

Kansela Merkel akizungumza bungeni Alhamisi 27.06.2013.
Kansela Merkel akizungumza bungeni Alhamisi 27.06.2013.Picha: picture-alliance/dpa

Kuhusu mfuko wa mshikamano wa Umoja wa Ulaya, Merkel amesema hana tatizo na mfuko huo, pale kanda ya sarafu ya euro itakapokubaliana juu ya sera ya pamoja ya uchumi na fedha. Lakini hakubainisha ni namna gani mfuko huo utafanya kazi, na alisisitiza kuwa inachokitaka Ulaya si mfuko mwingine bali kufanya mageuzi ya miundombinu. Alisema unachohitaji Umoja wa Ulaya hasa ni kuwekeza katika elimu na utafiti, ili kendelea kushindana kimataifa.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Nyiro Josephat Charo